Saturday, July 22, 2023

MHE.KIKWETE : TAALUMA YA UUGUZI NI YA KUJITOA NA YENYE UTHUBUTU

Na. Lusungu Helela-Chalinze

Tarehe 22 Julai, 2023 

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema taaluma ya Uuguzi ni kazi ya uthubutu, utayari pamoja na kujitoa kwa ajili ya kuwahudumia  wenye mahitaji ya kiafya huku akiwataka Wauguzi kuendelea kuchapa kazi  kwa weledi na kwa kuzingatia miiko na maadili ya taaluma yao. 

Mhe. Kikwete ameyasema hayo leo Jumamosi Julai 22, 2023 wakati akizungumza na Wauguzi wa Mkoa wa Pwani kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ambapo amewahimiza Wauguzi hao kuwahudumia wananchi kwa moyo na upendo wa hali ya juu. 

Amesema, Serikali inatambua kuwa Wauguzi ni kundi muhimu sana  kwani  ndio shina na mhimili mkubwa wa utendaji na ufanisi wa sekta ya afya nchini na ulimwenguni kote. 

Mhe. Kikwete ametumia fursa hiyo kumshukuru  Rais  wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi Wauguzi hao ikiwa ni pamoja na  kuweka mikakati mbalimbali ili kuyafikia malengo endelevu ya afya kwa wote. 

Aidha, Mhe. Kikwete amesema Ofisi ya Rais-UTUMISHI inaendelea kuzifanyia kazi changamoto za kimuundo za taaluma hiyo na changamoto nyingine itaishirikisha Wizara husika ya Afya ili ziweze kufanyiwa kazi. 

Katika hatua nyingine, Mhe. Kikwete amekubali ombi la kuwa mlezi wa Wauguzi katika Mkoa wa Pwani huku akiahidi kuwapa ushirikiano ili kuwaongezea morali Watumishi hao katika kutekeleza majukumu yao. 

‘’Natambua mchango wenu adhimu kwa mustakabali wa afya zetu kwani ziko mikononi mwenu, napenda kuwaahidi mimi kama mlezi wenu niko tayari kuwapa ushirikiano muda wote mtakaponihitaji” amesisitiza Mhe, Kikwete. 

Awali Katibu wa Chama cha Wauguzi Mkoa wa Pwani, Bi, Dafroza Mnzava akisoma risala kwa Naibu Waziri Mhe. Kikwete, ameiomba Serikali kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili ikiwemo suala la muundo na posho ya mazingira hatarishi na stahiki mbalimbali. 

Pia Katibu huyo ameiomba Serikali kuendelea kuajiri wauguzi ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. 

Maadhimisho hayo yenye kauli mbiu WAUGUZI WETU, MUSTAKABALI WA AFYA ZETU” yamefanyika mkoani humo ikiwa ni kuenzi kumbukumbu ya Muasisi wa Uuguzi na Ukunga Duniani, Bi. Florence Nightingale wa nchini Italia, aliyejitoa kwa moyo kuwahudumua wenye mahitaji ya kiafya.  



Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akikabidhi zawadi kwa Mariam Moyo aliyejifungua katika Wodi ya Wazazi iliyopo katika Hospitali ya Chalinze mkoani Pwani ikiwa ni shamrashamara ya Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani iliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Wauguzi wa Mkoa wa Pwani kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani ambapo amewahimiza Wauguzi hao kuwahudumia wananchi na jamii yote ya Kitanzania kwa moyo na upendo wa hali ya juu. 


Sehemu ya Wauguzi wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati akizungumza nao kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani ambapo amewahimiza Wauguzi hao kuwahudumia wananchi na jamii yote ya Kitanzania kwa moyo na upendo wa hali ya juu.


Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Wauguzi mara baada ya kukabidhi zawadi mbalimbali kwenye Wodi ya Wazazi katika Hosiptali ya Chalinze ikiwa ni katika kuadhimisha Siku ya Wauguzi Duniani iliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani.


