Na. James K. Mwanamyoto – Morogoro
Tarehe
22 Disemba, 2020
Watumishi
wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma wametakiwa kutekeleza majukumu
yao kwa kuzingatia maadili na uwajibikaji ili kutenda haki kwa kila mwombaji wa
ajira Serikalini ambaye ana sifa za kupata kazi kwa mujibu wa nafasi husika
zinazotangazwa na Taasisi mbalimbali za umma.
Wito
huo umetolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora Mhe. Kapt. (Mst) George H. Mkuchika (Mb) wakati akifungua
kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa
Umma kilichofanyika mjini Morogoro.
Mhe. Mkuchika
amewasisitiza watumishi hao kuendelea kuzingatia Uadilifu, Sheria, Kanuni na
Taratibu zinazosimamia Utumishi wa Umma nchini kwani kazi wanayoifanya ni nyeti
na inagusa maisha ya watu, hivyo inahitaji watu waadilifu, wapenda haki na
ambao ni mfano wa kuigwa na jamii kwa uadilifu.
Akizungumzia
utoaji wa huduma kwa wateja, Mhe. Mkuchika amesema, ni muhimu watumishi wa
Sekretarieti ya Ajira kuwahudumia wateja wao kwa lugha nzuri kwani ndio nyenzo
muhimu katika utoaji wa ajira.
“Tumieni
lugha nzuri na zenye staha kwa kuwasikiliza na kuwahudumia vizuri wateja wenu
kwani nyie ndio lango kuu la kuingiza watu katika Utumishi wa Umma, hivyo
mienendo yenu ndio picha ya aina ya watumishi watakaopatikana kwa ajili ya kuja
kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayofanywa na Serikali”,
Mhe. Mkuchika amefafanua.
Mhe.
Mkuchika amewahimiza watumishi hao, kufanya kazi kwa kushirikiana na waajiri
kwani jukumu walilopewa la kuendesha mchakato wa ajira ni kwa niaba ya waajiri
hivyo ni muhimu wakashirikiana kuhakikisha mchakato wa ajira unakwenda vizuri
na kwa wakati na hatimaye kupata watumishi wenye sifa stahiki ambao watalisukuma
gurudumu la maendeleo ya Taifa kwa kasi zaidi.
Aidha,
Mhe. Mkuchika amewataka watumishi wa Sekretarieti ya Ajira kurahisisha mchakato
wa ajira kwa kuongeza matumizi ya TEHAMA katika kuchuja waombaji wa kazi, hatua
hiyo ni kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais kuhimiza matumizi ya TEHAMA
ikizingatiwa kuwa, suala hili amelipa uzito mkubwa mpaka kuliundia Wizara.
Akizungumzia
kuhusu matumizi ya TEHAMA, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa
Umma Bw. Xavier Daudi amesema, Mifumo ya TEHAMA imeiwezesha ofisi yake
kuthibiti matumizi ya vyeti vya kughushi katika uendeshaji wa mchakato wa ajira
Serikalini kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine zenye dhamana katika sekta za
elimu na mafunzo katika zoezi la uhakiki.
Bw.
Daudi ameongeza kuwa, kupitia mifumo ya kiutendaji ya TEHAMA wamewawezesha
waombaji kazi kupata na kufuatilia taarifa za matangazo ya kazi kupitia teknolojia
rahisi ya simu za kiganjani popote alipo mteja ikiwemo mitandao ya kijamii
ambayo imewapunguzia adha wafuatiliaji wa fursa za ajira kwani taarifa
zinawafakia popote walipo.
Kuhusiana
na suala la uadilifu, Bw. Daudi amesema Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi
wa Umma imejiwekea malengo kuhakikisha wanaoajiriwa katika Taasisi za Umma wanakuwa na sifa ya uadilifu
na uwajibikaji.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Kapt.
(Mst) George H. Mkuchika (Mb) akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Ajira
katika Utumishi wa Umma wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la
ofisi hiyo kilichofanyika jana mjini Morogoro.
Baadhi
ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Sekretarieti ya Maadili katika Utumishi
wa Umma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora Mhe. Kapt. (Mst) George H. Mkuchika (Hayupo pichani)
wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la ofisi hiyo kilichofanyika
jana mjini Morogoro.
Katibu
wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Kapt. (Mst) George
H. Mkuchika (Hayupo pichani) kabla ya Waziri huyo kufungua kikao cha Baraza la
Wafanyakazi la ofisi hiyo kilichofanyika jana mjini Morogoro.
Katibu
Tawala Mkoa wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Kalobelo akitoa neno la
shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Mhe. Kapt. (Mst) George H. Mkuchika mara baada ya Waziri huyo
kufungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Sekretarieti ya Ajira katika
Utumishi wa Umma kilichofanyika jana mjini Morogoro.
No comments:
Post a Comment