Tuesday, December 6, 2022

WATUMISHI OFISI YA RAIS-UTUMISHI WAFANYA UTALII HIFADHI YA TAIFA TARANGIRE KUMUUNGA MKONO MHE. RAIS KUUTANGAZA UTALII

 Na. James K. Mwanamyoto-Manyara

Tarehe 06 Disemba, 2022

Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora walioshiriki Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, uliofanyika Babati Mkoani Manyara wamefanya utalii katika Hifadhi ya Taifa Tarangire kwa lengo la kuunga Mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vya utalii ili taifa liongeze kipato kitakachotumika kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali nchini.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Cosmas Ngangaji kwa niaba ya watumishi waliofanya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, mara baada ya watumishi hao kujionea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo katika hifadhi hiyo.

Bw. Ngangaji amesema, nchi ina hazina kubwa ya vivutio vya utalii ambavyo vimetunzwa vizuri hivyo, katika kuhakikisha vivutio hivyo vinatoa mchango katika maendeleo ya taifa wameamua kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Mhe. Rais za kutangaza vivutio vya utalii kupitia filamu ya THE ROYAL TOUR kwa kufanya utalii kwenye Hifadhi ya Taifa Tarangire ili kuchangia pato na kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza hifadhi hiyo kwa watanzania wote.

Bw. Ngangaji ameongeza kuwa, utalii wa ndani umewekewa mazingira wezeshi kwa kuweka viingilio ambavyo Watanzania wengi wanavimudu hivyo, ametoa wito kwa watumishi walio katika taasisi nyingine za umma na Watanzania kwa ujumla kufanya utalii wa ndani.

“Mtumishi wa umma au Mtanzania yeyote akitembelea Hifadhi ya Taifa ya Tarangire akiwa ameambatana na familia yake licha ya kuchangia pato la taifa litakaloboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, pia atakuwa ameimarisha familia yake kwa kujenga umoja, mshikamano na upendo,” Bw. Ngangaji amefafanua.

Bw. Ngangaji amewapongeza watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na hifadhi nyingine nchini kwa kufanya kazi nzuri ya kuhifadhi vivutio vya utalii, kwani wanasaidia taifa kuingiza kipato na kutunza mazingira ili kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa upande wake, Afisa Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Bw. Godfrey Mwakapeje amesema hifadhi ina makundi makubwa ya tembo na wanyama wengine hivyo, amewahimiza watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwenda na familia zao wakati mwingine na kuwaomba wawe mabalozi wazuri wa hifadhi hiyo kwa Watanzania wote ili nao wapate fursa ya kuitembelee hifadhi hiyo yenye vivutio vingi vya utalii.


Mkurugenzi wa Idara ya Mipango, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Cosmas Ngangaji akieleza lengo la Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kufanya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, mara baada ya kumalizika kwa Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi la ofisi hiyo uliofanyika Babati Mkoani Manyara.



 

Afisa Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, Bw. Godfrey Mwakapeje akieleza vivutio vilivyopo katika hifadhi hiyo kwa Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.


 

Sehemu ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora waliofanya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, mara baada ya kumalizika kwa Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi la ofisi hiyo uliofanyika Babati Mkoani Manyara.

 

Mmoja wa tembo anayepatika katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire ambayo ni hifadhi maarufu kwa makundi makubwa ya tembo.


 

 

No comments:

Post a Comment