Na. Veronica E. Mwafisi-Namtumbo
Tarehe 18 Agosti, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewaagiza Watendaji wa Kijiji cha Namanguli, Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma kuwatafutia fursa za mafunzo ya ufundi watoto wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini walioshindwa kuendelea na masomo ya sekondari ili wapate ujuzi katika fani mbalimbali kwa lengo la kuendelea kuboresha maisha yao.
Mhe. Jenista ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Kijiji cha Namanguli, Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wakati wa ziara yake ya kikazi katika halmashauri hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Waziri Jenista amesema watoto hao wa walengwa wa TASAF waliomaliza darasa la saba na kidato cha nne lakini wameshindwa kuendelea na masomo yao kwa namna moja au nyingine, zinapokuja programu za ufundi wapelekwe huko ili wapate ujuzi katika fani mbalimbali.
“Leo hii, vijijini tunahitaji mafundi waliobobea katika fani mbalimbali wakiwemo mafundi umeme, bomba, seremala na wengine, wa kuweza kufanya hayo ni vijana hao tutakaowasomesha katika vyuo vya ufundi, hivyo muangalie namna ya kuwasaidia ili wakasome pale Namtumbo VETA baadae waje kuwasaidia wazazi,’’ Mhe. Jenista amesisitiza.
Aidha Mhe. Jenista amesisitiza suala la kuwatambua watoto wa walengwa wa TASAF waliomaliza kidato cha sita na kutakiwa kujiunga na vyuo vikuu kupewa mkopo wa asilimia mia moja kama ilivyoelekezwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ili waweze kupata elimu katika vyuo hivyo.
“Hili la watoto wa walengwa wa TASAF kupewa
mkopo wa elimu ya juu kwa asilimia mia moja ni agizo la Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo ni lazima
litekelezwe kikamilifu ili watoto hawa waweze kusoma bila shida yoyote.” Mhe.
Jenista amesisitiza.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Jenista Mhagama akizungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na
wananchi wa Kijiji cha Namanguli, Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani
Ruvuma wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo.
Walengwa
wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Kijiji cha Namanguli,
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma wakimsikiliza Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista
Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya
Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
katika halmashauri hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali Laban
Thomas akitoa neno la utangulizi
kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama
kuzungumza na walengwa
wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na wananchi wa Kijiji cha Namanguli,
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wakati wa ziara ya kikazi ya
Waziri Jenista ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika
halmashauri hiyo.
Mwakilishi
wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Bw. John Steven
akitoa salamu za TASAF kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji
cha Namanguli, Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wakati wa ziara
ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo.
No comments:
Post a Comment