Friday, August 21, 2026

WAZIRI KIKWETE: SERIKALI YAONGEZA TAASISI ZINAZOKAGULIWA KUHUSU UZINGATIAJI WA SHERIA KATIKA UTUMISHI WA UMMA ILI KUIMARISHA UWAJIBIKAJI

Na Lusungu Helela, Morogoro

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amesema Serikali imeongeza idadi ya taasisi zitakazokaguliwa kuhusu uzingatiaji wa sheria katika usimamizi wa utumishi wa umma kutoka 160 mwaka 2025/26 hadi 300 mwaka 2026/27

Mhe. Kikwete ametoa kauli hiyo leo, Ijumaa, Agosti 21, 2026, mkoani Morogoro, wakati akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, mara baada ya kuzindua zoezi la ukaguzi katika halmashauri hiyo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Amesema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha uadilifu, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Amesema ukaguzi huo unafanyika kwa mujibu wa Kifungu cha 12(1)(c) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298, Marejeo ya Mwaka 2023, kwa lengo la kufuatilia na kutathmini kiwango cha uzingatiaji wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika usimamizi wa masuala ya kiutumishi na kiutawala.

Kwa mujibu wa Mhe. Kikwete, ukaguzi huo utasaidia taasisi kubaini na kurekebisha kasoro za kiutendaji, kuimarisha uwajibikaji, kupunguza migogoro ya kiutumishi na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.

Ameongeza kuwa ukaguzi huo utaiwezesha Serikali kupata taarifa kuhusu hali ya utumishi wa umma nchini na kutoa mapendekezo ya kuboresha sera, sheria na kanuni za utumishi wa umma.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kikwete amewataka watumishi wa umma kuzingatia maadili na wajibu wao, huku akiwaagiza waajiri kutoa motisha kwa wanaofanya vizuri na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wanaokiuka maadili ya utumishi.

Amesisitiza kuwa rasilimaliwatu ni msingi muhimu wa maendeleo kwa kuwa ndiyo inayosimamia rasilimali nyingine zote, hivyo inapaswa kusimamiwa kwa ufanisi.

Aidha, Mhe. Kikwete amesema Serikali inaendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa umma kwa kuzingatia uwezo wa bajeti, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola, ameishukuru Serikali kwa kuiwezesha Tume kuendelea kuimarisha shughuli zake, ikiwemo matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kutekeleza majukumu ya ukaguzi.

Amesema matumizi ya teknolojia yamerahisisha kwa kiasi kikubwa kazi ya ukaguzi kwa kuwezesha ukusanyaji, uchambuzi na ufuatiliaji wa taarifa kwa ufanisi zaidi, hivyo kuongeza kasi na ubora wa utekelezaji wa majukumu ya Tume.

Awali, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Nolasco Kipanda, amesema ukaguzi huo ni muhimu katika kubaini maeneo yenye changamoto na kusaidia waajiri kuchukua hatua za kuboresha usimamizi wa rasilimaliwatu. “Lengo ni kuhakikisha waajiri na watumishi wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi,” amesema Kipanda.

Ameongeza kuwa zoezi hilo la ukaguzi linafanyika katika mikoa 16 na linatekelezwa na wataalamu wa Tume hiyo anayoiongoza.

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Bw. Emmanuel Mkongo, amesema halmashauri hiyo itaendelea kushirikiana na Tume ya Utumishi wa Umma kuhakikisha usimamizi wa utumishi unazingatia Sheria na Kanuni zilizopo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro  mara baada ya kuzindua zoezi la ukaguzi katika halmashauri hiyo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akisalimiana na baadhi viongozi  wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na vingozi wa  Tume ya Utumishi wa Umma, mara baada ya kuwasili kwa ajili ya kuzindua zoezi la ukaguzi katika halmashauri hiyo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akisalimiana na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola mara baada ya kuwasili kwa ajili ya kuzindua zoezi la ukaguzi katika halmashauri hiyo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, mara baada ya kuwasili kwa ajili ya kuzindua zoezi la ukaguzi katika halmashauri hiyo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete kwa ajili ya kuzungumza  na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwenye uzinduzi wa zoezi la ukaguzi katika halmashauri hiyo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Nolasco Kipanda akizungumza kabla Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete  kuzungumza  na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwenye uzinduzi wa zoezi la ukaguzi katika halmashauri hiyo,


Baadhi ya watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wakimsililiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati  akizungumza nao mara baada ya kuzindua zoezi la ukaguzi katika halmashauri hiyo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.


 

 

 

 

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment