Wednesday, November 10, 2021

WANANCHI WAIPONGEZA OFISI YA RAIS-UTUMISHI KWA KUSIMAMIA MASILAHI YA WATUMISHI WA UMMA YANAYOJENGA MORALI KIUTENDAJI

Na. Nasra Mwondwe-Dodoma

Tarehe 10 Novemba, 2021

Viongozi na Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wamepongezwa na wananchi wa Rufiji kwa kusimamia vema maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuzitaka Taasisi za Umma kuwapatia stahili watumishi kwa wakati hivyo kujenga morali ya kiutendaji kwa Watumishi wa Umma nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rufiji, Mhe. Rajab Mbonde kwa niaba ya wananchi wa Rufiji walioitembelea Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa lengo la kujifunza masuala ya kiutumishi na utawala bora.

Mhe. Mbonde amesema kuwa, kutokana na usimamizi mzuri wa masilahi ya Watumishi wa Umma uliopo hivi sasa, Watumishi wa Umma wamekuwa na morali ya kuendelea kuutumikia umma tofauti na hapo awali.

“Nina hakika leo ukimuuliza Mtumishi wa Umma kama anatamani kuendelea na kazi au apewe stahiki zake ili aachane na utumishi wa umma, atasema anatamani kuendelea na kazi kwasababu Serikali ya sasa inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inazingatia masilahi yao,” Mhe. Mbonde amefafanua.

Ameongeza kuwa, kitendo cha usimamizi mzuri wa masilahi ya Watumishi wa Umma nchini kimeipa heshima kubwa Chama Tawala ambacho ndio chenye jukumu la kuisimamia Serikali katika utekelezaji wa Ilani yake.

Sanjali na hilo, amemuomba Katibu Mkuu-UTUMISHI kuendelea kumsaidia Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma na msaidizi wake ili waweze kutekeleza vema jukumu la kumsaidia Mhe. Rais kusimamia Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Akieleza kuhusu majukumu yanayotekelezwa na ofisi yake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro amesema kwa upande wa Utawala Bora ofisi yake inasimamia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Katika eneo la Utumishi wa Umma, Dkt. Ndumbaro amesema kuwa ofisi yake inashughulika na masuala ya ajira, maadili, upandishwaji wa madaraja, upangaji na uidhinishaji mishahara, uhamisho, usimamizi wa rasilimaliwatu na masuala yote yanayohusu usimamizi wa Utumishi wa Umma nchini.

Ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, Dkt. Ndumbaro amesema Ofisi yake imekasimu baadhi ya madaraka kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Katibu Tawala Mkoa na Wakurugenzi wa Halmashauri.

Dkt. Ndumbaro amefafanua kuwa, Katibu Mkuu-TAMISEMI amekasimiwa madaraka ya uhamisho wa watumishi wa Serikali za Mitaa kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine, Katibu Tawala wa Mkoa amekasimiwa madaraka ya uhamisho wa watumishi kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine ndani ya mkoa na Wakurugenzi wa Halmashauri wamekasimiwa madaraka ya uhamisho wa watumishi ndani ya Halmashauri.

Katibu Mkuu-UTUMISHI amesema, ofisi yake imebaki na madaraka ya kumhamisha mtumishi kutoka Serikali za Mitaa kwenda Serikali Kuu, Kutoka Serikali Kuu kwenda kwenye Taasisi za Umma au kutoka Serikali za Mitaa kwenda kwenye Taasisi za Umma na kutoka Taasisi za Umma kwenda Serikali za Mitaa.

Licha ya kukasimisha madaraka ya uhamisho kwa Katibu Mkuu-TAMISEMI, Katibu Tawala Mkoa na Wakurugenzi wa Halmashauri, Dkt. Ndumbaro amesema ofisi yake inayo mamlaka ya kumhamisha mtumishi yeyote kutoka sehemu moja kwenda nyingine kutokana na mahitaji kwa masilahi ya taifa.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na wananchi wa Rufiji walioitembelea Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa lengo la kujifunza masuala ya kiutumishi na utawala bora.


Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Rufiji wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) wakati akielezea majukumu ya Ofisi yake kwa wananchi hao walioitembelea Ofisi hiyo kwa lengo la kujifunza masuala ya kiutumishi na utawala bora.


Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rufiji Mhe. Rajab Mbonde, akiongea kwa niaba ya wananchi wa Rufiji walioitembelea Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa lengo la kujifunza masuala ya kiutumishi na utawala bora.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akitoa maelezo ya ujenzi ya jengo kubwa la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Rufiji walipotembelea eneo ambalo jengo kubwa la Ofisi hiyo linajengwa katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.


Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Rufiji wakijionea maendeleo ya ujenzi ya jengo kubwa la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora walipotembelea eneo ambalo jengo hilo kubwa la Ofisi hiyo linajengwa katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.


 

No comments:

Post a Comment