Tuesday, November 23, 2021

MHE. NDEJEMBI AWATAKA WATUMISHI KUTOWEKA MASILAHI BINAFSI MBELE KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO

Na. Veronica Mwafisi-Muheza

Tarehe 23 Novemba, 2021

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Watumishi wa Umma kutotanguliza mbele masilahi binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na badala yake wafikirie njia sahihi ya kutekeleza miradi hiyo ili kuleta tija kwa taifa.

Mhe. Ndejembi ameyasema hayo Wilayani Muheza wakati wa ziara yake ya kikazi katika Wilaya hiyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Wilaya hiyo.

Mhe. Ndejembi amesema, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo hivi karibuni ametoa kiasi cha shilingi trilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, vituo vya afya na ununuzi wa vifaa mbalimbali hivyo, watumishi wanaohusika na utekelezaji wa miradi hiyo wasimamie kikamilifu na kwa weledi mkubwa badala ya kufikiria watapata nini kutoka kwenye fedha hizo.

“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akipeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwenye halmashauri, hivyo tulinde rasilimali hizo na kuwa wabunifu katika kuweka njia sahihi za utekelezaji wa miradi hiyo.” Mhe. Ndejembi amesema na kuongeza kuwa mtumishi akiwa mbunifu na kutekeleza majukumu yake kwa weledi anaisaidia Serikali kufikia malengo ya maendeleo kwa taifa.

Aidha, Mhe. Ndejembi amesema kukosekana kwa maadili kwa baadhi ya watu kumesababisha baadhi ya watumishi wanaoajiriwa kutaka maisha mazuri na kumiliki vitu vya gharama hali inayosababisha kuingia kwenye rushwa kutokana na kutamani vitu wasivyokuwa na uwezo navyo.

“Leo hii, kuna watu wakiajiriwa, badala ya kutekeleza kazi kwa weledi, wanataka kesho wamiliki gari na nyumba nzuri, hapo ndipo rushwa na udokozi vinaanza kwasababu ya kutamani vitu ambavyo wanajua kwa muda wao bado,” Mhe. Ndejembi amesisitiza. 

Katika kukabiliana na tatizo hilo, Mhe. Ndejembi amewasistiza waajiri kuwapeleka Chuo cha Utumishi wa Umma Watumishi wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza Serikalini kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yao ili wapate elimu itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuiishi miiko ya Utumishi wa Umma.

Mhe. Ndejembi ameendelea na ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Jiji la Tanga ambapo leo alikuwa Wilayani Muheza.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Wilaya ya Muheza jijini Tanga wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Wilaya hiyo. Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhe. Halima Bulembo na kulia kwake ni Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Rasilimaliwatu na Utawala wa Mkoa wa Tanga, Bw. Sebastian Masanja.


Baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Wilaya ya Muheza jijini Tanga wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Wilaya hiyo.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akisisitiza jambo kwa Viongozi na Watumishi wa Wilaya ya Muheza wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Wilaya hiyo. Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhe. Halima Bulembo na kulia kwake ni Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Rasilimaliwatu na Utawala wa Mkoa wa Tanga, Bw. Sebastian Masanja. 


Mtumishi wa Wilaya ya Muheza kutoka Idara ya Mifugo, Bibi Ruth Mwilongo, akiwasilisha hoja za kiutumishi kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Wilaya hiyo.


 

No comments:

Post a Comment