Na. Veronica Mwafisi - Maswa
Tarehe 28 Septemba, 2022
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
amewataka watendaji wa serikali kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu
katika utekelezaji wa miradi ya TASAF nchini, ukiwemo wa ujenzi wa bweni la
wasichana katika shule ya Sekondari Budekwa wilayani Maswa ili kuunga mkono jitihada
ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan za kuliletea taifa maendeleo.
Mhe. Ndejembi ametoa wito huo, mara baada ya kukagua ujenzi wa bweni katika shule ya Sekondari Budekwa akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Kijiji cha Kiloleli wilayani Maswa.
Mhe. Ndejembi amesema, njia
pekee ya watendaji wa serikali kumuunga mkono Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan
katika utekelezaji wa miradi ya TASAF ni kuwahamasisha wananchi kushiriki utekelezaji
wake kuanzia ngazi ya kijiji, kata, tarafa hadi wilaya ili miradi hiyo iweze
kukamilika kwa wakati.
Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya jitihada
kubwa kupeleka mradi huo wa ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Budekwa
ili kuwalinda na kuwaepusha watoto wa kike na changamoto zinazokwamisha malengo
yao katika elimu.
“Mwanafunzi anapoishi katika
mazingira ya shule kutokana na uwepo wa bweni, itamsaidia fikra zake zote
kuzielekeza katika masomo, na hilo ndio lengo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan,”
Mhe. Ndejembi amesema.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bi.
Prisca Kayombo amesema Serikali
imetekeleza wajibu wake kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huo wa TASAF, hivyo
wananchi wa Kijiji cha Kiloleli wanapaswa kuhakikisha wanashiriki kukamilisha
mradi huo ili wanafunzi waweze kupata elimu bora.
Aidha, Bi. Kayombo amesema
ujenzi wa bweni hilo ukikamilika utasaidia pia kupunguza changamoto ya uwepo wa
mimba zisizotarajiwa kwa wanafunzi wa kike ambao baadhi yao hulazimika
kukatisha masomo yao.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji
wa mradi huo wa ujenzi wa bweni, Afisa Mtendaji wa Kata ya Budekwa, Bw. Masesa
Madirisha amesema, mradi huo una faida kubwa katika kuboresha mazingira ya
kusoma kwa watoto wa kike ambao wanapaswa kutimiza ndoto zao kama ilivyo kwa
watoto wa kiume.
Kijiji cha Kiloleli ni
miongoni mwa vijiji vitano vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
ambavyo vinatekeleza miradi ya kupunguza umaskini ya OPEC IV Awamu ya Kwanza.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi akizungumza
na wanafunzi na wananchi wa Kijiji cha Kiloleli wilayani Maswa, wakati wa ziara
yake ya kikazi ya kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya
Sekondari Budekwa unaotekelezwa na TASAF.
Sehemu
ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Budekwa wilayani Maswa wakimsikiliza Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri
huyo iliyolenga kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la wasichana katika shule
hiyo.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi akisisitiza jambo kwa wananchi wakati wa ziara ya kikazi ya
Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la wasichana
katika shule ya Sekondari Budekwa wilayani Maswa.
Mkuu
wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Asengwe Kaminyoge (Wakwanza kulia) akitoa neno la
utangulizi kabla ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na wanafunzi na
wananchi wa Kijiji cha Kiloleli wilayani Maswa, wakati wa ziara yake ya kikazi
ya kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya Sekondari
Budekwa unaotekelezwa na TASAF.
Mwonekano
wa bweni la wasichana wa shule ya Sekondari Budekwa wilayani Maswa,
linalojengwa kwa ufadhili wa TASAF kupitia miradi ya kupunguza umaskini –OPEC
IV.
No comments:
Post a Comment