Friday, November 12, 2021

WANUFAIKA WA TASAF JITOKEZENI KUPATA CHANJO YA CORONA MUWE NA AFYA YA KUWAWEZESHA KUBORESHA MAISHA-Mhe. Ndejembi


Na. Veronica Mwafisi-Kongwa

Tarehe 12 Novemba, 2021

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewaasa Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji cha Songambele wilayani Kongwa kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya ugonjwa wa Corona (COVID-19) kwani ni salama na itawasaidia kulinda afya itakayowawezesha kutumia vema ruzuku wanayoipata katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kuboresha maisha yao.

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo kwa wanufaika wa TASAF, akiwa Wilayani Kongwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini zinazoratibibiwa na ofisi yake kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Mhe. Ndejembi amesema, ni jambo lisilokubalika kwa mlengwa wa TASAF ambae bado hajapata bima ya afya kukataa chanjo ya Corona inayotolewa bure na Serikali halafu baadae apate maradhi hayo na kulazimika kutumia fedha anayoipata kwa ajili ya matibabu.

 “Mnufaika wa TASAF asiye na bima ya afya, atakayekataa chanjo ya Corona na kupata ugonjwa huo, ataanza kuumwa hivyo fedha ya TASAF atakayoipata kwa ajili ya kuboresha maisha yake atalazimika kuitumia kwa ajili ya matibabu,” Mhe. Ndejembi amefafanua.

Akizungumzia upotoshwaji unaofanywa kuhusu athari za chanjo ya COVID-19, Mhe. Ndejembi amesema, wananchi wasidanganyike na propaganda zinazofanywa na wenye nia ovu kwani chanjo inayotolewa na Serikali kwa wananchi wake imethibitika kuwa ni salama kiafya.

 “Mimi binafsi nimechanja na mnaniona nipo mbele yenu nikiwa mzima wa afya, sijafa au kunyonyoka nywele kama wapotoshaji wanavyosema,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Akihimiza matumizi mazuri ya ruzuku inayotolewa na TASAF, Katibu Umoja wa Vijana wa CCM Wilaya ya Kongwa Bw. Emmanuel Msemwa amewataka walengwa wa TASAF kuhakikisha fedha wanazozipata zinawasaidia kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayoboresha maisha yao.

“Fedha mnayoipata kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini msiitumie kunywea pombe au kununulia vitu visivyo na msingi wowote kwenye magulio, ambavyo haviwasaidii katika kujenga uchumi,” Bw. Msemwa amehimiza.

Mhe. Deogratius Ndejembi amehitimisha ziara yake kikazi ya siku nne ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Wilaya ya Chamwino na Kongwa.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wanufaika wa TASAF na Wananchi wa Kijiji cha Songambele wilayani Kongwa, akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani humo. 


Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Songambele wilayani Kongwa wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani humo. 


Mtendaji wa Kijiji cha Songambele, Bi. Paulina Ndaga akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ya Kijiji chake wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Ndejembi ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji hicho kilichopo Wilayani Kongwa. 


Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Remidius Mwema akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Ndejembi kuzungumza na wanufaika wa TASAF na Wananchi wa Kijiji cha Songambele wilayani Kongwa, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani humo. 


Mwananchi wa Kijiji cha Songambele wilayani Kongwa, Bw. Peter Makapi akiwasilisha hoja kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani humo. 


Mwananchi wa Kijiji cha Songambele wilayani Kongwa Ndyonya Mgosi akiwasilisha hoja kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani humo. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akijibu hoja zilizowasilishwa na Wananchi wa Kijiji cha Songambele wilayani Kongwa wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wilayani humo. 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akicheza ngoma na Wananchi wa Kijiji cha Songambele wilayani Kongwa alipowasili katika kijiji hicho wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kijijini humo. 


 

No comments:

Post a Comment