Na. Veronica Mwafisi - Meatu
Tarehe 27 Septemba, 2022
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
amesema Serikali kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko
wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) imejenga bweni katika Shule ya Sekondari Bukundi
iliyopo Kijiji cha Bukundi wilayani Meatu, ili kuweka mazingira rafiki ya kuongeza
ufaulu wa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuwaepusha na changamoto ya mimba za
utotoni.
Mhe. Ndejembi ameyasema hayo,
mara baada ya kukagua bweni la wanafunzi wa shule ya Sekondari Bukundi akiwa
katika ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya
Maskini katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.
Mhe. Ndejembi amesema, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametafuta fedha hizo za
TASAF na kujenga bweni hilo kwa ajili ya kutatua changamoto na adha zinazowakabili
wanafunzi wa eneo hilo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilazimika kusafiri
umbali mrefu ili kuhudhuria masomo.
Kutokana na umuhimu wa bweni
hilo, Mhe. Ndejembi ametoa mwenzi mmoja kwa viongozi na wasimamizi wa ujenzi wa
bweni hilo kushirikiana kikamilifu na TASAF ili likamilike kwa wakati na kuanza
kutoa huduma.
“Bweni hili likikamilika kwa
wakati litaongeza ufaulu na kusaidia kuondoa changamoto ya mimba za utotoni,
kwani wanafunzi wataishi katika eneo hili la shule badala ya kwenda kuishi kwenye
jamii ambayo ina changamoto nyingi,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, licha ya TASAF kuwezesha mradi wa bweni hilo lakini imejenga miradi ya maji, zahanati na vituo vya afya katika kipindi kifupi cha uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo amewataka wananchi wa Kijiji cha Bukundi kulinda miradi hiyo ili iwanufaishe wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani.
“Sisi wananchi wa Bukundi tuna
jukumu moja la kulinda miradi hii kwa manufaa yetu kwani serikali imetumia fedha
nyingi kuitekeleza miradi hiyo,” Mhe. Ndejembi ameongeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa
Wilaya ya Meatu, Mhe. Fauzia Ngatumbura amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu
Hassan kwa kuwapatia fedha za ujenzi wa bweni hilo la wanafunzi katika Shule ya
Sekondari Bukundi ambalo litaboresha mazingira ya wanafunzi kusoma.
Mhe. Fauzia amesema, shule
ambayo bweni hilo limejengwa ipo katika jamii ya wafugaji ambao wanaishi maeneo
ya mbali na shule hiyo, kutokana na umbali huo watoto wengi walitamani kusoma
lakini walishindwa kutokana na kutembea umbali mrefu, hivyo bweni hilo
litasaidia kuondoa changamoto hiyo.
Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi
Mtendaji wa TASAF, Bw. Oscar Maduhu amewasisitiza wananchi wa Kijiji cha
Bukundi kuilinda miundombinu ya bweni hilo kwani litawawezesha wanafunzi kupata
elimu bora kwa ajili ya manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Bweni la wanafunzi katika Shule
ya Sekondari Bukundi wilayani Meatu, linalojengwa kwa ufadhili wa TASAF litakuwa
na uwezo wa kuwahudumia wanafunzi 80.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi akizungumza
na wanafunzi na wananchi wa Kijiji cha Bukundi wilayani Meatu, wakati wa ziara
yake ya kikazi ya kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi katika shule ya
Sekondari Bukundi unaotekelezwa na TASAF wilayani humo.
Sehemu
ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bukundi wilayani Meatu wakimsikiliza Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri
huyo iliyolenga kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi katika shule hiyo.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi (Wapili kutoka kushoto) akizungumza jambo na Mwakilishi wa
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Oscar Maduhu (Wakwanza kushoto) wakati wa
ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua iliyolenga kukagua
mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi katika shule ya Sekondari Bukundi
wilayani Meatu. Wakwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Meatu Mhe. Fauzia
Ngatumbura.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi (Wakwanza kulia) akisikiliza taarifa ya utekelezaji wa
mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi shule ya Sekondari Bukundi wilayani Meatu,
wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la
wanafunzi katika shule ya Sekondari Bukundi wilayani humo. Katikati ni Mkuu wa
Wilaya Meatu, Mhe. Fauzia Ngatumbura na wakwanza kushoto ni Katibu Tawala Mkoa
wa Simiyu Mhe. Prisca Kayombo.
Mwakilishi
wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Oscar Maduhu akitoa salamu za TASAF wilayani
Meatu, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo
pichani) yenye lengo la kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi katika
shule ya Sekondari Bukundi wilayani humo.
Baadhi
ya wananchi wa Kijiji cha Bukundi wilayani Meatu wakimsikiliza Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
(hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga
kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la wanafunzi katika shule ya Sekondari Bukundi
wilayani humo.
Mwonekano
wa bweni la wanafunzi wa shule ya Sekondari Bukundi wilayani Meatu,
linalojengwa kwa ufadhili wa TASAF.
No comments:
Post a Comment