Wauguzi wakiwa katika maandamano wakiadhimisha Siku ya Wauguzi Duniani iliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani na kupokelewa maandamano hayo na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akiwa na baadhi ya Viongozi na Wauguzi wakielekea katika Wodi ya Wazazi kwa ajili ya kuwajulia hali pamoja na kuwapatia zawadi mbalimbali kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akiwa ameshika mshumaa na baadhi ya Wauguzi katika shamrashamara ya kuadhimisha  Siku ya Wauguzi Duniani iliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani.


Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mganga Mkuu wa mkoa wa Pwani, Dkt. Gunini Kamba akizungumza na Wauguzi wa Mkoa wa Pwani kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani iliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani.


 

Thursday, July 20, 2023

MHE.SIMBACHAWENE ATAKA NGUVU ZA WANANCHI KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA KIMKAKATI

Na Lusungu Helela-Kibakwe

Tarehe 20 Julai, 2023                           

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene, amewataka wananchi kuibua miradi ya kimkakati katika maeneo yao ili Serikali iweze kusaidia katika ukamilishaji wa miradi hiyo.              

Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi kwa nyakati tofauti katika Kata ya Luhundwa, Lufu, Wangi na Wotta, Wilayani Mpwapwa, Mkoani Dodoma kupitia mikutano ya hadhara katika Vijiji vya Jimbo la Kibakwe, ikiwa ni muendelezo wa kuelezea mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Amesema Serikali inavutiwa na uongozi wenye maono na mtazamo wa kimapinduzi kwa kuanza kusaidia pale nguvu za wananchi zilipoishia ili kuistawisha jamii hiyo.  

Ametolea mfano wa miradi hiyo ya kimkakati kuwa ni ujenzi wa shule, zahanati, nyumba za watumishi pamoja na ujenzi wa kumbi za mikutano.   

“Viongozi na watendaji mna kazi kubwa ya kuhakikisha wananchi wanashiriki katika ujenzi wa miradi ya maendeleo, kwani wenye uhitaji ni sisi hatutegemei kuona nyie mpo nyuma katika kutekeleza miradi hiyo. Kila mmoja ana wajibu wa kuchangia na kuona miradi inakamilika kwa wakati na kusimamia matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali.” Amesisitiza Mhe. Simbachawene. 

Amefafanua kuwa, Serikali ina vipaumbele vingi, hivyo nguvu za wananchi katika kuchangia miradi ya maendeleo haiepukiki. 

Ameongeza kuwa, jamii inayojitegemea hujipatia heshima, hivyo kitendo cha vijiji hivyo kubuni na kutekeleza miradi ya maendeleo yake kunaleta heshima kwa viongozi na wananchi kwa ujumla. 

Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Simbachawene amepongeza jitihada za viongozi na watendaji wa Kata ya Wangi na Wotta kwa kubuni miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa zahanati na ofisi za Mwenyekiti wa Kijiji, kisha kuiomba Serikali isaidie kukamilisha ujenzi huo. 

“Wananchi mkileta ndoo ya maji au mchanga inahesabika mmechangia, mchango sio lazima fedha" amesisitiza

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kusaidia kukamilisha kwa haraka miradi iliyobuniwa na wananchi kwani kwa kufanya hivyo kutachochea ushindani wa maendeleo katika jamii. 

Katika hatua nyingine, Mhe.Simbachawene ametoa wito kwa Viongozi wa Kata nyingine kubuni na kutekeleza miradi kwa kutumia nguvu za wananchi katika maeneo yao ili kuichochea Serikali kuwaongezea nguvu katika hatua za ukamilishaji.  

Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Mhe. George Fuime amesema wataangalia uwezekano wa kutenga fedha za kumalizia ujenzi wa ofisi ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Lwihomelo kwa nia ya kuunga mkono shughuli zinazofanywa na wananchi wa Kijiji hicho. 

