Thursday, August 18, 2022

SERIKALI IMETHIBITISHA KUJALI MASILAHI YA WATUMISHI KWA KUTUMIA SHILINGI BILIONI 50.7 KILA MWEZI KULIPA MISHAHARA MIPYA YA WATUMISHI 229,792 WALIOPANDISHWA MADARAJA

 Na. Veronica E. Mwafisi-Namtumbo

Tarehe 18 Agosti, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imethibitisha kujali masilahi ya watumishi wa umma kwa kutumia kiasi cha shilingi bilioni 50,663,802,729 kila mwezi kulipa mishahara mipya ya watumishi 229,792 waliopandishwa madaraja tangu iingie madarakani. 

Mhe. Jenista amesema hayo alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wakati wa ziara yake ya kikazi katika halmashauri hiyo, iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi wa umma wilayani humo.

Akieleza namna Serikali ilivyotoa kipaumbele kwenye masilahi ya watumishi wa umma, Mhe. Jenista amesema pamoja na kulipa mishahara hiyo ya watumishi waliopandishwa madaraja, Serikali pia imetumia kiasi cha shilingi bilioni 4,315,551,640 kulipa watumishi 21,204 waliobadilishwa kada na shilingi bilioni 124,369,178,888 kulipa malimbikizo ya madeni yanayotokana na mishahara kwa watumishi wa umma 75,007.

Sambamba na hayo, Waziri Jenista ameongeza kuwa, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kibali cha kuwapandisha madaraja kwa mserereko watumishi 67,244 waliokuwa na barua za upandishwaji wa madaraja tangu mwaka 2016/2017 lakini barua hizo zikafutwa.

Waziri Jenista amesema Mhe. Rais anayafanya haya yote kutokana na mapenzi mema aliyo nayo kwa watumishi wa umma na hata alipolihutubia Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza tarehe 22 Aprili, 2021 alisisitiza juu ya Waziri atakayemteua katika sekta ya utumishi wa umma kushughulikia stahiki za watumishi ambazo hawakuzipata kwa muda mrefu.

“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alipolihutubia Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza tarehe 22 Aprili, 2021, aliweka bayana vipaumbele vyake kwenye sekta ya utumishi wa umma ambapo alisema Waziri atakayepewa dhamana ya kumsaidia katika sekta hiyo ya Utumishi wa Umma asimamie haki, stahiki na wajibu, na ndio maana natekeleza maelekezo yake.’’ Mhe. Jenista amesisitiza. 

Mhe. Jenista amesema, kwa kuwa Serikali imeweka kipaumbele kwenye usimamizi wa stahiki za watumishi wa umma, hivyo ni wajibu wa watumishi wote kumuunga mkono Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili kutoa huduma bora kwa wananchi kwani haki inaenda sambamba na wajibu na kuongeza kuwa, watumishi wanapaswa kuwa na mpango mkakati utakaowawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kuchangia ustawi wa taifa.

Amesema kwa mujibu wa Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma, watumishi walio katika Serikali za Mitaa kazi yao kubwa ni kufikisha mahitaji kwa wananchi na kuongeza kuwa ili kufanikiwa katika hili ni vema kila mmoja akajiuliza juu ya huduma zinazotolewa endapo wananchi wanazifurahia.

“Ili kuwa na matokeo chanya katika utekelezaji wa majukumu yetu ni lazima kupanga, kutathmini na kujua mwelekeo wa halmashauri zetu,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Amesisitiza kuwa, hayo yote yanaweza kutekelezeka kwa ufasaha iwapo rasilimawatu iliyopo itathaminiwa na ndio maana amekuwa akiwasisitiza Maafisa Utumishi mara kwa mara kuwa walezi wa watumishi walio katika sehemu zao za kazi kwa kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzifanyia kazi kwa lengo la kuwajenga morali ya kufanya kazi kikamilifu.

Ziara ya Mhe. Jenista mkoani Ruvuma imelenga kuboresha utendaji kwa watumishi wa umma kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mkoa wa Ruvuma wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.


Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mkoa wa Ruvuma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo mkoani Ruvuma iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisikiliza taarifa ya utekelezaji ya utumishi na utawala kwa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.


Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Mhe. Dkt. Julius Ningu akimpokea Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama alipowasili katika ofisi hiyo kwa lengo la kuzungumza nao watumishi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo mkoani Ruvuma iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali Laban Thomas.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza jambo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.



 

 

No comments:

Post a Comment