Na. James K. Mwanamyoto-TEKEKE
Tarehe 16 Novemba, 2021
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameiomba Benki ya Dunia kuendeleza ushirikiano uliopo wa kuzisaidia kaya maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwasababu umetoa matokeo chanya kwa kuboresha maisha ya kaya maskini nchini.
Mhe.
Mchengerwa ametoa ombi hilo wakati wa ziara ya kikazi ya ujumbe wa Benki ya
Dunia uliolenga kukagua utekelezaji
wa miradi ya TASAF katika Mtaa wa Nzasa A, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke
jijini Dar es Salaam.
Mhe. Mchengerwa amesema lazima Serikali ikiri kuwa
TASAF haijasaidia tu kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja bali imesaidia
kusogeza karibu huduma za kijamii kwa kujenga madaraja, shule na zahanati, hii
yote ni kutaka Watanzania waondokane na umaskini unaosababishwa na maadui
watatu ambao ni umaskini, ujinga na maradhi.
Mhe. Mchengerwa amesema, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa
na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kama ilivyokuwa kwa Serikali ya Awamu
zilizopita ni kuumaliza umaskini kwa Watanzania na ndio maana imejipanga
kuhakikisha watoto wanaotokana na kaya maskini ambao wamefaulu kujiunga na
elimu ya juu wanapatiwa mikopo kwa asilimia mia moja ili elimu watakayoipata
iwasaidie kupambana na umaskini.
Mhe. Mchengerwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Benki ya Dunia
katika kupambana na umaskini na kuongeza kuwa TASAF itabakia kuwa ndio nyenzo
mojawapo ya kuziinua kaya maskini nchini.
“Mhe. Mgeni Rasmi, tutaendelea kushirikiana katika kuboresha maisha ya
Watanzania kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini ili
kuondoa kaya maskini,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Sera za
Maendeleo na Ubia wa Benki ya Dunia, Prof. Mari Pangestu amesema ameona jinsi
TASAF ilivyoboresha maisha ya Watanzania wengi wanaotokana na kaya maskini na
kuongeza kuwa, ni dhahiri TASAF imepunguza kiwango cha umaskini nchini.
“Nikiwaangalia ninawaona mkiwa na afya njema, na
ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kujali afya zenu ili muweze kujishughulisha
na shughuli mbalimbali za maendeleo,” Prof. Pangestu ameongeza.
Prof. Pangestu amemhakikishia Mhe. Mchengerwa kuwa,
Benki ya Dunia itaendeleza ushirikiano na Tanzania katika kupambana na umaskini
kupitia Utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini unaoratibiwa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Mkurugenzi
Mtendaji wa Sera za Maendeleo na Ubia wa Benki ya Dunia, Prof. Mari Pangestu
akizungumza na wajasiriliamali wanaonufaika na TASAF
wa Mtaa wa Nzasa A, Kata ya Kilungule, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini
Dar es Salaam wakati wa ziara ya kikazi ya Ujumbe wa Benki ya Dunia uliolenga
kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika mtaa huo.
Mbunge wa Jimbo la Temeke, Mhe.
Abdallah Chaurembo akizungumza na
wajasiriliamali wanaonufaika na TASAF wa Mtaa wa Nzasa A, Kata ya
Kilungule, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam wakati wa
ziara ya kikazi ya Ujumbe wa Benki ya Dunia uliolenga kukagua utekelezaji wa
miradi ya TASAF katika mtaa huo.
Mnufaika wa Kikundi cha TASAF Vicoba
Group cha Mtaa wa Nzasa A, Kata ya Kilungule, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke
jijini Dar es Salaam, Bibi Glory Paul akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa
kikundi hicho kwa Ujumbe wa Benki ya Dunia ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Sera za Maendeleo na
Ubia wa Benki ya Dunia, Prof. Mari Pangestu wakati wa ziara ya kikazi ya
ujumbe huo uliolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Mtaa huo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Sera za Maendeleo na
Ubia wa Benki ya Dunia, Prof. Mari Pangestu wakiangalia bidhaa za wanufaika wa
TASAF wa Mtaa wa Nzasa A, Kata ya Kilungule, Halmashauri ya Manispaa ya
Temeke jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kikazi ya Ujumbe wa Benki ya
Dunia uliolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika mtaa huo.
No comments:
Post a Comment