Na. James K. Mwanamyoto-Chamwino
Tarehe 18 Septemba, 2022
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah
Chaurembo ameipongeza MKURABITA kwa kuwapatia Hati Miliki za Ardhi za Kimila
wananchi wa Kijiji cha Manyemba wilayani Chamwino, na kuelekeza hati zote
zinazohusisha familia pindi zinapoandaliwa umiliki wake uwe na majina ya akina
mama pia badala ya majina ya akina baba pekee.
Mhe.
Chaurembo ametoa maelekezo hayo akiwa katika Kijiji
cha Manyemba wakati wa ziara ya kikazi ya kamati
yake wilayani Chamwino, iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa
Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) wilayani humo.
Mhe.
Chaurembo amesema, MKURABITA licha ya kutekeleza vizuri wajibu wa kujenga masijala na kuwapatia wananchi wa
kijiji hicho hati miliki za ardhi, lakini wanapaswa kuzingatia kuwa hati zote
za kifamilia umiliki wake uwe na majina ya akina
mama na akina baba kwani wote wana haki sawa katika umiliki wa ardhi.
“Kama
eneo ni la familia, baba na mama wanamiliki hakikisheni majina ya wote wawili
yameandikwa kwenye hati, jina la mama liwepo na la baba liwepo kwani si dhambi
kwa hati moja kuwa na jina zaidi ya moja, hivyo tunapaswa kujenga utamaduni wa
akina mama nao wawe sehemu ya kumiliki ardhi,” Mhe. Chaurembo amesisitiza.
Naye,
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Deogratius Ndejembi amesema kuwa, MKURABITA katika Kijiji cha Manyemba
imefanya kazi kubwa sana ya kutoa hati zilizosaidia kutatua migogoro mingi ya
umiliki wa ardhi.
Mhe.
Ndejembi ameongeza kuwa, mara baada ya MKURABITA kuwezesha upimaji wa ardhi
kwenye kijiji hicho, migogoro mingi na mikubwa ya ardhi imekwisha na kubaki
changamoto ndogo ndogo zinazotatulika ambapo kipindi cha nyuma kulikuwa na
migogoro mikubwa sana ya ardhi.
Mmoja
wa wananchi wa Kijiji cha Manyemba aliyekabidhiwa hati ya kumiliki ardhi, Bw.
Timothy Lesi ameishukuru MKURABITA kwa kuwapatia hati ambazo zitatatua migogoro
ya ardhi inayotokana na wageni katika kijiji chao kuvamia ardhi za wenyeji
jambo ambalo linahatarisha amani iliyopo.
Kwa
upande wake, Mratibu wa MKURABITA, Dkt. Seraphia Mgembe amesema uzinduzi wa
jengo la masijala ni kiashiria cha wananchi wa Kijiji cha Manyemba kuwa karibu
na maendeleo na kuongeza kuwa, mara baada ya MKURABITA kuwapimia mashamba
wananchi wa kijiji hicho tayari wameshawapatia mafunzo kwa kushirikiana na
benki ya NMB na CRDB ya namna gani wanaweza kutumia hati kupata mikopo.
Mpango
wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) umeendelea kuwa
ni sehemu ya utatuzi wa migogoro mingi ya ardhi nchini hususani katika maeneo
ya vijijini.
Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo
(Mb) akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Manyemba
wilayani Chamwino wakati wa ziara ya kikazi ya kamati yake wilayani humo,
iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kurasimisha Rasilimali
na Biashara za Wanyonge (MKURABITA).
Baadhi ya wananchi wa
Kijiji cha Manyemba wilayani Chamwino wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo
(hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo wilayani humo,
iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kurasimisha Rasilimali
na Biashara za Wanyonge (MKURABITA).
Naibu Waziri, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Manyemba wilayani Chamwino, wakati wa
ziara ya kikazi ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa,
iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kurasimisha Rasilimali
na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) wilayani humo.
Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo
(Mb) akimkabidhi hati mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Manyemba wilayani
Chamwino wakati wa ziara ya kikazi ya kamati yake wilayani humo, iliyolenga
kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara
za Wanyonge (MKURABITA). Anayeshuhudia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb).
Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo
(Mb) akizindua jengo la masijala ya ardhi la Kijiji cha Manyemba wilayani
Chamwino wakati wa ziara ya kikazi ya kamati yake wilayani humo, iliyolenga
kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara
za Wanyonge (MKURABITA). Wengine ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi na Mratibu wa
MKURABITA, Dkt. Seraphia Mgembe.
Mkurugenzi wa
Urasimishaji MKURABITA, Bi. Jane Lyimo akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa
majukumu ya MKURABITA kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na
Serikali za Mitaa, wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo katika Kijiji cha
Manyemba wilayani Chamino iliyolenga kukagua utekelezaji wa shughuli za
MKURABITA.
Mratibu wa MKURABITA,
Dkt. Seraphia Mgembe akieleza manufaa ya utekelezaji wa Mpango wa Kurasimisha
Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA) katika Kijiji cha Mayemba
wilayani Chamwino, mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na
Serikali za Mitaa kuhitimisha ziara ya kikazi wilayani Chamwino.
Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo
akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati yake pamoja na wananchi wa
Kijiji cha Manyemba wilayani Chamwino waliokabidhiwa hati, mara baada ya kamati
yake kuhitimisha ziara ya kikazi wilayani humo iliyolenga kukagua utekelezaji
wa shughuli za MKURABITA.
No comments:
Post a Comment