Na. Veronica E. Mwafisi-Ilala
Tarehe 15 Disemba, 2022
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi amekemea tabia ya baadhi ya watumishi wa umma nchini
kujihusisha na vitendo vya wizi ambavyo vinakwenda kinyume na dhamira ya Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuujenga
Utumishi wa Umma wenye uadilifu na unaowajibika kwa wananchi kwa kutoa huduma
bora.
Akizungumza na Watumishi wa
Umma wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Ndejembi amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
ana maono makubwa ya kuujenga utumishi wa umma wenye uadilifu, hivyo amewataka
watumishi wa umma nchini kutokumuangusha
badala yake wafanye kazi kwa bidii na uadilifu mkubwa katika kulitumikia taifa.
“Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan amejipambanua wazi kututhamini watumishi wa umma kwa kuboresha maslahi
na stahili zetu hivyo, hatuna budi kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili
kuunga mkono kwa vitendo dhamira yake ya kuujenga Utumishi wa Umma wenye
uadilifu na unaowajibika kwa wananchi,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka
Watumishi wa Umma kutafakari madhara ya wizi na kutathmini mienendo yao ili
kutokuwa ni sehemu ya kukwamisha dhamira ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
ya kuboresha huduma kwa wananchi na kuliletea taifa maendeleo katika sekta zote
muhimu kama vile afya, kilimo, uvuvi, biashara, uwekezaji na miundombinu.
Sanjari na hilo, Mhe, Ndejembi
amewataka Waajiri na Maafisa Utumishi Serikalini kuwasimamia vema watumishi
wanaowaongoza badala ya kusubiria mpaka viongozi wa juu wa kitaifa kufika katika maeneo yao ya kazi kukemea uovu
pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.
Akizungumzia matumizi ya fedha
za umma, Mhe. Ndejembi amesema kuwa fedha za umma zinapaswa kutumika kwa
malengo yaliyokusudiwa na Serikali kwani kinyume na hilo ni ukosefu wa maadili
katika Utumishi wa Umma.
Mhe Ndejembi ameeleza bayana
kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita haitomvumilia mtumishi yeyote atakayekwenda
kinyume na maadili ya Utumishi wa Umma kwa kujihusisha na vitendo vya wizi katika
eneo lake la kazi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameendelea
na ziara ya kikazi Jijini Dar es Salaam yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa
watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya
Maskini nchini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Ilala (hawapo
pichani), akiwa katika ziara yake ya kikazi yenye lengo kuhimiza uwajibikaji na
kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma walio katika Halmashauri
hiyo ya Jiji.
Sehemu ya Watumishi wa
Umma wa Halmashauri ya Jiji la Ilala wakimsikiliza Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi (aliyekaa meza kuu katikati), alipokuwa akizungumza nao
wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua
changamoto zinazowakabili watumishi wa Halmashauri hiyo ya Jiji.
Mkuu wa
Wilaya ya Ilala, Mhe. Ng’wilabuzu Ludigija akitoa neno la utangulizi kabla ya
kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi kuzungumza na watumishi wa Wilaya ya Ilala (hawapo pichani), wakati
wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na
kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma walio katika wilaya hiyo.
Afisa Tawala wa Wilaya ya Ilala, Bi.
Charangwa Makwiro akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi mara
baada ya kuzungumza na watumishi wa Wilaya ya Ilala (hawapo pichani),
wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji
na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma walio katika wilaya hiyo.
Mtumishi wa Halmashauri ya Jiji la Ilala, Bi. Subira
Mwakibete akiwasilisha hoja kwa Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi (hayupo pichani), wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo
iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi
wa Halmashauri hiyo ya Jiji.
No comments:
Post a Comment