Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 30 Agosti, 2022
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro ameelekeza Mwongozo wa Mpango wa Urithishanaji Madaraka katika Utumishi wa Umma wa mwaka 2011 uboreshwe ili kuendana na dhamira ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuujenga Utumishi wa Umma wenye uadilifu, nidhamu na unaowajibika kwa hiari kwa wananchi katika kutoa huduma bora.
Dkt. Ndumbaro ametoa maelekezo hayo leo jijini Dodoma, wakati akifungua kikao kazi cha wadau cha kujadili Mwongozo wa Mpango wa Urithishanaji madaraka katika Utumishi wa Umma kilichofanyika katika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.
Dkt. Ndumbaro amesema, mwongozo huo ni vema ukaainisha taratibu zitakazowezesha urithishanaji wa madaraka kwa viongozi wenye uadilifu na nidhamu katika utendaji kazi ili watoe mchango katika maendeleo ya taifa na uweke misingi madhubuti ya kuwa na Utumishi wa Umma wenye kuwajibika, uzalendo wa kitaifa na moyo wa kujitolea.
“Mwongozo ujenge mazingira wezeshi ya kuwa na watumishi wa umma wanaowajibika kwa wananchi kwa kutoa huduma bora, wanaowajibika kwa kuzingatia taaluma, wanaowajibika kwa wanaowasimamia na kwa viongozi,” Dkt. Ndumbaro amesisitiza.
Akizungumza kwa niaba ya wadau wanaoshiriki kujadili mwongozo huo, Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Marko Masaya amemhakikishia Dkt. Ndumbaro kuwa, watawasilisha maoni na mapendekezo ambayo yatawezesha kuandaa Mwongozo wa Mpango wa Urithishanaji Madaraka katika Utumishi wa Umma ambao utaliwezesha taifa kuwa na mpango mzuri wa kurithishana madaraka.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Dkt. Edith Rwiza amesema Serikali imekuwa ikitumia Mwongozo wa Mpango wa Urithishanaji Madaraka katika Utumishi wa Umma kwa kipindi cha miaka 11 sasa, ambapo kumekuwa na mabadiliko na changamoto mbalimbali za kimenejimenti na za kiutumishi, hivyo mamlaka imeelekeza kuupitia upya mwongozo huo wa mwaka 2011 ili kuona kama unahitaji maboresho, au kuhuishwa au kuandikwa upya ili kuendana na mahitaji.
Kikao kazi hicho kilichoandaliwa na
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia Idara ya
Uendelezaji Rasilimaliwatu kimehudhriwa na wadau kutoka katika Wizara, Idara
Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mamlaka za Serikali, Sekretarieti za Mikoa
na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na wadau walioshiriki kikao kazi cha
kujadili Mwongozo wa Mpango wa Urithishanaji Madaraka katika Utumishi wa Umma
kilichofanyika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.
Sehemu ya wadau kutoka katika taasisi mbalimbali za umma
wakimsikiliza Katibu Mkuu,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo
pichani) wakati akifungua kikao kazi cha kujadili Mwongozo wa Mpango wa Urithishanaji Madaraka
katika Utumishi wa Umma kilichofanyika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka
za Taifa jijini Dodoma.
Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Dkt.
Edith Rwiza akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (kulia) kufungua kikao kazi cha wadau kujadili
Mwongozo wa Urithishanaji Madaraka katika Utumishi wa Umma kilichofanyika ukumbi
wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.
Afisa
Utumishi Mkuu wa Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi.
Judith Shoo akiwasilisha mada kuhusu Mwongozo wa Mpango wa Urithishanaji Madaraka wakati wa
kikao kazi cha kujadili mwongozo huo kilichowashirikisha wadau wa taasisi
mbalimbali za Serikali kilichofanyika ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka
za Taifa jijini Dodoma.
Mshiriki
wa kikao kazi cha kujadili
mwongozo wa urithishanaji madaraka katika utumishi wa umma, Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya usimamizi wa
Rasilimaliwatu-TAMISEMI, Bw. Marko Masaya akitoa neno la shukrani kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi hicho kilichofanyika Ukumbi wa Idara ya
Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao kazi cha kujadili mwongozo wa
urithishanaji madaraka katika utumishi wa umma mara baada ya kufungua kikao
kazi hicho kilichofanyika Ukumbi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini
Dodoma.
No comments:
Post a Comment