Na. Veronica E. Mwafisi-Kinondoni
Tarehe 13 Disemba, 2022
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi amesema likizo za mwaka kwa watumishi wa umma katika
kipindi cha sikukuu zisiwe kikwazo cha kutoa huduma kwa wananchi.
Akizungumza na Watumishi wa
Umma wa Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Mhe. Ndejembi amesema, likizo
ya mwaka ni haki ya mtumishi lakini inatakiwa kuchukuliwa kwa tahadhari hasa
katika kipindi cha sikukuu ili isiathiri utoaji wa huduma kwa wananchi
wanaofuata huduma katika taasisi za Serikali.
Mhe. Ndejembi amesema
watumishi wanapochukua likizo kipindi cha sikukuu, ni vema baadhi wakabaki
ofisini ili kuendelea kutoa huduma kama kawaida kwani wananchi wanahitaji
huduma nyakati zote za sikukuu na za kawaida.
“Tuhakikishe huduma zinatolewa kama kawaida katika
vituo vyetu vya kazi katika kipindi hiki cha Sikukuu kama zinavyotolewa katika
siku za kawaida kwani serikali hailali, hufanya kazi wakati wote,” Mhe. Ndejembi
amesisitiza.
Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka
watumishi wa umma nchini kujitathmini kiutendaji kwa kujiwekea malengo kupitia
watumishi binafsi, Idara na Taasisi kwa ujumla katika kutekeleza majukumu yao
ya kuwahudumia wananchi ili kuunga mkono kwa vitendo Kaulimbiu ya Kazi Iendelee ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake, Katibu Tawala
wa Wilaya ya Kinondoni, Bi. Stella Msofe amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuhimiza
uwajibikaji, kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwa ni
pamoja na kutatua kero na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili watumishi
walio katika wilaya yake.
Bi. Msofe, ameahidi kusimamia
utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Naibu Waziri aliyoyatoa kwa watumishi kwa
kushirikiana na wasaidizi wake kuanzia ngazi ya Kata, Mtaa na Halmashauri kwa
ujumla.
Naye, Mtumishi wa Manispaa ya
Kinondoni, Bi. Happyfania Mabala amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kutoa ufafanuzi
wa masuala mbalimbali ya kiutumishi, ikiwa ni pamoja na kutatua kero na
changamoto zilizokuwa zikiwakabili watumishi wa Halmashauri hiyo kwa muda mrefu.
Kadhalika, Bi. Mabala ameushukuru
uongozi wa Wilaya yake kwa kuwakaribisha viongozi mbalimbali na kuzungumza nao
masuala ya kiutumishi, jambo ambalo linawaongezea ari kubwa katika utendaji
kazi wao kupitia utumishi wa umma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameanza
ziara ya kikazi jijini Dar es salaam yenye lengo kuhimiza uwajibikaji kwa
watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya
Maskini nchini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Kinondoni, jijini
Dar es Salaam (hawapo pichani), akiwa katika ziara yake ya kikazi yenye lengo
la kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma
walio katika Wilaya hiyo.
Sehemu ya Watumishi wa
Umma wa Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam wakimsikiliza
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
(hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi
iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa
Wilaya hiyo.
Katibu
Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Bi. Stella Msofe akitoa neno la utangulizi kabla
ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza
na watumishi wa Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es salaam (hawapo pichani), wakati
wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na
kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.
Mhandisi Mitambo wa Manispaa ya Kinondoni, Bw. Hamed Hamdun akiwasilisha hoja kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani), wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es salaam.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati)
akisikiliza hoja iliyokuwa ikiwasilishwa na mtumishi wa Manispaa ya Kinondoni, wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga
kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma wa Wilaya
hiyo. Kulia kwake ni Katibu Tawala Wilaya ya Kinondoni, Bi. Stella Msofe na
kushoto kwake ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Songoro Mnyonge.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni,
Bi. Hanifa Suleiman akisoma taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu ya Manispaa
ya Kinondoni kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu
Waziri huyo iliyolenga kuhimiza
uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma katika
Wilaya ya Kinondoni.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya
Kinondoni Mhe. Songoro Mnyonge akitoa salamu za Manispaa ya Kinondoni kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi wakati
wa ziara ya Naibu Waziri huyo iliyolenga
kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa
umma katika Wilaya ya Kinondoni.
No comments:
Post a Comment