Friday, September 2, 2022

KAMATI YA UKAGUZI OFISI YA RAIS-UTUMISHI YAPATIWA MAFUNZO YA KUDHIBITI MATUMIZI YA FEDHA ZA SERIKALI KWA MUJIBU WA MAELEKEZO YA MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN

Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Tarehe 02 Septemba, 2022

Wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wamepatiwa mafunzo ya namna bora ya kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali katika shughuli za kila siku ikiwemo fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu-UTUMISHI, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Hilda Kabissa amesema, mafunzo hayo yatasaidia kufikia azma ya Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuleta maendeleo katika taifa.

“Washiriki zingatieni mafunzo haya kwani yatasaidia kufikia azma ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kudhibiti rasilimalifedha katika utekezaji wa miradi ya maendeleo ya serikali ili iweze kutoa matokea chanya yatakayoboresha maisha ya wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zitolewazo na taasisi za serikali.” Mkurugenzi Kabissa amesisitiza.

Mkurugenzi Kabissa ameongeza kuwa, uelewa utakaojengwa kupitia mafunzo hayo pamoja na kuwezesha kamati kusimamia kikamilifu udhibiti wa rasilimalifedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili iwe na tija kwa taifa pia yatawezesha rasilimaliwatu kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, uzalendo na bila kushurutishwa kama ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza mara kwa mara.

Akizungumzia lengo la mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Victor Kategere amesema mafunzo hayo yamelenga kuiwezesha kamati kupata weledi na ujuzi wa masuala ya ukaguzi ili waweze kusimamia kikamilifu matumizi ya rasilimalifedha na rasilimali nyingine.

Naye Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ambaye pia ni Mratibu wa Vikao vya Kamati ya Ukaguzi, Bi. Martha Wililo amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwa kamati hiyo ya ukaguzi kwani yataiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa miongozo na sheria zilizopo katika kulinda rasilimalifedha na rasilimali nyingine zilizopo kwa manufaa ya taifa.

Akizungumzia faida za mafunzo hayo katika usimamizi wa Serikali Mtandao, Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA Serikalini ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Ukaguzi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Priscus Kiwango amesema, mafunzo hayo yataisaidia kamati kupata ujuzi wa namna ya kukagua mifumo ya TEHAMA inayotumika Serikalini katika kutoa huduma kwa wananchi.

Mada mbalimbali zimewasilishwa katika mafunzo hayo ya siku mbili ikiwemo Mabadiliko ya Sheria ya Fedha, Muundo wa Kamati ya Ukaguzi na Uteuzi wa Wajumbe, Majukumu ya Wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi, Majukumu ya Sekretarieti ya Kamati ya Ukaguzi, Mkataba wa Kamati ya Ukaguzi (Audit Committee Charter) pamoja na Muundo wa Taarifa za Kamati ya Ukaguzi na Uwajibikaji wa kuwasilisha Taarifa husika.


Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Hilda Kabissa akifungua mafunzo kwa Kamati ya Ukaguzi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa niaba ya Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro leo jijini Dar es Salaam. 


Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Victor Kategere akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Hilda Kabissa kufungua mafunzo kwa Kamati ya Ukaguzi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma leo jijini Dar es Salaam. 


Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ambaye pia ni Mratibu wa Vikao vya Kamati ya Ukaguzi, Bi. Martha Wililo akieleza namna mafunzo ya Kamati ya Ukaguzi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora yatakavyosaidia Kitengo chake katika utekelezaji wa shughuli za Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.


Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA Serikalini ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Ukaguzi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Priscus Kiwango akieleza namna mafunzo ya Kamati ya Ukaguzi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora yatakavyosaidia katika kusimamia utekelezaji wa serikali mtandao.

 

Mjumbe wa Kamati ya Ukaguzi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Mathias Abisai akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Hilda Kabissa kwa kufungua mafunzo kwa Kamati ya Ukaguzi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora leo jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Hilda Kabissa akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na baadhi ya watendaji wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora mara baada ya kufungua mafunzo ya kamati hiyo leo jijini Dar es Salaam. 


 

No comments:

Post a Comment