Na. James K. Mwanamyoto
Tarehe 04
Disemba,2020
Serikali imeandaa Mfumo Mahsusi wa Kielektroniki wa Mpango wa
Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma (e-HRP) utakaowezesha Taasisi za Umma nchini
kusimamia Rasilimaliwatu vizuri na kupata takwimu sahihi za mahitaji ya
watumishi wake.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael wakati akifungua kikao kazi cha wadau kujadili mahitaji ya Mfumo wa Kielektroniki wa Mpango wa Rasilimaliwatu kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Rais Utumishi - Mtumba jijini Dodoma.
Dkt. Michael amefafanua kuwa, mfumo huo utawezesha kubaini mahitaji sahihi
ya Rasilimaliwatu kwa wakati wa sasa na baadae ili kuwa na mipango mahususi ya kiutumishi
pamoja na matumizi mazuri ya Rasilimaliwatu.
Ameongeza kuwa, matumizi ya mfumo huo utaziwezesha Taasisi za Umma kuwa
na watumishi wa kutosha, wenye sifa na uwezo unaotakiwa mahali pa kazi katika
utekelezaji wa majukumu ya taasisi zao.
Dkt. Michael amesisitiza kuwa, Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2008 imeelekeza kila Taasisi ya Umma kuwa na mpango wa kati na mpango wa kila mwaka wa Rasilimaliwatu kulingana na malengo yake kwani Mpango wa Rasilimaliwatu ni moja ya nyenzo muhimu katika Usimamizi na Menejimenti ya Watumishi.
Kikao kazi hicho cha siku moja kimewajumuisha Wasimamizi wa
Rasilimaliwatu kutoka katika Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali,
Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kitaiwezesha
Serikali kupata maoni ambayo yataboresha
Mfumo huo wa Kielektroniki wa Mpango wa Rasilimaliwatu katika
Utumishi wa Umma.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akifungua kikao
kazi cha wadau kujadili mahitaji ya Mfumo wa Kielektroniki wa Mpango wa Rasilimaliwatu
kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Rais Utumishi - Mtumba jijini Dodoma.
Wasimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka katika Wizara, Idara
Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa
na Mamlaka za Serikali za Mitaa, wakifuatilia mada kuhusu Mpango wa
Rasilimaliwatu iliyowasiliswa na Mkurugenzi Msaidizi Idara wa Mipango ya
Rasilimaliwatu Dkt. Edith Rwiza ili kutoa fursa kwa wadau hao kutoa maoni ya
kuboreresha Mfumo wa Kielektroniki wa Mpango wa
Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Dkt. Francis Michael akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao kazi cha
kujadili mahitaji ya Mfumo wa Kielektroniki wa Mpango wa Rasilimaliwatu
kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Rais Utumishi - Mtumba jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment