Na. James K. Mwanamyoto-Moshi
Tarehe 15 Disemba, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amezionya
taasisi za umma nchini zinazokaidi kutekeleza takwa la kisheria la kufanya
vikao vya mabaraza ya wafanyakazi kuhakikisha wana kufanya vikao hivyo ili
kuboresha utendaji kazi kwa lengo la kutoa huduma kwa wananchi.
Mhe. Jenista ametoa onyo hilo wakati akifungua Kikao cha Pili cha Baraza la Sita la Wafanyakazi la Ofisi ya Taifa ya Takwimu kilichofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mhe. Jenista amesema ni lazima taasisi zote zihakikishe zinatekeleza takwa hilo la kisheria kwa kufanya mabaraza ya wafanyakazi ili kujadili changamoto zinazoukabili utendaji kazi wa taasisi zao ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma.
Ameongeza kuwa, vikao vya mabaraza ya wafanyakazi vikifanywa kwa wakati, vinaondoa uwezekano wa kufanyika kwa vikao vya watumishi visivyo rasmi, ambavyo mara nyingi vinatengeneza makundi na kuibomoa taasisi kwani havina tija katika kufikia malengo ya taasisi.
“Kwa ujumla, vikao vya mabaraza ya wafanyakazi vina tija kwenye ustawi wa nchi kwani vinawezesha kuongeza ari na morali ya utendaji kazi pamoja na kujenga mahusiano na ushirikiano mzuri ya kiutendaji baina ya menejienti na watumishi,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mhe. Jenista amesisitiza kuwa, ushirikishwaji wa wafanyakazi katika mabaraza ya wafanyakazi ni lazima kwani sheria zinaeleza wazi umuhimu wa mabaraza hayo ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, hivyo taasisi zote za umma zinapaswa kufanya vikao vya mabaraza ya wafanyakazi kwa wakati.
“Nazionya taasisi zote za umma ambazo hazitekelezi takwa hili la kisheria kuhakikisha zinatekeleza ili kutoa fursa ya majadiliano ya pamoja kwa mustakabali wa maslahi ya watumishi na maendeleo ya taifa kwa ujumla,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mhe. Jenista amesema, Serikali inatarajia kuwa baada ya kikao hicho, kupitia maazimio watakayokuwa wamejiwekea kila mtumishi kwa nafasi yake atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutekeleza majukumu yake kikamilifu ili kufikia malengo ya taasisi.
Akizungumzia faida ya kikao hicho cha baraza la wafanyakazi, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi hiyo, Dkt. Albina Chuwa amesema kikao hicho kina mchango mkubwa katika kufikia malengo ya taasisi ya kutoa takwimu sahihi za kupanga mipango ya maendeleo katika taifa.
Dkt. Chuwa ametaja baadhi ya mafanikio ambayo taasisi yake imeyapata ndani ya miezi sita katika kutekeleza bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 ni pamoja na kupata takwimu sahihi za mfumuko wa bei, pato la taifa la kila mwezi na kutoa takwimu za idadi ya watalii walioongezeka kupitia filamu ya The Royal Tour ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitumia kutanga vivutio vya utalii nchini.
Mhe. Jenista ameendelea kuwasisitiza waajiri katika taasisi za umma kufanya vikao vya mabaraza ya wafanyakazi ambavyo vimekuwa vikiongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa watumishi na kuleta tija kwa maendeleo ya taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifungua Kikao cha Pili cha Baraza la Sita la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kilichofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.
Sehemu ya wajumbe na wageni waalikwa wa Kikao cha Pili cha Baraza la Sita la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati akifungua kikao hicho kilichofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu akitoa salamu za mkoa wake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kabla ya Waziri huyo kufungua Kikao cha Pili cha Baraza la Sita la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kilichofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Ofisi hiyo, Dkt. Albina Chuwa akielezea lengo la kikao cha Baraza la Wafanyakazi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kabla ya Waziri huyo kufungua Kikao cha Pili cha Baraza la Sita la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kilichofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.
Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Mhe. Anne Makinda akielezea namna zoezi la sensa lilivyofanyika kwa umakini na umuhimu wa zoezi hilo kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kufungua Kikao cha Pili cha Baraza la Sita la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kilichofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.
Meneja kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Benedict Mugambi akiwasilisha taarifa ya matumizi ya takwimu za kijiografia zilizoandaliwa kwa kutumia mfumo wa GIS kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kufungua Kikao cha Pili cha Baraza la Sita la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kilichofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika Kikao cha Pili cha Baraza la Sita la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kilichofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu na wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kikao cha Pili cha Baraza la Sita la Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kilichofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro mara baada ya Waziri huyo kufungua kikao cha pili cha baraza la sita la wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kilichofanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment