Na. Veronica Mwafisi – Dar es salaam
Tarehe 17 Disemba, 2022
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutoa
kipaumbele cha kuwapatia mikopo walengwa wa TASAF walio kwenye vikundi, kupitia
fedha za asilimia 10 zinazotengwa kwa ajili ya kuvikopesha vikundi vya
wanawake, vijana na wenye ulemavu ili mikopo hiyo iboreshe maisha ya kaya
maskini nchini kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan amekusudia.
Mhe. Ndejembi ametoa rai hiyo, kwa Wakurugenzi wa Halmashauri
nchini wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mhe. Ndejembi amesema, ameweza
kutembelea vikundi mbalimbali vya walengwa wa TASAF katika Halmashauri zote zilizopo
jijini Dar es salaam na kuona utekelezaji wa kazi za vikundi mbalimbali
vinavyojumuisha Vijana, Wazee, Walemavu na Wanawake.
“Wilayani Kinondoni kuna
vijana walio kwenye vikundi vya TASAF walipatiwa mikopo wa pikipiki ambapo wamemudu
kurejesha, pia wanawake Temeke walio kwenye vikundi vya TASAF wamepatiwa mikopo
ya shilingi milioni 10 na Ilala wamepatiwa milioni 30 ambayo imewawezesha
kuboresha maisha yao na kujishughulisha na ujasiriamali,” Mhe. Ndejembi amefafanua.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Bi. Salome Mwakigomba
amesema TASAF imefanya jitihada kubwakuhamasisha uundaji wavikundi vya walengwa
katika halmashauri zote ambazo Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unatekelezwa
hivyo wakipatiwa mikopo hiyo ya asilimia 10 watendelea kuboresha maisha yao.
Bi. Mwakigomba amesema, TASAF
itatekeleza maelekezo ya Ndejembi ya kuwahamasisha walengwa wa TASAF kuwa na
miradi endelevu ili wajiongezee kipato kitakachowawezesha kuboresha maisha yao.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amehitimisha ziara yake ya kikazi Mkoani Dar es salaam iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi akizungumza
na walengwa wa TASAF wa Kikundi cha Twiyendage
kilichopo Wilaya ya Ubungo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua
utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini jijini Dar es salaam.
Sehemu
ya walengwa wa TASAF wa kikundi cha Hapa
Kazi tu na Umoja Group vya Wilaya ya Kigamboni
wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati akizungumza nao,
alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Sehemu
ya walengwa wa TASAF wa kikundi cha Jiwezeshe
Women Group Wilaya ya Temeke wakionesha baadhi ya bidhaa
wanazotengeneza, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
(hayupo pichani) iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya
Maskini kwenye Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Mwakilishi
wa Mtendaji Mkuu wa TASAF, Bi. Salome Mwakigomba akitoa taarifa ya utekelezaji
wa majukumu ya TASAF wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
jijini Dar es Salaam, iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya
Maskini.
No comments:
Post a Comment