Tuesday, September 20, 2022

WAAJIRIWA WAPYA 553 WA TAKUKURU WATAKIWA KUTUMIKIA MIAKA 5 BILA KUHAMIA TAASISI NYINGINE ILI KUTIMIZA LENGO LA MHE. RAIS LA KUTOKOMEZA RUSHWA NCHINI

 Na. James K. Mwanamyoto-Moshi

Tarehe 20 Septemba, 2022

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amemuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU kuweka kipengere kwenye mkataba wa waajiriwa wapya 553 wa TAKURURU chenye sharti la kutumikia miaka mitano katika taasisi hiyo kabla ya kufikiria kuhamia taasisi nyingine ili kutimiza lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan la kutokomeza vitendo vya rushwa nchini. 

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro, wakati akifunga mafunzo ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wapya wanaoajiriwa na TAKUKURU, yaliyotolewa katika Shule ya Polisi Tanzani iliyopo Moshi ili kuwajengea uwezo wa kupambana na vitendo vya rushwa nchini.

Mhe. Ndejembi amesema, amelazimika kutoa maelekezo hayo ili kukomesha tabia iliyoibuka ya baadhi ya watu kuomba kazi yoyote inayotangazwa serikalini na pindi akiajiriwa anataka kuhamia taasisi nyingine kwa maslahi yake binafsi, wakati serikali imemuajiri ili kuutumikia umma wa watanzania katika taasisi aliyopangiwa.

“Ninaelekeza kwa ajira hizi 553 za TAKUKURU, kiwekwe kipengere kinachoainisha kuwa, ni lazima waitumikie TAKUKURU si chini ya miaka 5 bila kuhamia taasisi nyingine kwani serikali imewekeza kiasi kikubwa katika kuwapatia mafunzo na kuwaajiri, hivyo ni lazima muutumikie umma katika mapambano dhidi ya rushwa ili thamani ya fedha iliyowekezwa ionekane,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amejipambanua kuichukia rushwa na hataki kuona maendeleo ya taifa yanakwamishwa na vitendo kwa rushwa, hivyo amewataka waajiriwa hao wapya wa TAKUKURU kuunga mkono kwa vitendo azma hiyo ya Mheshimiwa Rais.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu amesema kuwa Mhe. Rais amefanya mengi mazuri ikiwa ni pamoja na kutoa ajira hizo 553 za TAKUKURU, ili kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa nchini na amewataka watakaopangiwa kwenye mkoa wake wafanye kazi kwa bidii na uadilifu katika kusimamia fedha za miradi ya maendeleo ambazo Mhe. Rais amezitoa kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi mkoani Kilimanjaro.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni amesema waliohitimu mafunzo hayo watapangiwa vituo vya kazi na kuwataka kila mmoja akubali kituo atakachopangiwa kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan za kupambana na rushwa.

“Sitarajii kuona vimemo vya kuniomba niwabadilishie vituo vya kazi kwani wakati mnaomba ajira na wakati mnafanya usaili tuliwauliza kama mko tayari kufanya kazi popote nchini, na kila mmoja wenu alisema kuwa yuko tayari kufanya kazi sehemu yoyote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” ACP Hamduni amesisitiza.

Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan inaendelea na jitihada za kuijengea uwezo kiutendaji Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kuipatia rasilimaliwatu yenye tija katika kuendeleza mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa nchini ambavyo vinakwamisha maendeleo ya taifa.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akikagua gwaride la wahitimu wa mafunzo ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wapya wanaoajiriwa na TAKUKURU kabla ya kufunga mafunzo hayo mjini Moshi.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akikaribishwa kukagua gwaride la wahitimu wa mafunzo ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wapya wanaoajiriwa na TAKUKURU kabla ya kufunga mafunzo hayo mjini Moshi.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akipokea heshima ya gwaride la wahitimu wa mafunzo ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wapya wanaoajiriwa na TAKUKURU wakati akifunga mafunzo hayo mjini Moshi.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akishuhudia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakionyeshwa na wahitimu wa mafunzo ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wapya wanaoajiriwa na TAKUKURU (hawapo pichani) kabla ya kufunga mafunzo hayo mjini Moshi. Kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni na kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo cha Polisi Tanzania SACP Ramadhani Mungi.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akifunga mafunzo ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wapya wanaoajiriwa na TAKUKURU baada ya kuhitimu mafunzo hayo katika Chuo cha Polisi Tanzania, mjini Moshi.

 

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akifunga mafunzo ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wapya wanaoajiriwa na TAKUKURU baada ya kuhitimu mafunzo hayo katika Chuo cha Polisi Tanzania, mjini Moshi.

Sehemu ya wahitimu wa mafunzo ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wapya wanaoajiriwa na TAKUKURU wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wakati akifunga mafunzo hayo mjini Moshi.


Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu akitoa salamu za mkoa wake kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kufunga mafunzo ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wapya wanaoajiriwa na TAKUKURU mjini Moshi. 


Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni akielezea lengo la mafunzo ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi wapya wanaoajiriwa na TAKUKURU yaliyofanyika katika Chuo cha Polisi Tanzania mjini Moshi kabla ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kufunga mafunzo hayo.

 



 

No comments:

Post a Comment