"Mhe. Waziri tutajitahidi katika kuhakikisha fedha zinatengwa kwa ajili ya kuunga mkono nguvu za wananchi katika masuala ya maendeleo yaliyobuniwa na wananchi wenyewe, amesema Mhe. Fuime.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kidenge katika Kata ya Luhundwa wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi hao Wilayani Mpwapwa, Mkoani Dodoma, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma uliolenga kuwahamasisha wananchi katika kuibua miradi ya kimkakati katika maeneo yao ili Serikali iweze kusaidia katika ukamilishaji wa miradi hiyo na kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.


Wananchi wa Kijiji cha Kidenge wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene alipokuwa akizungumza nao wakati ziara yake ya kikazi katika Kata ya Luhundwa Wilayani Mpwapwa, Mkoani Dodoma, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma uliolenga kuwahamasisha wananchi katika kuibua miradi ya kimkakati katika maeneo yao ili Serikali iweze kusaidia katika ukamilishaji wa miradi hiyo na kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

 

Tuesday, July 18, 2023

WANANCHI WA JIMBO LA KIBAKWE WAMUOMBA WAZIRI SIMBACHAWENE KUSAIDIA KUREKEBISHA MCHAKATO WA KUWAPATA WALENGWA WA TASAF

 Na. Lusungu Helela-Kibakwe

Tarehe 18 Julai, 2023 

Wananchi wa Kata ya Malolo iliyopo Jimbo la Kibakwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa wamepaza sauti zao kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene wakimuomba asaidie kubadili mchakato wa kuwapata walengwa halisi wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) huku wakisisitiza kuwa utaratibu unaotumika kwa sasa umegubikwa na sintofahamu.

Aidha, Wananchi hao wamewataka walengwa wa Mpango huo ambao tayari wameimarika kiuchumi kuwa na utu kwa kujiondoa na kuwapisha wengine wanaostahili kuingizwa kwenye Mpango.

Hayo yamesemwa na Wananchi mbalimbali kwa nyakati tofauti kupitia mikutano ya hadhara ya Waziri huyo anayoendelea kuifanya katika Vijiji vya Jimbo la Kibakwe ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambapo wananchi hao wameomba ubainishaji huo wa walengwa ufanyike kwa uwazi ikiwezekano kupitia mikutano ya hadhara ili waweze kuwapata walengwa halisi.

Wamefafanua kuwa licha ya TASAF kuwashirikisha viongozi wa vijiji husika katika kuwabaini Walenga halisi lakini bado hawaridhishwi na jinsi mchakato unavyoendeshwa kwani kuwekuwa na usiri wa hali ya juu.

Wamesema kuwa mchakato huo katika ngazi za vijiji haufanyiki vizuri hivyo kupelekea wale ambao sio maskini halisi kuwa wanufaika ilhali wale maskini halisi wakiendelea kutaabika.

Malalamiko hayo ya wananchi yalitokana na maswali ya Mhe. Simbachawene ya kutaka kuwatambua walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kata hiyo ya Malolo na namna walivyopatikana ili kujiridhisha na minongóno aliyoisikia juu ya upatikanaji wa walengwa hao.

Akijibu malalamiko hayo, Waziri Simbachawene amesema tayari ameshatoa maelekezo kwa Menejimenti ya TASAF Makao Makuu kuangalia namna bora ya kuwapata walengwa halisi wa Mpango.

Ameongeza kuwa TASAF msingi wake ni mpango shirikishi wa kuondoa umasikini uliokithiri kwa wananchi, hivyo ni lazima kutafuta njia sahihi ili  kutimiza azma ya kuanzishwa kwake.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nzugilo wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi hao katika Kijiji hicho, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma uliolenga kuwasikiliza wananchi wa kijiji hicho kuhusiana na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.


