Na. Veronica E. Mwafisi-Meatu
Tarehe 27 Septemba, 2022
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi amewataka watumishi wa umma nchini kujituma na kujitoa
kikamilifu katika kuwahudumia wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma
zinazotolewa na Serikali kupitia taasisi zake.
Mhe. Ndejembi ametoa wito huo
kwa watumishi wa umma, wakati akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri
ya Wilaya ya Meatu akiwa katika ziara ya kikazi yenye lengo la kuhimiza
uwajibikaji na kutatua changamozo zinazowakabili watumishi wa umma katika Wilaya
hiyo.
Mhe. Ndejembi amesema,
watumishi wa umma ni mabalozi wa serikali hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa
uadilifu, weledi, kujituma na kujitoa kwa ajili ya serikali katika kutoa huduma
bora kwa wananchi.
“Mtumishi wa umma ni mwakilishi
wa serikali mahali anapofanya kazi, hivyo hana budi kutambua kuwa serikali
imemuajiri ili kuwatumikia wananchi kwa kuwapatia huduma bora kama ambavyo
serikali imekusudia,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
Halmashauri wa Wilaya ya Meatu, Bw. Msoleni Dakawa amemshukuru Mhe. Rais Samia
Suluhu Hassan kwa kutoa ajira mpya 104 katika Halmashauri hiyo zikiwemo kada za
elimu na afya ili kuwahudumia wananchi wilayani humo.
Aidha, Bw. Msoleni ameishukuru
ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kutoa
kipaumbele cha kuwapatia stahiki watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya
Meatu.
Naye, Mtumishi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Meatu, Bw. Thomas Shishwa kwa niaba ya watumishi wengine,
amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kutenga muda wake kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili
na kuzitafutia ufumbuzi papo kwa hapo, ikiwa ni pamoja na kuwapatia ufafanuzi
wa hoja za masuala ya kiutumishi walizoziwasilisha.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi anaendelea
na ziara ya kikazi Mkoani Simiyu yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa
watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
mkoani humo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu,
wakati wa ziara yake ya kikazi katika halmashauri hiyo iliyolenga kuhimiza
uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili.
Watumishi wa Umma wa Halmashauri
ya Wilaya ya Meatu wakimsikiliza Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao, wakati wa ziara
yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto
zinazowakabili.
Mkurugenzi
wa Halmashauri Wilaya ya Meatu, Bw. Msoleni Dakawa, akitoa taarifa ya utelezaji
wa majukumu ya halmashauri yake kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
(Wakwanza kulia), wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga
kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi katika
halmashauri hiyo.
Mkuu wa Shule ya Kimali, Bw. Marco Ng’wendamunkono wa
Halmashauri ya Wilaya ya Meatu (aliyesimama) akiwasilisha
hoja kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya
kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua
changamoto zinazowakabili watumishi wa halmashauri hiyo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi
(Wakwanza kushoto) akijibu hoja iliyokuwa imewasilishwa na mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Meatu wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua
changamoto zinazowakabili watumishi wa umma wa Halmashauri hiyo. Kulia Kwake ni
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe. Fauzia Ngatumbura na kushoto kwake ni Mwakilishi
wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw.
Oscar Maduhu.
Mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Meatu, Bw. Thomas Shishwa akitoa neno la
shukurani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati wa ziara yake ya kikazi ya Naibu
Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto
zinazowakabili watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu.
No comments:
Post a Comment