Thursday, August 11, 2022

MHE JENISTA ARIDHISHWA NA NAMNA e-GA INAVYOWAJENGEA UWEZO VIJANA WA VYUO VIKUU KUFANYA TAFITI NA UBUNIFU WA MIFUMO YA TEHAMA KATIKA KUTATUA CHANGAMOTO KWENYE SEKTA MBALIMBALI NCHINI

 Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 11 Agosti, 2022 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameridhishwa na kazi inayofanywa na vijana wa Vyuo Vikuu wanaofanya utafiti na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA kupitia Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), mifumo ambayo itasaidia kutatua changamoto zinazokwamisha maendeleo katika sekta ya kilimo, nishati, madini na uchumi. 

Mhe. Jenista amesema hayo, mara baada ya kukitembelea Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) na kujionea kazi inayofanywa na vijana hao wa vyuo vikuu waliochukuliwa na e-GA kwa lengo la kuwajengea uwezo katika eneo la utafiti na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA ambayo itakuwa na tija katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, kuna utafiti mkubwa wa kimkakati unaofanya na vijana hao wa vyuo vikuu, ambao utaiwezesha Serikali kukusanya mapato ya kutosha yatakayotumika na Serikali katika kuleta ustawi wa taifa na maendeleo ya wananchi.

“Ninaipongeza menejimenti ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kuwa na mkataba maalum unaowawezesha kuwapata hawa vijana kutoka vyuo vikuu ili kuwapatia mafunzo kwa njia ya vitendo kwenye eneo la utafiti na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA itakayolisaidia taifa kuingia kwenye uchumi wa kidigitali,” Mhe. Jenista amefafanua. 

Mhe. Jenista amesisitiza kuwa, matokeo ya kazi nzuri ya utafiti na ubunifu huo wa mifumo ya TEHAMA, yatakuwa ni utoaji wa huduma bora kwa wananchi kwani mifumo hiyo itawarahisishia wananchi kupata huduma bora na kwa wakati katika taasisi za umma. 

“Kupitia mifumo itakayobuniwa, huduma zitatolewa kwa wananchi kwa gharama nafuu, mapambano dhidi ya rushwa yataimarika, mapato ya serikali yataongezeka ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa usimamizi wa matumizi sahihi wa fedha za umma,” Mhe. Jenista ameeleza.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amesema kuwa, utafiti na ubunifu unaofanywa na vijana wa Vyuo Vikuu kupitia Kituo hicho  unaonesha kuwa taifa limeanza kupiga hatua kwa kuwatumia vijana kuleta maendeleo, na kuongeza kuwa alichojifunza ni kuwa, kama nchi tunaweza kuwatumia vijana katika tafiti na bunifu zenye tija kwa taifa.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) amesema kwa sasa Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha e-GA kina uwezo wa kuchukua wanafunzi wa mazoezi kwa njia ya vitendo wapatao 100, lakini mamlaka ina mpango wa kuongeza uwezo wa kituo ili hapo baadae kiweze kuchukua wanafunzi kati ya 300 hadi 500 kwa wakati mmoja.

Mmoja wa vijana walionufaika na kituo hicho, Bw. Edward Sultan amesema Serikali kwa upande wake imeshatekeleza wajibu wake wa kuanzisha Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha e-GA ambacho kina vitendea kazi vyote vinavyohitajika, hivyo ni jukumu la vijana wa Vyuo Vikuu wanaofanya utafiti, ubunifu waliopata nafasi ya kufanya mazoezi kwa njia ya vitendo kufikiri walifanyie nini taifa ambalo limewapa fursa ya kutoa mchango katika eneo la utafiti na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA.

Mnufaika mwingine wa kituo hicho, Bi. Lina Lajo ameshukuru kupata fursa ya kujifunza kwa njia ya vitendo katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha e-GA na kuongeza kuwa, kituo hicho ni sehemu nzuri ya kujifunza na kutoa mchango kwa taifa kama vijana.

Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kilianza kupokea wanafunzi wa mazoezi kwa njia vitendo kutoka katika vyuo vikuu kuanzia mwaka 2019 mpaka sasa 2022 ambao wameshiriki katika ujenzi wa mifumo ya TEHAMA kama vile Mfumo wa e-Mrejesho, Mfumo wa e-Mikutano, Mfumo wa e-Dodoso na Mfumo wa e-Board ambayo inatumika hivi sasa Serikalini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza wakati wa kikao kazi chake na vijana wa Vyuo Vikuu wanaofanya utafiti na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA kupitia Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kilichofanyika jijini Dodoma.


Vijana wa Vyuo Vikuu wanaofanya utafiti na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA kupitia Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi kuona kazi inayofanywa na vijana hao katika kituo hicho jijini Dodoma.


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa ofisi yake, Mhe. Jenista Mhagama kufungua kikao kazi chake na vijana wa Vyuo Vikuu wanaofanya utafiti na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA kupitia Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kilichofanyika jijini Dodoma.


Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) mara baada ya Waziri Jenista kufungua kikao kazi chake na vijana wa Vyuo Vikuu wanaofanya utafiti na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA kupitia Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kilichofanyika jijini Dodoma.


Mmoja vijana wa Vyuo Vikuu wanaofanya utafiti na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA kupitia Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Bi. Faith Chilongani akimuelezea Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama namna wanavyofanya utafiti na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo alipotembelea kituo hicho kwa lengo la kuona kazi inayofanywa na vijana hao jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama (wakwanza kushoto) akipokelewa na    Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba mara baada ya kuwasili katika ofisi za Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) jijini Dodoma. Wakwanza kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - UTUMISHI, Bw. Xavier Daudi.


Mmoja wa wanafunzi wanaofanya kazi ya tafiti katika Kituo cha Utafiti na Ubunifu wa mifumo ya TEHAMA, Bi. Lina Lajo akishukuru kupata fursa ya kujifunza kwa njia ya vitendo katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha e-GA wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama alipotembelea kituo hicho kwa lengo la kuona kazi inayofanywa na vijana hao katika kituo hicho jijini Dodoma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya vijana wa Vyuo Vikuu wanaofanya utafiti na ubunifu wa mifumo ya TEHAMA kupitia Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Mifumo cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) mara baada ya kumaliza kikao kazi chake na vijana hao kilichofanyika jijini Dodoma. Wakwanza kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Xavier Daudi na wakwanza kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Mhandisi Benedict Ndomba.



 

 

No comments:

Post a Comment