Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 15 Novemba, 2021
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa ameelekeza mchakato wa ajira katika taasisi zote za umma
nchini uratibiwe na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kama chombo
huru ili kuleta uwazi na kuwezesha haki kutendeka.
Mhe.
Mchengerwa ametoa maelekezo hayo leo jijini Dodoma wakati akizindua Bodi ya
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma iliyopewa dhamana ya kusimamia
mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma.
Mhe.
Mchengerwa amesema amelazimika kutoa maelekezo hayo kwasababu hivi karibuni
baadhi ya waajiri wamekuwa wakiomba vibali vya ajira na kutaka kuendesha
mchakato wa ajira wao wenyewe katika taasisi zao hali inayoondoa uwazi,
ushindani na usawa katika kuendesha mchakato wa ajira.
Amesema
lengo la Serikali ni kuondoa upendeleo unaotokana na undugu, ukabila, udini na
masuala mengine yasiyo ya kimaadili katika mchakato wa ajira kwenye Utumishi wa
Umma.
“Utakuta
baadhi ya taasisi, watumishi wake wameajiriwa kindugu, kidini na kikabila, nikiwa
ndiye Waziri mwenye dhamana ya kusimamia utendaji kazi wa Sekretarieti ya Ajira
katika Utumishi wa Umma, ninataka tuondokane na changamoto hiyo ili twende
kwenye uwazi na haki katika mchakato wa ajira Serikalini kama ambavyo Mhe. Rais
Samia Suluhu Hassan ameelekeza,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe.
Mchengerwa amesema baada ya maelekezo aliyoyatoa, hategemei kusikia taasisi
yoyote ya umma inafanya mchakato wa ajira bila kupitia Sekretarieti ya Ajira
katika Utumishi wa Umma.
Aidha,
Mhe. Mchengerwa amewataka Wajumbe wa Bodi aliyoizindua, kutekeleza majukumu yao
kwa kuzingatia weledi kwani wameaminiwa na Serikali na ndio maana wakapewa
nafasi hizo ili kuisaidia Serikali kupata watumishi wenye uwezo ambao watatoa
mchango kwa maendeleo ya taifa.
Akitoa
neno la Shukrani, Mwenyekiti wa Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi
wa Umma, Bibi Sophia Kaduma amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa
kumuamini na kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo na Mhe. Mchengerwa kwa
kuwateua Wajumbe wa Bodi yake.
Bibi
Kaduma amemhakikishia Mhe. Mchengerwa kuwa wanao uwezo wa kutekeleza majukumu
waliyopewa kwa ufanisi na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za mchakato
wa ajira ili Serikali iweze kupata watumishi watakaoweza kuleta maendeleo
katika taifa.
Akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji wa Ofisi yake, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika
Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi, amesema ofisi yake imefanya maboresho ya
utendaji kupitia TEHAMA inayowezesha kutoa taarifa za ajira kupitia tovuti (www.ajira.go.tz)
tofauti na awali ambapo walilazimika kutangaza ajira kupitia vyombo vya habari.
Bw.
Daudi amesema, tovuti hiyo inatumika kutoa matangazo ya ajira na ufafanuzi wa
masuala mbalimbali yanayohusina na ajira.
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, ilianzishwa kwa mujibu wa Kifungu 29(1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 (iliyorejewa 2019) kwa ajili ya kushughulikia mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza
na Wajumbe wa Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma wakati akizindua bodi hiyo leo jijini Dodoma. Kushoto
kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi na kulia kwake ni Naibu
Katibu Mkuu wa ofisi yake, Dkt. Francis Michael na Mwenyekiti wa Bodi, Bibi
Sophia Kaduma.
Wajumbe wa Bodi ya Sekretarieti ya
Ajira katika Utumishi wa Umma na baadhi ya watendaji wa Sekretarieti wakimsikiliza
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akizindua bodi hiyo leo jijini Dodoma.
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira Katika
Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi akielezea majukumu ya ofisi yake kabla ya
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzindua Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi
wa Umma leo jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Sekretarieti ya
Ajira katika Utumishi wa Umma, Bibi Sophia Kaduma akitoa neno la shukrani kwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa kuzindua bodi hiyo leo jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
akiteta jambo na Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi kabla ya Mhe.
Mchengerwa kuzindua Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma leo
jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa
katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Sekretarieti ya Ajira katika
Utumishi wa Umma mara baada ya kuzindua bodi hiyo leo jijini Dodoma. Waliokaa
kushoto kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi na kulia kwake ni
Naibu Katibu Mkuu wa ofisi yake, Dkt. Francis Michael na Mwenyekiti wa Bodi,
Bibi Sophia Kaduma.
No comments:
Post a Comment