Wednesday, September 7, 2022

KAMATI YA USEMI YARIDHISHWA NA UBORA WA MAFUNZO YA UONGOZI YANAYOTOLEWA NA TAASISI YA UONGOZI ILI KUENDANA NA KASI YA UTENDAJI KAZI ANAOUTAKA MHE. RAIS SAMIA SULUHU HASSAN

Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 07 Septemba, 2022

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo amesema kamati yake imeridhishwa na ubora wa mafunzo yanayotolewa na Taasisi ya UONGOZI kwa viongozi wa umma na maafisa waandamizi ambao wanajengewa uwezo kiutendaji, unaowawezesha kuendana na kasi na azma ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuliletea taifa maendeleo.

Akiongoza kikao kazi cha kamati yake kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya UONGOZI kwa mwaka 2021/2022, Mhe. Chaurembo amesema, Mhe. Constantine Kanyasu ambaye ni mjumbe wa kamati yake amenufaika na mafunzo yaliyotolewa na Taasisi ya UONGOZI na kuonesha mabadiliko makubwa kiutendaji, hivyo ameelekeza kamati ipatiwe mafunzo ya uongozi ili kuongeza ufanisi kiutendaji.

“Sasahivi namuona Mhe. Kanyasu ameiva na ana muonekano halisi wa kiuongozi, tofauti na hapo awali kabla hajapata mafunzo katika Taasisi ya UONGOZI, hivyo na sisi ambao hatukupata fursa hiyo ya mafunzo, tukipatiwa walau mafunzo ya siku mbili, tutapata elimu na ujuzi utakaoboresha utendaji kazi wetu,” Mhe. Chaurembo amesisitiza.

Akielezea umuhimu wa mafunzo aliyoyapata katika Taasisi ya UONGOZI, Mhe. Constantine Kanyasu amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa viongozi mbalimbali kushiriki kwani yana tija kwa taifa hivyo ameungana na Mwenyekiti wa Kamati yake, Mhe. Abdallah Chaurembo kumuhimiza Mhe. Jenista Mhagama kuangalia uwezekano wa Taasisi ya UONGOZI kuipatia mafunzo ya uongozi kamati ya USEMI ili kamati nayo ipate maarifa yatakayoiongezea wigo wa ufanisi kiutendaji.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameielekeza Taasisi ya UONGOZI kujipanga kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wajumbe wa kamati ya USEMI, na kuongeza kuwa ofisi yake iko tayari kutekeleza maelekezo ya Kamati hiyo kwa kutoa mafunzo yatakayokuwa na tija kiutendaji.

Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo amempongeza Mhe. Constantine Kanyasu kwa kuhitimu awamu ya tano ya programu ya Stashahada ya Uzamili iliyoendeshwa na Taasisi ya UONGOZI kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Alto cha nchini Finland.

Bw. Singo ameongeza kuwa, mafunzo hayo yalijikita kwenye masuala ya uongozi wa matokeo, ubunifu, uandaaji wa mpango mkakati na utekelezaji wake, mawasiliano yenye tija, usimamizi wa rasilimaliwatu pamoja na jinsi ya kuongoza mabadiliko.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) imepewa dhamana ya kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na taasisi zilizo chini yake.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo akiongoza kikao cha kamati yake leo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya UONGOZI kwa mwaka 2021/2022. 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa kikao cha kamati hiyo leo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya UONGOZI kwa mwaka 2021/2022.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifafanua hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa kikao cha kamati hiyo leo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya UONGOZI kwa mwaka 2021/2022.


Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Mhe. Constantine Kanyasu akielezea umuhimu wa mafunzo aliyoyapata katika Taasisi ya UONGOZI wakati wa kikao cha kamati hiyo leo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya UONGOZI kwa mwaka 2021/2022.


Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, Mhe. Sebastian Kapufi akichangia hoja wakati wa kikao cha kamati hiyo leo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya UONGOZI kwa mwaka 2021/2022.


Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mhe. Dkt. Alice Kaijage akichangia hoja wakati wa kikao cha kamati hiyo leo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya UONGOZI kwa mwaka 2021/2022.


Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo leo jijini Dodoma kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa mwaka 2021/2022.


 

No comments:

Post a Comment