Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 11 Desemba, 2020
Serikali inazingatia haki za binadamu na kupambana na rushwa katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuhakikisha taasisi za umma nchini zinatoa huduma bora kwa wananchi na bila upendeleo.
Hayo yamesemwa na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb) alipokuwa akitoa neno la utangulizi kabla
ya kumkaribisha Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Peter Pinda kwenye Kongamano
la Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu lililofanyika tarehe 10
Desemba, 2020 jijini Dodoma.
Mhe. Mkuchika amesema,
suala la haki za binadamu na mapambano dhidi ya rushwa ni mtambuka, ndio maana taasisi
zote zinazojishughulisha na utawala bora zimekutana na wadau wa sekta ya umma
na binafsi katika Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za
Binadamu mwaka huu ili kujadili na kutoa mapendekezo yatakayoboresha mapambano
dhidi ya rushwa na uzingatiaji wa haki za binadamu.
Mhe Mkuchika ameeleza
kuwa, uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za binadamu kwa mwaka
huu ulifanyika kwa kuzungumza na Waandishi wa Habari ili washiriki kutoa elimu
kwa umma dhidi ya rushwa na uzingatiaji wa haki za binadamu.
Taasisi zilizoshiriki
kuandaa maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu ni Ofisi ya Rais
Ikulu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Wizara
ya Katiba na Sheria,Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali, Mamlaka
ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma, Tume ya Utumishi wa Umma na Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora.
Kaulimbiu ya maadhimisho
ya mwaka huu ni “Uzingatiaji wa Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi na Watumishi kwa
Ustawi wa Utawala Bora na Haki za Binadamu nchini”.
Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe.
George Mkuchika (Mb) akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri
Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Peter Pinda kufungua Kongamano la Maadhimisho ya Siku
ya Maadili na Haki za Binadamu lililofanyika tarehe 10 Desemba, 2020 jijini
Dodoma.
Waziri Mkuu Mstaafu
Mhe. Mizengo Peter Pinda akizungumza na washiriki wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Maadili
na Haki za Binadamu lililofanyika tarehe 10 Desemba, 2020 jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki
wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu
wakimsikiliza Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Peter Pinda kabla ya kufungua
kongamano hilo.
No comments:
Post a Comment