Mnamo tarehe 27 Oktoba,
2022 nilitoa maelekezo ya Serikali ya namna ya kushughulikia watumishi wa umma
walioondolewa kazini kwa sababu ya kughushi vyeti. Katika maelekezo hayo,
niliwahimiza waajiri kutekeleza masuala yafuatayo:-
a)
Kutoa
ushirikiano kwa watumishi walioghushi vyeti pindi wanapofika katika Ofisi zao
kukamilisha taratibu za ulipwaji ikiwa ni pamoja na kuwasilisha nyaraka muhimu
kwa ajili ya kulipwa michango yao walioiachanga kwenye mifuko ya hifadhi ya
jamii ikiwa ni pamoja na kujaza na kusaini Hati ya Ridhaa (Commitment Bond).
Aidha, niliwaagiza waajiri wote kuwasiliana na Ofisi za Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii za Wilaya na Mikoa ili kupata taarifa sahihi za watumishi hao zinazohusiana
na zoezi hilo.
b)
Kuandaa
na kuwasilisha kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii hati ya ridhaa (Commitment
Bond) pamoja na nyaraka nyingine kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya Mifuko
husika;
c)
Kuandaa
Dawati la Msaada (Help Desk) ili kufanikisha na kurahisha mchakato wa ulipaji
wa michango hiyo ikiwa ni pamoja na ujazaji wa mkataba wa makubaliano (Commitment
Bond);
d)
Kuzingatia
misingi ya utawala bora ikiwa ni pamoja na kuepuka vitendo vya rushwa wakati wa
zoezi hili.
Pamoja na kutoa
maelekezo hayo, mara kadhaa Ofisi yangu imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa
baadhi ya walengwa wanaohusika na zoezi hili kuwa baadhi ya waajiri
hawatekelezi maelezo hayo ya Serikali kwa ukamilifu na hasa kutokutoa
ushirikiano katika ujazaji wa Hati ya Ridhaa (Commitment Bond) pamoja na
kuchelewesha kuwasilisha vielelezo husika kwa ajili ya kuwawezesha walengwa kurejeshewa
michango yao, jambo ambalo linaleta usumbufu kwa walengwa kufuatilia msamaha
ambao Mhe. Rais ameutoa.
Kwa kuwa nina dhamana
ya kumsaidia Mhe. Rais kusimamia masuala ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
natumia fursa hii kwa mara nyingine kuwaelekeza tena waajiri wote kuhakikisha
wanatekeleza ipasavyo maelekezo ya Serikali niliyoyatoa mnamo tarehe 27 Oktoba,
2022.
Hata hivyo, kupitia Ofisi yangu, nimekwisha kuunda Timu ya kufanya uhakiki na kufuatilia mienendo ya waajiri wote katika kutekeleza maelekezo haya ya Serikali. Ninaamini kila mwajiri atatekeleza wajibu wake ipasavyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akihimiza
utekelezaji
wa agizo la kuwarejeshea michango waliyochangia katika mifuko ya hifadhi ya
jamii watumishi walioondelewa katika utumishi wa umma kwa kughushi vyeti.
No comments:
Post a Comment