Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Tarehe 09 Disemba, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, matokeo ya utafiti wa hali ya uzingatiaji wa maadili katika Utumishi wa Umma kwa mwaka 2022 yanaonesha kiwango cha uzingatiaji wa maadili kimefikia asilimia 75.9, hivyo kuongezeka kwa wastani wa asilimia 9.8 kikilinganishwa na cha asilimia 66.1 kinachotokana na matokeo ya utafiti uliofanywa mwaka 2014.
Mhe. Jenista ametoa takwimu hizo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma, na kuongeza kuwa matokeo hayo yanatokana na jitihada za kuimarisha uzingatiaji wa maadili chini ya Uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Jenista amesema, kutokana na dhamira thabiti ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali ya Awamu ya Sita imeweka misingi imara ya usimamizi wa maadili ya kiutendaji kwa watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya kuimarisha uwajibikaji katika utumishi wa umma.
Mhe. Jenista ameongeza kuwa, matokeo hayo pia yanatokana na ushirikiano na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Serikali na sekta binafsi kwenye eneo la ukuzaji maadili, pamoja na utekelezaji mzuri wa Mkakati wa Kitaifa wa kupambana na Rushwa.
Aidha, Mhe. Jenista amesema ofisi yake iliamua kutojitathmini yenyewe na badala yake kumpatia kazi ya utafiti Mtaalam Mwelekezi Dkt. Francis Mwaijande kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam ili afanye utafiti utakaokuwa na tija katika kuimarisha uzingatiaji wa maadili kwa watumishi wa umma.
“Tuliamua kumtafuta mtafiti huru kutoka nje ya ofisi yetu kwa lengo la kupata maoni na takwimu sahihi ya hali ya uzingatiaji wa maadili katika utumishi wa umma” Mhe. Jenista amefafanua
Katika kuhakikisha Serikali inafanyia kazi matokeo ya utafiti huo, Mhe. Jenista amezitaka taasisi simamizi za maadili na utawala bora pamoja na vyama vya kitaaluma kuendelea kushirikina na ofisi yake ili kuhakikisha ajenda ya kukuza maadili na kutumia matokeo ya utafiti huo inakuwa ni miongoni mwa mikakati ya kila siku ya usimamizi wa masuala ya maadili katika Taasisi za Umma.
Aidha, Mhe. Jenista amewataka
waajiri katika taasisi za umma kuhakikisha wanaweka na kuimarisha mifumo tumizi
ya utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na mifumo ya utoaji mrejesho wa
utendaji kazi wa taasisi za umma ili kuendelea kutoa fursa kwa wananchi ya
kukemea vitendo vya ukiukwaji wa maadili vinavyofanywa na baadhi ya watumishi
wa umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza
na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) jijini Dodoma leo wakati akitoa matokeo ya tafiti ya hali ya
uzingatiaji maadili katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2022. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa
Polisi, Salum Hamduni.
Sehemu ya Watendaji wa Ofisi ya Rais - UTUMISHI
pamoja na Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo
pichani) wakati akitoa matokeo
ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2022.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) kuzungumza na Waandishi wa Habari wakati akitoa matokeo ya tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2022.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama
akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani) jijini Dodoma
leo wakati akitoa matokeo ya
tafiti ya hali ya uzingatiaji maadili katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2022. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa
Polisi, Salum Hamduni.
No comments:
Post a Comment