Sehemu ya wananchi wa Kijiji cha Nzugilo wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene alipokuwa akizungumza nao wakati ziara yake ya kikazi katika kijiji hicho, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma uliolenga kuwasikiliza wananchi wa kijiji hicho kuhusiana na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ambaye pia ni Diwani wa Mpwapwa Mjini, Mhe. George Fuime akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha Nzugilo wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji hicho, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma uliolenga kuwasikiliza wananchi wa kijiji hicho kuhusiana na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa na wananchi wa Kijiji cha Nzugilo ambao wanakijiji wenzao waliwabaini kuwa wanastahili kuingizwa kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) lakini wameachwa.

 

 



Sunday, July 16, 2023

WAZIRI SIMBACHAWENE ATOA WITO KWA KANISA LA KKKT USHARIKA WA KIBAKWE KUJITANUA ZAIDI KWA MAENDELEO YA TAIFA

Na. Lusungu Helela-Kibakwe

Tarehe 16 Julai, 2023 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) tangu kuanzishwa kwake katika Usharika wa Kibakwe limekuwa neema na baraka kubwa kwa wakazi wa eneo hilo huku akisema limeleta mapinduzi makubwa kiuchumi na kifikra kwa wananchi. 

Waziri Mhe. Simbachawene ameyasema hayo leo Jumapili Juni 16, 2023 alipokuwa akizungumza na Viongozi wa Dini na Washarika katika Ibada Takatifu ya kumwingiza kazini Mkuu wa Jimbo la Kibakwe, Dayosisi ya Dodoma ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mchungaji Emanuel Milangasi iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Dodoma, Christian Ndossa katika usharika wa Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma. 

Amesema Kanisa hilo limekuwa chachu kwa Wakazi wa Kibakwe na wengine katika suala zima la maendeleo na hivyo kumpelekea yeye kama Mbunge wa Jimbo hilo na Waziri anayeshughulikia masuala ya utawala bora kupata urahisi pindi anapohamasisha masuala ya maendeleo. 

Akitolea mfano kuwa tangu kuanzishwa kwa Kanisa hilo limekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma za kiroho na kijamii kwa Washarika hao. 

Aidha, Mhe. Simbachawene amesema Kanisa hilo limeleta umoja na mshikamo katika jamii kupitia mafundisho yake ambayo yamejikita kwenye kuhubiri upendo. 

"Ukizungumzia maendeleo ya Jimbo la Kibakwe huwezi kuacha kulitaja Kanisa la KKKT la Usharika wa Kibakwe" amesema Mhe. Simbachawene. 

Amefafanua kuwa Kanisa hilo limeleta mageuzi makubwa katika Jimbo hilo ikiwa ni pamoja  na kuwa wamiliki wa mwanzo kabisa wa Nyumba ya kulala na kutumia nishati ya jua kwa ajili ya kusambaza huduma ya maji kwa wananchi. 

Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Simbachawene ameliomba Kanisa hilo kuendelea kuwekeza zaidi katika kutoa huduma za jamii ikiwemo ujenzi wa kituo cha watoto yatima pamoja na shule. 

Aidha, Mhe. Simbachwene ametumia fursa hiyo kumhakikishia Mkuu huyo mpya wa Jimbo, Mchungaji Emanuel Milangasi kuwa atampa ushikirikiano kwa lengo la kuijenga Kibwake mpya yenye hofu ya Mungu na yenye uchumi endelevu. 

Hata hivyo Mhe. Simbachawene amewasihi Washarika hao kumpa ushikiano Mchungaji huyo ili aweze kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma ya kiroho kwa Washarika kama ilivyokusudiwa.    

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Dodoma KKKT, Christian Ndossa amemshukuru Waziri Simbachawene kwa kukubali kushiriki katika Ibada hiyo Takatifu katika Usharika wa Kibakwe huku akimhakikishia kuwa watazidi kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuendelea kutekeleza majukumu yake mazito aliyo nayo kwa maslahi mapana ya kitaifa. 

Pia, Askofu Christian Ndossa amemtakia majukumu mema katika kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kufikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwaletea maendeleo Watanzania. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na Viongozi wa Dini na Washarika katika Ibada Takatifu ya kumwingiza kazini Mkuu wa Jimbo la Kibakwe, Dayosisi ya Dodoma ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mchungaji Emanuel Milangasi iliyofanyika leo katika usharika wa Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma.


