Na.
James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 10 Novemba, 2021
Waajiri
wanaoshindwa kuwasilisha vielelezo vya rufaa za Watumishi wa Umma katika Tume
ya Utumishi wa Umma kwa ajili ya kuwezesha maamuzi ya mashauri ya kinidhamu
yaliyowasilishwa katika Tume hiyo, wametakiwa kutoa maelezo ya sababu za
kutowasilisha kwa wakati vielelezo hivyo.
Akizungumza
na Mwenyekiti, Makamishna na Watendaji wa Tume ya Utumishi wa Umma leo jijini Dodoma,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema, haiwezekana Mwajiri amsimamishe kazi Mtumishi
wa Umma na kuchukua hatua za kinidhamu halafu ashindwe kuwasilisha vielelezo
Tume ya Utumishi wa Umma ili haki itendeke.
“Zipo
rufaa nyingi zimewasilishwa Tume ya Utumishi wa Umma bila vielelezo lakini Tume
imekuwa ikilalamikiwa kwa kutoshughulikia kwa wakati rufaa hizo, huku kosa likiwa
ni la mwajiri kwa kutowasilisha vielelezo kwa wakati, hivyo Serikali
haitovumilia jambo hili,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.
Katika
kuhakikisha haki inatendeka kwa Watumishi waliochukuliwa hatua za kinidhamu, Mhe.
Mchengerwa amemuelekeza Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama kuwasilisha
orodha ya Waajiri walioshindwa kuwasilisha vielelezo ili Ofisi yake iwaandikie
barua ya kuwataka kutoa maelezo ya sababu ya kutowasilisha vielelezo vya rufaa
za Watumishi.
Aidha,
Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, Ofisi yake itaandaa Waraka utakaosisitiza
Waajiri kuwasilisha vielelezo vya rufaa kwa wakati na pindi watakaposhindwa,
zitaandaliwa kanuni za kuiwezesha Tume kuendelea kufanya maamuzi kwa kutumia
vielelezo vya upande mmoja ili kuharakisha utoaji wa maamuzi kwa kuzingatia
misingi ya utawala bora.
“Inawezekana
rufaa mlizozifanyia kazi leo ni za hivi karibuni, lakini yapo mashauri mengi
yaliyowasilishwa muda mrefu na mmeshindwa kuyafanyia kazi kwasababu waajiri
hawajawasilisha vielelezo,” Mhe. Mchengerwa ameongeza.
Mhe.
Mchengerwa amesema, lazima Serikali isimamie haki za watumishi kwani ndio
msingi ambao Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza mara kwa mara.
Amesema
Serikali haitosita kuwachukulia hatua za kinidhamu Waajiri wote watakaoshindwa
kuwasilisha vielelezo vya rufaa za Watumishi wa Umma Tume ya Utumishi wa Umma
ambayo ndiyo mamlaka ya nidhamu kwa Watumishi wa Umma.
Akitoa
neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Mchengerwa kuzungumza nao, Mwenyekiti
wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Mhe. Steven Bwana amemhakikishia Mhe.
Waziri kuwa Tume itaendelea kutoa uamuzi wa haki na kutoa elimu kwa Waajiri,
Mamlaka za Ajira na Nidhamu na Watumishi wa Umma kuhusu uzingatiaji wa Kanuni,
Sheria na Taratibu za Kitumishi ili kuhakikisha haki inatendeka.
Ameongeza
kuwa, iwapo Tume na wadau wake watatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Kanuni,
Sheria na Taratibu za Kitumishi, Serikali itaweza kujenga utumishi wa umma uliotukuka,
wenye tija na unaotoa huduma bora kwa wananchi.
Akitoa
neno la shukrani kwa niaba ya Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Kamishna
Khadija Mohammed amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa kuwatembelea na kushuhudia
jinsi wanavyofanya kazi, kitendo kinachoonyesha ni kwa kiasi gani anaheshimu
majukumu ya Tume ambayo yamejikita katika utoaji haki kwa Watumishi wa Umma.
Kamishna
Khadija ameishukuru Serikali kwa kuwaamini na kuwateua kuitumikia Tume kwa
kipindi cha miaka mitatu ambacho wameweza kupitia rufaa na malalamiko
mbalimbali ya kiutumishi yaliyowasilishwa katika Tume hiyo na kuyatatua kwa
njia ya haki.
Mhe. Mchengerwa ameitembelea Tume ya Utumishi wa Umma ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kuhakikisha taasisi zilizo chini ya Ofisi yake zinatekeleza wajibu wake kikamilifu.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akizungumza na Mwenyekiti Makamishna na Watendaji wa
Tume ya Utumishi wa Umma leo jijini Dodoma wakati wa ziara yake ya kikazi ya
kuhimiza uwajibikaji kwa Watendaji wa Tume hiyo.
Kamishna wa
Tume ya Utumishi ya Utumishi wa Umma, Khadija Mohammed akitoa neno la shukrani
kwa Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa baada ya Mhe. Mchengerwa kufanya ziara ya kikazi katika Tume
hiyo jijini Dodoma leo.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akiwasili katika Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Umma iliyopo
UDOM Jijini Dodoma alipofanya ziara ya kikazi katika Tume hiyo. Kushoto kwake
kwake ni Mwenyekiti
wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Mhe. Steven Bwana na kulia kwake ni
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti, Makamishna na
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma alipofanya ziara yake ya kikazi katika Tume
hiyo leo jijini Dodoma.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa akiagana na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji
Mstaafu Mhe. Steven Bwana baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi aliyoifanya
katika Tume hiyo leo jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment