Na. Veronica
E. Mwafisi-Songea
Tarehe 16 Agosti,
2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama amewaelekeza Viongozi wa Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha wanasimamia vema utendaji kazi wa watumishi wa umma ili kuongeza pato la taifa kupitia filamu ya ‘The Royal Tour’ iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo wakati akizindua rasmi tamasha la kuenzi mchango wa filamu ya ‘The Royal Tour” katika Mkoa wa Ruvuma iliyoasisiwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuleta maendeleo ya nchi.
Waziri Jenista amesema, viongozi na watumishi wa umma wanapaswa kufanya kazi kwa bidii, uzalendo na uadilifu katika kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vya utalii, na kuongeza kuwa viongozi Serikalini hawana budi kusimamia kikamilifu utendaji kazi ili kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.
“Niwaombe
viongozi wenzangu kila mmoja wetu katika eneo lake la kazi, asimame na ajenda
ya kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais za kuchangia maendeleo ya taifa kwa
kufanya kazi kwa bidii, uzalendo na uadilifu.” Mhe. Jenista amesisitiza.
Katika suala la ukusanyaji mapato mkoani Ruvuma, Mhe. Jenista amewakumbusha viongozi hao kupanua wigo wa ukusanyaji mapato kwa kutumia mifumo madhubuti ya TEHAMA ya ukusanyaji mapato, ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wananchi kulipa kodi kwa hiari ili kuongeza pato la Taifa.
Aidha, Mhe. Jenista amewasisitiza viongozi hao kusimamia kikamilifu mfumo mpya wa ruzuku ya mbolea ulioasisiwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ili uwafikie wananchi kwa utaratibu uliopangwa na Serikali na uwe na manufaa kwenye kilimo.
“Mhe. Mkuu wa Mkoa katika eneo hili, hatutegemei kusikia kazi hii nzuri iliyofanywa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya mfumo wa ruzuku ya mbolea umeingiliwa na rushwa, tusimame imara ili mfumo huu umfikie kila mlengwa kwa utaratibu uliopangwa na Serikali.” Mhe. Jenista amesisitiza.
Akimkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na viongozi na wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali Laban Thomas amesema kufanyika kwa tamasha hilo mkoani Ruvuma ni sehemu ya kumshukuru na kumpongeza Mhe. Rais kwa maono yake makubwa ya kuamua kuitangaza Tanzania kupitia filamu ya ‘The Royal Tour’ ili kuwavutia watalii na wawekezaji mbalimbali kutoka pande zote za dunia.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alizindua filamu
ya ‘The Royal Tour’ tarehe 28 Aprili, 2022 jijini Arusha yenye lengo la kuvutia
watalii na uwekezaji kwa maendeleo ya taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akionyesha tuzo aliyoipokea kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan baada ya kukabidhiwa na Mkuu wa
Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali Laban Thomas wakati wa
tamasha la kuenzi mchango wa filamu ya ‘The Royal Tour’ lililofanyika uwanja wa
Majimaji mkoani Ruvuma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na viongozi
na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma wakati wa tamasha la kuenzi mchango wa filamu ya
‘The Royal Tour’ katika uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.
Baadhi ya Watumishi wa
Umma mkoani Ruvuma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa
akizungumza nao kwenye tamasha
la kuenzi mchango wa filamu ya ‘The Royal Tour’ lililofanyika katika uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.
Wananchi wa Mkoa wa
Ruvuma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa
akizungumza nao kwenye tamasha
la kuenzi mchango wa filamu ya ‘The Royal Tour’ lililofanyika katika uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali Laban
Thomas akitoa neno la utangulizi
kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista
Mhagama kuzungumza na viongozi na wananchi wakati wa tamasha la kuenzi mchango
wa filamu ya ‘The Royal Tour’ lililofanyika katika uwanja wa Majimaji mkoani
Ruvuma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza jambo
alipotembelea banda la Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) kwenye tamasha
la kuenzi mchango wa filamu ya ‘The Royal Tour’ katika uwanja wa Majimaji Mkoa
wa Ruvuma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akipata maelezo ya Nyara
za Serikali kutoka kwa Afisa Utalii Pori la Akiba Liparamba, Bi. Maajabu Mbogo wakati wa tamasha la kuenzi
mchango wa filamu ya ‘The Royal Tour’ lililofanyika katika uwanja wa Majimaji
mkoani Ruvuma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akicheza ngoma ya Mganda kwenye tamasha la
kuenzi mchango wa filamu ya ‘The Royal Tour’ lililofanyika katika uwanja wa Majimaji
mkoani Ruvuma.
No comments:
Post a Comment