Sehemu ya Viongozi wa Dini na Washarika wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa Ibada Takatifu ya kumwingiza kazini Mkuu wa Jimbo la Kibakwe, Dayosisi ya Dodoma ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mchungaji Emanuel Milangasi iliyofanyika leo katika usharika wa Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma.


Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Askofu Christain Ndossa, akiongoza Ibada Takatifu ya kumwingiza kazini Mkuu wa Jimbo la Kibakwe, Dayosisi ya Dodoma ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mchungaji Emanuel Milangasi iliyofanyika leo katika usharika wa Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (aliyekaa katika mstari wa mbele) akifuatilia Ibada Takatifu ya kumwingiza kazini Mkuu wa Jimbo la Kibakwe, Dayosisi ya Dodoma ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mchungaji Emanuel Milangasi iliyofanyika leo katika usharika wa Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma.


Wanakwaya wakiimba wakati wa Ibada Takatifu ya kumwingiza kazini Mkuu wa Jimbo la Kibakwe, Dayosisi ya Dodoma ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mchungaji Emanuel Milangasi iliyofanyika leo katika usharika wa Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Dini wakati wa Ibada Takatifu ya kumwingiza kazini Mkuu wa Jimbo la Kibakwe, Dayosisi ya Dodoma ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mchungaji Emanuel Milangasi iliyofanyika leo katika usharika wa Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisalimiana na Mkuu wa Jimbo la Makao Makuu na Mchungaji Kiongozi Usharika wa Arusha Road, Mchungani Lucy Semsungu wakati wa Ibada Takatifu ya kumwingiza kazini Mkuu wa Jimbo la Kibakwe, Dayosisi ya Dodoma ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mchungaji Emanuel Milangasi iliyofanyika leo katika usharika wa Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma.

 


 

Saturday, July 15, 2023

MHE. KIKWETE AWAELEKEZA MAAFISA UTUMISHI KUTOCHELEWESHA KUWASILISHA OFISI YA RAIS-UTUMISHI VIBALI VYA MAOMBI YA WATUMISHI WANAOSTAHILI KUPANDA MADARAJA

Na. Veronica Mwafisi-Bagamoyo

Tarehe 15 Julai, 2023

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka Maafisa Utumishi wote kuhakikisha maombi yote ya watumishi wa umma nchini wanaostahili kupanda madaraja yanawasilishwa katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya  Utumishi wa Umma  na Utawala Bora ili yaweze kushughulikiwa kwa wakati kwa lengo la kutenda haki na kuondoa malalamiko yasiyokuwa na ulazima.

Mhe. Kikwete amesema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji na kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.

“Serikali imeshatoa maelekezo ya kuwasilisha maombi ya watumishi wa umma wanaostahili kupanda madaraja ili yafanyiwe kazi, hivyo Afisa Utumishi hakikisha unahakiki vizuri na kuwasilisha maombi ya kupandishwa madaraja kwa watumishi hawa,” amesisitiza Mhe. Kikwete.

Mhe. Kikwete amesema kuwa, Serikali inayoongozwa na Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan haina tatizo katika suala la kutafuta mafungu ya fedha kwa ajili ya kuwapa watumishi wake stahili zao ili waweze kufanya kazi vizuri.   

Mhe. Kikwete amesema kuwa, Mhe. Rais Dkt. Samia anataka watumishi wake wawe na ari ya kufanya kazi kwani kukiwepo na manung’uniko itaondoa morali ya kufanya kazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Shauri Selenda, amemshukuru Naibu Waziri Kikwete kwa kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi hao kwa ajili ya kuzifanyia kazi.  

