Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam
Tarehe 18 Novemba, 2021
Serikali imewataka Waajiri
wote katika taasisi za umma nchini kuhakikisha Watumishi wanaoajiriwa kwenye
taasisi zao wanapata mafunzo elekezi katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania
(TPSC) kabla ya kuanza kazi ili kufikia azma ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu
Julius Nyerere ambaye alitaka Utumishi wa Umma kuwa uliotukuka.
Hayo yamesemwa jijini Dar es
Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akizindua Bodi ya Ushauri ya Chuo
cha Utumishi wa Umma Tanzania.
Mhe. Mchengerwa amesema,
mafunzo watakayoyapata watumishi hao yatasaidia kuwajenga kimaadili, kutambua
na kuiishi miiko ya Utumishi wa Umma, kujua mwelekeo wa Serikali, kuwa na
mienendo sahihi inayotakiwa katika Utumishi wa Umma na kuwajengea uzalendo kwa
taifa.
“Mafunzo haya ni muhimu sana
kwa Watumishi wa Umma kuwajenga kiutendaji kwasababu leo hii ukipita kwenye
taasisi za umma utabaini baadhi ya Watumishi hawako hai kiutendaji kwa sababu
ya kukosa mafunzo elekezi ambayo yangewajengea nidhamu ya utendaji kazi,’’Mhe.
Mchengerwa ameongeza.
Mhe. Mchengerwa ameongeza
kuwa, ukosefu wa mafunzo kwa Watumishi wa Umma yanasababisha baadhi ya
Watendaji na Watumishi kutoelewana kwasababu binafsi hali inayofanya baadhi ya
Watendaji kutowapangia majukumu watumishi walio chini yao hivyo taifa linakosa
mchango wao wakati Serikali inawalipa mshahara.
Katika kushughulikia masuala
ya nidhamu ya Watumishi wa Umma, Mhe. Mchengerwa amewataka Waajiri kuzingatia
taratibu za kushughulikia masuala ya nidhamu ili kulinda haki za Watumishi wa
Umma.
Akitoa neno la utangulizi
kabla ya kumkaribisha Mhe. Mchengerwa kuzungumza na Wajumbe wa Bodi, Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi amesema Chuo cha Utumishi wa Umma kina jukumu kubwa la
kuwajengea uwezo wa kiutendaji Watumishi wa Umma na kuwaandaa wanaoingia kwenye
Utumishi wa Umma ili wawe na mwenendo bora.
Ameongeza kuwa, Chuo hicho
hakitakiwi kushindana na vyuo vingine kwasababu hata wahitimu wa vyuo vingine
wanapaswa kujengewa uwezo kiutendaji na chuo hicho pindi wanapoingia kwenye Utumishi
wa Umma.
Akitoa neno la shukrani,
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma, Dkt. Florens Turuka
amesema Bodi yake inatambua dhamana kubwa waliyopewa na Serikali katika
kuhakikisha Chuo kinatoa mafunzo yatakayojenga Utumishi wa Umma wenye tija
katika maendeleo ya taifa.
Dkt. Turuka amemshukuru Mhe.
Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kushika wadhifa huo pamoja na
Mhe. Waziri Mchengerwa kwa kuwateua Wajumbe wa Bodi yake ambapo ameahidi kuwa
watafanya kazi kwa bidii, juhudi na weledi ili chuo kitimize majukumu yake
kikamilifu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza
na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (hawapo
pichani) wakati akizindua bodi hiyo jijini
Dar es Salaam.
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha
Utumishi wa Umma Tanzania na baadhi ya Watendaji wa Chuo cha Utumishi wa Umma
Tanzania wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) wakati akizindua
bodi hiyo jijini Dar es Salaam.
Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi akitoa maelezo mafupi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzungumza na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo
cha Utumishi wa Umma kabla ya kuzindua bodi hiyo jijini Dar
es Salaam.
Mkuu
wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt.
Selemani Shindika akiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi
yake kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzindua Bodi ya Ushauri
ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo
cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Florens Turuka akitoa neno la shukrani kwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) kwa kuzindua bodi hiyo jijini Dar es
Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
akifurahia jambo na Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi (kushoto kwake)
na Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro (kulia kwake) kabla ya Mhe.
Mchengerwa kuzindua Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania
jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa
akionyesha baadhi ya nyenzo zitakazotumiwa na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya
Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania mara baada ya kuizindua bodi hiyo jijini Dar
es Salaam. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi na
kulia kwake ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro na Mwenyekiti wa
Bodi, Dkt. Florens Turuka.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akiwa
katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa
Umma Tanzania mara baada ya kuzindua bodi hiyo jijini Dar es Salaam. Waliokaa wa
kwanza kushoto kwake ni Naibu Waziri wake, Mhe. Deogratius Ndejembi na kulia
kwake ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro na Mwenyekiti wa Bodi, Dkt.
Florens Turuka
No comments:
Post a Comment