Wednesday, August 17, 2022

MHE. JENISTA AMUAGIZA MRATIBU WA TASAF HALMASHAURI YA WILAYA YA MADABA KUHAKIKISHA WOTE WANAOSTAHILI KUINGIZWA KWENYE MPANGO WA KUNUSURU KAYA MASKINI WANAANDIKISHWA

Na. Veronica E. Mwafisi-Madaba

Tarehe 17 Agosti, 2022 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amemuagiza Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma kuhakikisha anafanya ufuatiliaji katika halmashauri hiyo na kuwatambua wote wenye sifa za kuingizwa kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wanaandikishwa ili wanufaike na mpango huo kwa lengo la kuboresha maisha yao. 

Mhe. Jenista ametoa maagizo hayo alipokuwa akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Kijiji cha Mtyangimbole, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa shughuli za TASAF katika halmashauri hiyo.p 

Waziri Jenista amesema, inawezekana kabisa katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba kuna baadhi ya wananchi ambao wana sifa za kuingizwa kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini lakini hawajaingizwa kutokana na sababu mbalimbali, hivyo Mratibu wa TASAF, Halmashauri hiyo ni lazima afuatilie ili watu hao waweze kuingizwa kwenye mpango huo na kuanza kupata huduma. 

“Mratibu wa TASAF wa Halmashauri, ninakuagiza kufanya ufuatiliaji na kuwatambua wananchi wote wenye vigezo vya kuingizwa kwenye mpango lakini wameachwa, baada ya kuwatambua uwasilishe taarifa zao TASAF Makao Makuu ili waweke utaratibu wa kuwahudumia kama wanavyohudumiwa walengwa wengine,” Mhe. Jenista amesisitiza. 

Aidha, Mhe. Jenista amewataka walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao wana uwezo wa kufanya kazi, kuibua miradi yenye faida kwa wananchi ili TASAF iweze kuiweka kwenye mpango kwa ajili ya kutekelezwa. 

 “Pamoja na kupeleka fedha moja kwa moja kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, TASAF pia ina maeneo ambayo walengwa hao wanaweza kuyafanyia kazi kwa kuibua miradi ya aina mbalimbali mfano miradi ya vivuko, barabara, uboreshaji wa visima, kujenga madaraja na madarasa, hivyo walengwa wenye uwezo wa kufanya kazi wanaweza kuibua miradi hiyo na kupata ujira.” Mhe. Jenista amefafanua. 

Mhe. Jenista amewataka Viongozi na Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba kujipanga kikamilifu katika usimamizi wa miradi hiyo inayoibuliwa na walengwa hao kwani ina manufaa makubwa kwa wananchi. 

Mhe. Jenista yuko mkoani Ruvuma kwenye ziara ya kikazi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama akimsikiliza mlengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji cha Mtyangimbole, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Mkoani Ruvuma, Bi. Geloada Fusi alipokuwa akieleza namna TASAF ilivyomuwezesha kuboresha maisha yake wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Jenista iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama akimsikiliza mlengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji cha Mtyangimbole, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Mkoani Ruvuma, Bi. Maklina Mhagama alipokuwa akieleza namna TASAF ilivyomuwezesha kuboresha maisha yake wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Jenista iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Kijiji cha Mtyangimbole, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo.


Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Kijiji cha Mtyangimbole, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, mkoani Ruvuma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo.


Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali Laban Thomas akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Kijiji cha Mtyangimbole, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri Jenista ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo.


Mbunge wa Jimbo la Madaba, Mhe. Joseph Mhagama akitoa salamu za jimbo lake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri Jenista ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma.


Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Bw. John Steven akitoa salamu za TASAF kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji cha Mtyangimbole, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo.


 

No comments:

Post a Comment