Aidha, Mkurugenzi Selenda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa stahiki mbalimbali za watumishi ikiwemo upandishwaji vyeo, ubadilishwaji kada, ajira mpya, vibali vya uteuzi, ulipaji wa malimbikizo ya mishahara, fedha za matibabu, mafao ya uzazi, fidia za watumishi wanaoumia kazini, pamoja na kuboresha vitendea kazi na maeneo ya kazi.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya watumishi wengine, Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bw. George Mwalukasa ametoa ahadi kwa Mhe. Naibu Waziri Kikwete kuwa watatekeleza maelekezo yote ambayo amewaagiza na kuhakikisha kwamba watumishi wote waliokuwa na changamoto za madaraja wanapatiwa ufumbuzi kama Serikali ilivyoelekeza.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amehitimisha ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Pwani iliyokuwa na lengo ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani wakati wa ziara yake ya kikazi katika mkoa huo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.


Sehemu ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa halmashauri hiyo.


Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Mhe. Muharami Mkenge akitoa salamu za wananchi na watumishi wa jimbo la Bagamoyo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.


Mtumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani Mwalimu Belloh Mkwazu (Aliyesimma) akiwasilisha hoja kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo mkoa wa Pwani iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (katikati) akisikiliza hoja iliyokuwa ikiwasilishwa kwake na Mtumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo mkoa wa Pwani iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.


Afisa Utumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani Bw. George Mwalukasa akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) mara baada ya Naibu Waziri huyo kuhitimisha kikao kazi chake na watumishi wa halmashauri hiyo kilicholenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.



   

WAZIRI SIMBACHAWENE AWATAKA VIONGOZI KUSIKILIZA MALALAMIKO YA WATUMISHI

 Na. Lusungu Helela-Mpwapwa

Tarehe 15 Julai, 2023

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewataka viongozi wa ngazi za Wilaya na Halmashauri zote nchini kujenga utamaduni wa kusikiliza na kufanyia kazi malalamiko mbalimbali ya Watumishi wa Umma  huku akisema kiu yake ni kuona watumishi  hao wakifurahia kuwa Watumishi wa Wananchi. 

Waziri Simbachawene ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya  Mpwapwa mkoani Dodoma, ambapo amesema yeye kama kiongozi anatambua watumishi wanakabiliwa na changamoto lukuki na hawana sehemu ya kusemea. 

Amesema watumishi waliokata tamaa hawawezi kutoa huduma bora kwa wananchi huku akisisitiza kuwa hali hiyo imekuwa ikiwaumiza wananchi na kuifanya serikali iliyopo madarakani kuchukiwa kwa matatizo yao kutopatiwa ufumbuzi.

Amefafanua kuwa anataka kuona watumishi wa umma wakipata stahiki zao lakini na wao wakitekeleza majukumu yao ipasavyo.

Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Simbachawene amewataka Makatibu Tawala wa Wilaya nchini ambao ndio wakuu wa utumishi wa umma katika ngazi ya wilaya kutekeleza majukumu yao kwa kusikiliza vilio na malalamiko ya watumishi walio chini yao. 

"Watumishi waliochukia na wenye malalamiko hawawezi kuleta matokeo chanya ambayo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anakusudia, hivyo Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri na Katibu Tawala wa Wilaya shughulikieni matatizo ya watumishi" amesisitiza Mhe. Simbachwene.

Aidha, Mhe. Simbachawene amesema  Watumishi wa Umma wanaokiuka misingi ya utumishi wa umma akitolea mfano ulevi kazini ni vizuri wakawa wanaonywa kabla ya kuadhibiwa ikizingatiwa sasa hivi waajiriwa wengi ni vijana sana hivyo wanachohitaji ni malezi pekee.

Katika zoezi hilo la kusikiliza malalamiko ya watumishi, miongini mwa malalamiko yaliyotewa kwa wingi na watumishi hao ni kuchelewa kulipwa malimbikizo yao ya mishahara, kupandishwa madaraja, kuchelewa kulipwa fedha za uhamisho pamoja na kubambikiwa mikopo. 

