Na. Veronica E. Mwafisi-Dodoma
Tarehe 25 Septemba, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameitaka Kamati ya Taifa ya Uongozi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuwa na utamaduni wa kuwatembelea walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, unaoratibiwa na TASAF ili kubaini na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazoweza kukwamisha utekelezaji wa mpango huo ambao Serikali inautekeleza kwa lengo la kuboresha maisha ya kaya maskini nchini.
Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma, wakati akizindua Kamati ya Taifa ya Uongozi ya TASAF iliyoteuliwa hivi karibuni mara baada ya kamati iliyopita kumaliza muda wake kiutendaji.
Waziri Jenista amewahimiza wajumbe wa kamati hiyo, kuhakikisha wanakwenda kuzungumza na viongozi, waratibu na walengwa katika maeneo yote ambayo Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unatekelezwa, ili kufikia lengo la Serikali la kuzikwamua kaya maskini kutoka katika lindi la umaskini.
“Mhe. Mwenyekiti na wajumbe wa kamati hii, tembeleeni maeneo ambayo mpango wa TASAF unatekelezwa ili mjiridhishe namna ambavyo unawafikia walengwa na kuwanufaisha,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mhe. Jenista ameongeza kuwa, wajumbe wa kamati wakitembelea maeneo ambayo mpango wa TASAF unatekelezwa, watapata fursa ya kujionea namna walengwa walivyonufaika, ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto ambazo walengwa hao wa TASAF wanakabiliana nazo.
Akizungumzia azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuzikwamua kaya maskini, Mhe. Jenista amesema kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan haitomuacha mtu nyuma katika kufikia malengo ya maendeleo kama yalivyoainishwa katika dira ya maendeleo (Vision 2025), na ndio maana imejipanga vema katika kuhakikisha inaboresha maisha ya kaya zote maskini kwenye vijiji, mitaa na shehia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Peter Ilomo amemhakikishia, Mhe. Jenista kuwa yeye pamoja na kamati yake watayafanyia kazi maelekezo yote ambayo ameyatoa ili kutimiza lengo la serikali la kuboresha maisha ya kaya maskini.
Naye, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Dkt. Moses Kusiluka amesema, ataendelea kushirikiana na TASAF ili kuhakikisha inatimiza lengo lake la kuboresha maisha ya wananchi ambao wanaishi katika familia zenye hali duni kiuchumi.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga amesema, TASAF imekuwa na mafanikio makubwa katika kuboresha maisha ya kaya maskini ikiwa ni pamoja na kujenga rasilimaliwatu ya kutosha kwa kuwawezesha kielimu wanafunzi wanaotoka kwenye kaya maskini kutoka hatua moja kwenda nyingine.
“Mwaka jana, TASAF kwa kushirikiana na bodi ya mikopo tumewawezesha wanafunzi 1200 kujiunga na elimu ya juu katika vyuo vikuu mbalimbali nchini, na mwaka huu mchakato bado unaendelea lakini tunatarajia kuwawezesha wengi zaidi kwani walioomba wako zaidi ya 3000,” Bw. Mwamanga amefafanua.
Kamati ya Taifa ya Uongozi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa sasa inaundwa na Mwenyekiti Bw. Peter Ilomo, pamoja na wajumbe wengine ambao ni Balozi Zuhura Bundala, Bw. Richard Shilamba, Dkt. Charles Mwamwaja, Dkt. Ruth Lugwisha, Dkt. Naftali Ng’ondi, Bw. Ali Salim Matta, Mhandisi Rogatus Mativila na Dkt. Grace Magembe.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama
akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Uongozi ya TASAF pamoja na
watendaji wa TASAF, wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo uliofanyika jijini
Dodoma.
Wajumbe wa Kamati ya Taifa ya
Uongozi ya TASAF na baadhi ya watendaji wa TASAF wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa
akizungumza nao wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo uliofanyika jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya
Uongozi ya TASAF, Bw. Peter Ilomo akizungumza kabla ya kumkaribisha Mhe.
Jenista Mhagama kuzungumza na wajumbe wa kamati na watendaji wa TASAF wakati wa
uzinduzi wa kamati hiyo uliofanyika jijini Dodoma.
Mwenyekiti aliyemaliza muda wake kuiongoza Kamati ya Taifa ya Uongozi ya TASAF, Dkt. Moses Kusiluka akitoa neno la shukrani kwa Mhe. Jenista Mhagama na watendaji wa TASAF, wakati wa hafla ya uzinduzi wa kamati mpya iliyoteuliwa hivi karibuni iliyofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga akitoa taarifa ya utekelezaji na majukumu ya taasisi yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kamati ya Taifa ya Uongozi ya TASAF uliofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama
akimkabidhi tuzo Mwenyekiti aliyemaliza muda wake kuiongoza Kamati ya Taifa ya
Uongozi ya TASAF, Dkt. Moses Kusiluka ya kutambua mchango aliotuoa wakati wa
uongozi wake. Wakwanza kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus
Mwamanga.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akisikiliza taarifa ya utekelezaji wa mjaukumu ya TASAF, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kamati ya Taifa ya Uongozi ya TASAF iliyofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya
pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Uongozi ya TASAF, mara baada ya kuizindua
kamati hiyo jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment