Saturday, November 27, 2021

TAKUKURU FUATILIENI MATUMIZI YA SHILINGI TRILIONI 1.3 ZILIZOTOLEWA NA MHE. RAIS KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA

 

Na. Veronica E. Mwafisi-Dodoma

Tarehe 27 Novemba, 2021.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameilekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufuatilia matumizi ya shilingi trilioni 1.3 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ustawi wa taifa inayojumuisha ujenzi wa madarasa, zahanati na vituo vya afya.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo, wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka 2021 wa Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) uliofanyika jijini Dodoma kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Morena Hoteli.

Mhe. Ndejembi amesema, viashiria vya rushwa na uvunjifu wa maadili vimeanza kuonekana kwenye baadhi ya maeneo ambayo fedha hizo zimeelekezwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya madarasa, zahanati, vituo vya afya na vifaa tiba.

“Viongozi mbalimbali wa Wilaya na Mikoa katika baadhi ya maeneo wameonekana wakikemea matumizi mabaya ya fedha zilizotolewa na Mhe. Rais, lakini kwenye maeneo mengine viongozi hao hao wanahusika kuhakikisha wanakuwa ni wasambazaji wa vifaa vya ujenzi, hivyo wanaondoa dhana nzima ya utawala bora,” Mhe. Ndejembi amefafanua.

Ameongeza kuwa, kuna maeneo imebainika kwamba tofali zinatolewa zaidi ya kilomita 150 hivyo kuongeza gharama za ujenzi, na kuna maeneo mengine gharama ya tofali moja ni shilingi 1200 lakini wenye nia ovu wanaenda kununua sehemu ambayo linauzwa shilingi 1700, kitendo hicho kinaonesha namna wanavyokwamisha juhudi za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma za kijamii.

Aidha, Mhe. Ndejembi amesema kuwa, yapo maeneo mengine ujenzi wa madarasa unakaribia kuisha lakini maeneo mengine wapo kwenye msingi, na ukiangalia sababu ya kwanini bado wako hatua ya msingi unakuta viongozi hao walikuwa wakivutana kwa masilahi yao binafsi.

“Viongozi wanavutana nani apate nini, nani amlete mzabuni wa tofali au wa saruji na kuna eneo moja mkoani Mara mzabuni huyo huyo ndio msambazaji wa saruji, nondo na mjenzi, hivyo amewataka TAKUKURU kuhakikisha wanachukua hatua ili kukomesha vitendo hivi kwa masilahi ya taifa,” Mhe. Ndejembi amesisitiza. 

Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake kabla ya kumkaribisha Mhe. Ndejembi kufunga Mkutano huo wa mwaka, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni amesema TAKUKURU inalo jukumu la kuhakikisha trilioni 1.3 zilizotolewa hivi karibuni na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Ameongeza kuwa, ni jukumu pia la TAKUKURU kushirikiana na wadau wengine katika kuhakikisha fedha hizo zinafanya kazi ambayo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imekusudia. 

Mkutano Mkuu wa Mwaka 2021 wa Viongozi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) uliofikia tamati leo umefanyika kwa siku tatu kuanzia Novemba 25 hadi 27, 2021 jijini Dodoma.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka 2021 wa Viongozi hao uliofanyika jijini Dodoma kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Morena Hoteli.

 

Baadhi ya Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka 2021 wa Viongozi wa Taasisi hiyo uliofanyika jijini Dodoma kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Morena Hoteli.

 

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi Salum Hamduni akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake kwa mgeni rasmi Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kabla ya Naibu Waziri huyo kufunga Mkutano Mkuu wa Mwaka 2021 wa Viongozi wa TAKUKURU uliofanyika jijini Dodoma kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Morena Hoteli.

 

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi Salum Hamduni wakiwa katika Mkutano Mkuu wa Mwaka 2021 wa Viongozi wa Taasisi ya TAKUKURU (hawapo pichani) kabla ya Naibu Waziri huyo kufunga Mkutano huo uliofanyika jijini Dodoma kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Morena Hoteli.

 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa Mwaka 2021 wa Viongozi wa (TAKUKURU) mara baada ya kufunga Mkutano huo uliofanyika jijini Dodoma kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Morena Hoteli.

 

 

 

No comments:

Post a Comment