Naye Mkuu wa wilaya ya Mpwapwa, Mhe. Sophia Kizigo amesema yeye na timu yake chini ya Katibu Tawala wa Wilaya watajipanga kusikiliza malalamiko ya watumishi ili kuhakikisha watumishi wa Mpwapwa wanaifurahia kazi yao.

Hata hivyo, Mhe. Kizigo ametumia fursa hiyo kuwaasa Watumishi wa Umma kuacha kukopea mshahara wote hali inayoufanya utumishi wa umma kudharauliwa kupelekea mtumishi kuishi maisha magumu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.


Sehemu ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa halmashauri hiyo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Bi. Mwanahamsi Ally Mara baada ya kuwasili katika halmashauri hiyo kwa ziara ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa halmashauri hiyo. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Mhe. Sophia Kizigo.



Friday, July 14, 2023

MHE. KIKWETE AWAPONGEZA VIONGOZI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA BAGAMOYO KWA KUSIMAMIA NA KUWAHUDUMIA VIZURI WALENGWA WA TASAF

 Na. Veronica Mwafisi-Bagamoyo

Tarehe 15 Julai, 2023

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewapongeza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kwa kusimamia na kuwahudumia vizuri walengwa wa Mradi wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao kwa asilimia kubwa umeinua maisha ya wananchi wa eneo hilo.

Mhe. Kikwete ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi na walengwa wa TASAF wa Kata ya Dunda, Kijiji cha Dunda katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.

“Kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora niwapongeze ninyi viongozi wa Halmashauri ya Bagamoyo kwa kujitoa kwenu katika kuwasimamia na kuwahudumia wananchi wa eneo hili la Bagamoyo,” Mhe. Kikwete amesema.

Mhe. Kikwete amesema kuwa, endapo halmashauri zote nchini Tanzania zitasimamia na kuratibu mradi wa TASAF kwa usahihi kama ambavyo halmashauri ya Bagamoyo inafanya, ifikapo mwaka 2026 nchi ya Tanzania itakuwa imeondokana na tatizo la wananchi kuwa na hali duni za maisha.

Aidha, Mhe. Kikwete amewataka wananchi na walengwa wa halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kumuombea Rais Mhe. Dkt. Samia Hassan kwa kuwa anafanya kazi kubwa ya kuhakikisha kila mwananchi anainuka kutoka katika hali duni na kuwa na maisha bora.

Kwa upande wake, mlengwa wa TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Mwanahawa Sobbo ameishukuru TASAF kwa kumuinua kimaisha na kumuunganisha na vikundi ambavyo vimemsaidia kupata mkopo wa Halmashauri ya Wilaya ambao umewawezesha kununua machine ya boti inayofanya biashara na kuwaingizia kipato kikubwa.

Naye, Mlengwa mwingine wa TASAF, Bi. Mwanaheri Maulidi ametoa shukrani kwa Serikali kupitia mradi wa TASAF kwa kuinua maisha yake kwani ruzuku ambayo alikuwa akiipokea ilimuwezesha kusomesha watoto wake pamoja na kupata ada yake ya kwenda kujifunza ufundi cherehani.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amehitimisha ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Pwani iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao pamoja na kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na wananchi na walengwa wa TASAF wa Kata ya Dunda, Kijiji cha Dunda katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.


Sehemu ya wananchi na walengwa wa TASAF wa Kata ya Dunda, Kijiji cha Dunda, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) wakati akizungumza nao alipokuwa kwenye ziara ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika halmashauri hiyo.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Shauri Selenda akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete kuzungumza na wanachi na walengwa wa TASAF wakati wa ziara yake ya kikazi katika Halmashauri hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.


Mlengwa wa TASAF, Bi. Mwanaheri Maulidi akitoa ushuhuda kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete namna TASAF ilivyomsaidia kuinua maisha yake wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akitazama baadhi ya bidhaa za walengwa wa TASAF katika Kata ya Dunda, Kijiji cha Dunda, Wilaya ya Bagamoyo wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.