Thursday, November 25, 2021

MHE. RAIS SAMIA ANAAMINI TAKUKURU ITAMSAIDIA KUJENGA TAIFA AMBALO WANANCHI WATANUFAIKA NA RASILIMALI ZILIZOPO

Na. Veronica E. Mwafisi-Dodoma

Tarehe 25 Novemba, 2021 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anaamini kuwa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) itamsaidia kujenga taifa ambalo wananchi anaowaongoza watanufaika na uwepo wa rasilimaliwatu na rasilimali za umma zilizopo pasipo kuombwa wala kutoa rushwa.

Waziri Mchengerwa amesema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka 2021 wa Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) uliofanyika leo jijini Dodoma.

Mhe. Mchengerwa amesema, mapambano dhidi ya rushwa yamejikita katika misingi ya Utawala Bora, hivyo amewataka viongozi wa TAKUKURU kujipanga katika mapambano dhidi ya rushwa ili taifa liwe na watumishi na taasisi za umma zinazotekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya Utawala Bora.

Ameongeza kuwa, moja ya vinyemelea vya rushwa katika Taasisi za Umma ni urasimu wa utoaji wa huduma hivyo kama utoaji wa huduma utazingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo hakuna mwananchi atakayeshawishika kutoa rushwa.

“Anayekwenda kusajili biashara yake BRELA akijua kwamba huduma ya usajili inapatikana ndani ya siku moja na ndani ya muda huo akafanikiwa kusajili biashara yake, hatakuwa na wazo la kutoa rushwa,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.

Katika kutekeleza jukumu la kumsaidia Mhe. Rais kuongoza mapambano dhidi ya rushwa, Mhe. Mchengerwa amewataka watendaji wa ofisi yake kujipanga vema katika kusimamia misingi ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kwa kufanya hivyo taifa litakuwa limefanikiwa katika mapambano dhidi ya rushwa.

Ili kuongeza ufanisi kiutendaji, Mhe. Mchengerwa ameitaka TAKUKURU kushirikiana na Idara ya Ukuzaji wa Maadili, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhakikisha wanapata takwimu sahihi ya namna ambavyo huduma katikaTaasisi za Umma zinatolewa kwa wananchi, na kwa taasisi zitakazobainika kutotoa huduma bora hatua stahiki zichukuliwe kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Salum Hamduni, amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na kufungua kikao kazi cha taasisi yake ambacho kitasaidia kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha utendaji kazi wa TAKUKURU.

Sanjali na hilo, amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa na kwa kutoa maelekezo ya mara kwa mara yenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa taasisi yake.

Mkutano Mkuu wa Mwaka 2021 wa Viongozi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) uliofunguliwa rasmi leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Mohamed Mchengerwa utafanyika kwa siku tatu kuanzia Novemba 25 hadi 27, 2021.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka 2021 wa viongozi wa TAKUKURU uliofanyika jijini Dodoma kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Morena Hoteli.


Baadhi ya Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka 2021 wa Viongozi wa TAKUKURU uliofanyika jijini Dodoma kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Morena Hoteli.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi Salum Hamduni akitoa taarifa ya utekelezaji ya taasisi yake kwa mgeni rasmi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka 2021 wa viongozi wa TAKUKURU uliofanyika jijini Dodoma kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Morena Hoteli.


Muwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Omary Kitenge (katikati) na Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Maadili, Bi. Leyla Mavika (wa kwanza kushoto) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka 2021 wa Viongozi wa TAKUKURU uliofanyika jijini Dodoma kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Morena Hoteli.


Baadhi ya wawakilishi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka 2021 wa viongozi wa TAKUKURU uliofanyika jijini Dodoma kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Morena Hoteli.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akipokea zawadi ya kumbukumbu ya mchango wake katika mapambano dhidi ya rushwa kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi Salum Hamduni wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka 2021 wa Viongozi wa TAKUKURU uliofanyika jijini Dodoma kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Morena Hoteli.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na  baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa Mwaka 2021 wa Viongozi wa TAKUKURU baada ya Waziri huyo kufungua Mkutano huo uliofanyika jijini Dodoma kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Morena Hoteli.



No comments:

Post a Comment