Saturday, December 10, 2022

SERIKALI YA AWAMU YA SITA HAITOWAVUMILIA WATUMISHI WA UMMA WANAOKIUKA MAADILI WANAPOWAHUDUMIA WANANCHI - Mhe. Jenista

 Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 10 Disemba, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan haitowavumilia watumishi watakaobainika kukiuka misingi ya maadili wakati wa kuwahudumia wananchi katika taasisi zao.

Mhe. Jenista amesema hayo leo wakati akizungumza na wananchi na watumishi wa umma jijini Dodoma katika Viwanja vya Nyerere Square, kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kufunga Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa.

Mhe. Jenista amesema, Serikali haiko tayari kuona mtumishi yeyote anakwenda kinyume na Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo wakati wa kutoa huduma kwa wananchi.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, ofisi yake itaendelea kusimamia kikamilifu uadilifu kwa watumishi wa umma ili kuunga mkono azma ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuujenga Utumishi wa Umma wenye uadilifu na unaozingatia maadili na uwajibikaji kwa wananchi kwa kutoa huduma bora.

Mhe. Jenista amesema, Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliiweka wazi azma yake ya kusimamia uadilifu katika Utumishi wa Umma wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Aprili 2021 na kunukuu maneno aliyoyasema “Serikali ninayoiongoza haitowaonea aibu viongozi na watumishi wa umma wanaokiuka maadili, wezi, wazembe na wabadhirifu wa mali za umma” mwisho wa kunukuu, hivyo ofisi yangu itaendelea kuhimiza uadilifu ili kutimiza azma hiyo ya Mhe. Rais.

Aidha, Mhe. Jenista amewataka Watanzania kila mmoja kwa nafasi yake kutimiza wajibu wa kushiriki katika kutoa taarifa za uvunjifu wa maadili na haki za binadamu kwenye vyombo vilivyopewa jukumu la kusimamia maadili na haki za binadamu ili kuimarisha utawala bora nchini.

Mhe. Jenista amesisitiza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kusimamia misingi ya maadili, haki za binadamu na utawala bora kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa taifa.

Sanjari na hilo, Mhe. Jenista amewapongeza watumishi wote wa umma ambao wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kikamilifu na kwa uadilifu mkubwa, kwani kitendo hicho kimekuwa ni chachu ya kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.

Kauli Mbiu ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa ni “Maadili, Haki za Binadamu, Utawala Bora na Mapambano Dhidi ya Rushwa ni Jukumu la pamoja kati ya Serikali, Wananchi na wadau wengine”.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akipata maelezo kwenye banda la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakati wa Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa yaliyofanyika katika viwanja vya  Nyerere Square Jijini Dodoma. Kulia kwake ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Wananchi na Watumishi wa Umma waliohudhuria Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa yaliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Wananchi na Watumishi wa Umma kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kufunga Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa yaliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.


Sehemu ya Washiriki waliohudhuria Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa yaliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akimkaribisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwenye maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa yaliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi mara baada ya kuhitimisha Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa yaliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.

 



No comments:

Post a Comment