Thursday, September 8, 2022

‘TAKUKURU RAFIKI’ NI MKOMBOZI KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA VITENDO VYA RUSHWA NCHINI - Mhe. Chaurembo

 Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 08 Septemba, 2022

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo amesema mpango wa TAKUKURU rafiki ambao utazinduliwa na Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa hivi karibuni utakuwa ni mkombozi katika mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Mhe. Chaurembo amesema, mpango wa TAKUKURU rafiki ukianza kutekelezwa utakuwa na manufaa katika kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa nchini, hasa katika kuzuia upotevu wa fedha za miradi ya maendeleo ambayo serikali inatoa fedha nyingi ili iwanufaishe wananchi.

Mhe. Chaurembo ameitaka TAKUKURU kutoa  elimu zaidi kwa wananchi wa  kawaida kuhusu utekelezaji wa mpango wa TAKUKURU rafiki ili watoe ushirikiano wa kutosha kwa TAKUKURU katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa.

“Elimu ya TAKUKURU rafiki ikimfikia mwananchi wa kawaida atasaidia kutoa taarifa kwa TAKUKURU ambazo zitawezesha kupambana na vitendo vya rushwa, ikiwa ni pamoja na kudhibiti upotevu wa fedha za serikali zinazotolewa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo,” Mhe. Chaurembo amesisitiza.

Akizungumzia utekelezaji wa mpango wa TAKUKURU rafiki, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, TAKUKURU imejipanga vema kutoa elimu ya utekelezaji wa mpango huo kwa wananchi ili wawe mstari wa mbele katika kutoa taarifa ambazo zitazuia vitendo vya rushwa vinavyokwamisha juhudi za maendeleo.

“Mpango huu wa TAKUKURU rafiki ukifanikiwa utakuwa ni sehemu ya kuunga mkono azma ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kutokomeza vitendo vya rushwa kwa maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi,” Mhe. Jenista amefafanua.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, Mhe. Rehema Migilla ameipongeza TAKUKURU kwa kuanzisha mpango wa TAKUKURU rafiki wenye lengo la kuwashirikisha wananchi ambao ndio waathirika wakubwa wa vitendo vya rushwa.

Akifafanua hoja kuhusu utekelezaji wa mpango wa TAKUKURU rafiki, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bi. Neema Mwakalyelye amesema mpango huo umelenga kumfikia Mtanzania aliye katika ngazi ya mtaa, kijiji na kata.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) imeendelea kupokea taarifa za utekelezaji wa majukumu ya taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo leo imepokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo akiongoza kikao kazi cha kamati yake leo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa mwaka wa fedha 2021/2022. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo leo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa mwaka wa fedha 2021/2022.


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Denis Londo akichangia hoja wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo leo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa mwaka wa fedha 2021/2022. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifafanua hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo leo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa mwaka wa fedha 2021/2022.


Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo leo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa mwaka wa fedha 2021/2022.


Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu, Mhe. Rehema Migilla akichangia hoja wakati wa kikao cha kamati hiyo leo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa mwaka wa fedha 2021/2022.


Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mhe. Mwantumu Zodo akichangia hoja wakati wa kikao cha kamati hiyo leo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa mwaka wa fedha 2021/2022.


Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bi. Neema Mwakalyelye akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo leo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.



No comments:

Post a Comment