Na. Veronica E. Mwafisi-Kigamboni
Tarehe 14 Disemba, 2022.
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi amewataka waajiri katika Taasisi za Umma kuhakikisha
wanatatua changamoto ya upungufu wa watumishi katika baadhi ya kada kwa
kuwabaini watumishi wenye ujuzi wa kada hizo na kuwaendeleza kielimu ili wapate
sifa ya kuziba nafasi wazi na hatimaye kutatua changamoto hiyo ya uhaba wa
watumishi, badala ya kuisubiri Serikali kutatua changamoto hiyo.
Akizungumza na Watumishi wa
Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Mhe. Ndejembi amesema, waajiri wanapaswa
kubaini watumishi wenye ujuzi na sifa ili kuwajengea uwezo kiutendaji kupitia
programu za mafunzo kwani watakapohitimu watarejea katika vituo vyao vya kazi wakiwa
na ujuzi na elimu itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa,
Serikali inaajiri watumishi kulingana na bajeti iliyopangwa katika mwaka wa
fedha husika, kwa mantiki hiyo, bajeti inaweza kutokidhi kuajiri watumishi kulingana
na uhitaji, hivyo waajiri wanayo nafasi ya kuisaidia Serikali kutatua
changamoto ya uhaba wa watumishi kwa kuwaendeleza baadhi ya watumishi
watakaosaidia kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi kwenye kada zenye
uhitaji.
Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka
waajiri kutowakaimisha nafasi watumishi wasio na sifa na utaalamu wa kazi katika
kada wanazotakiwa kuzisimamia, na kuongeza kuwa ni muhimu kwa watumishi wanaokaimishwa
kuwa na sifa na uwezo utakaowasaidia kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Bw. Erasto Kiwale amemshukuru Mhe.
Ndejembi kwa kufanya ziara ya kikazi katika halmashauri hiyo na kuhimiza
uwajibikaji, kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi, kutatua kero pamoja
na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili watumishi wa halmashauri yake.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi anaendelea
na ziara yake ya kikazi jijini Dar es salaam yenye lengo la kuhimiza
uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa
Kuzinusuru Kaya Maskini nchini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
(TASAF).
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Kigamboni (hawapo
pichani), akiwa katika ziara yake ya kikazi yenye lengo kuhimiza uwajibikaji na
kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma walio katika Wilaya hiyo.
Sehemu ya Watumishi wa Umma
wa Wilaya ya Kigamboni
wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani), alipokuwa
akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji
na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Bw. Erasto Kiwale akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi mara baada ya kuzungumza na
watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni wakati wa ziara ya kikazi ya
Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto
zinazowakabili watumishi wa umma walio katika Wilaya hiyo.
Afisa Hesabu Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Bi. Neema Masanja akiwasilisha hoja kwa Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi (hayupo pichani), wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu
Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto
zinazowakabili watumishi wa Wilaya ya Kigamboni.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati)
akisikiliza hoja iliyokuwa ikiwasilishwa na Mtumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, wakati wa ziara yake
ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili
watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa hiyo. Kushoto kwake ni Mkuu wa
Wilaya ya Kigamboni Mhe. Fatma Nyangasa na kulia kwake ni Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Bw. Erasto Kiwale.
No comments:
Post a Comment