Thursday, September 25, 2025

KATIBU MKUU MKOMI APOKEA MAKOMBE YA USHINDI MASHINDANO YA SHIMIWI 2025 ASISITIZA UMUHIMU WA MICHEZO KWA WATUMISHI WA UMMA

Na Eric Amani na Antonia Mbwambo, Mtumba Dodoma

Tarehe 24.09.2025

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi, leo Septemba 24, 2025 amepokea makombe ya ushindi yaliyonyakuliwa na timu ya OfisI yake katika Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) 2025, yaliyofanyika jijini Mwanza huku akisisitiza umuhimu wa michezo kwa Watumishi wa Umma nchini.

Akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika sehemu ya wazi ya Ofisi hiyo, Katibu Mkuu Bw. Mkomi amezipongeza timu zote zilizoshiriki katika mashindano hayo ya SHIMIWI jijini Mwanza kwa juhudi na uzalendo waliouonesha hadi kuibuka mabingwa katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu (wanaume) mabingwa nafasi ya kwanza, netiboli (wanawake) nafasi ya tatu, mbio za baiskeli na mchezo wa “darts” walipata ushindi wa nafasi ya tatu kwa jumla, aidha kwenye mbio za kupokeza mita 400 (Relay) mshindi wa kwanza kwa wanawake na wa pili kwa wanaume.

Bw. Mkomi amesema ushindi huo ni ishara ya mshikamano, nidhamu na mazoezi ya muda mrefu ya timu nzima. Amesisitiza kuwa michezo si tu burudani, bali pia ni nyenzo muhimu ya kuimarisha afya, mahusiano kazini na kuongeza ufanisi wa kazi.

“Michezo ni afya, hivyo ninawahimiza Watumishi wa Umma msiache kushiriki michezo kwani afya zenu zikiwa nzuri basi huduma zinatolewa kikamilifu kwa wananchi.” Amesisitiza na kuongeza kuwa pamoja na kuimarisha afya, pia inaleta ushirikiano.

Amesema Ofisi yake imeweka utaratibu wa watumishi kufanya mazoezi kila siku ya Jumanne na Alhamisi, hivyo amewasisitiza watumishi hao kushiriki kikamilifu.

“Utaratibu wa kufanya mazoezi kila Jumanne na Alhamisi tumeuweka makusudi ili kila mmoja ashiriki, hivyo ukifika muda uliopangwa wa kuanza mazoezi wote tunatakiwa kuelekea kwenye mazoezi,” ameongeza.

Pamoja na kuhimiza kushiriki michezo, Katibu Mkuu Mkomi amewataka Watumishi wa Umma kujiepusha na tabia zinazoharibu taswira ya Ofisi. “Haipendezi kuona mtumishi wa umma anafanya mambo ya ajabu huko mtaani, sisi ni kioo, hivyo tunatakiwa kuwa mfano wa kuigwa katika kuzingatia maadili ndani na nje ya ofisi," amesema.

Naye Kiongozi wa timu ya UTUMISHI ambaye ni Afisa Tawala Mwandamizi wa Ofisi hiyo, Bw. Charles Shija kwa niaba ya wanamichezo wote, alimshukuru Katibu Mkuu kwa kuwawezesha kushiriki michezo hiyo na kupata ushindi.

Aidha, Bw. Shija pamoja na wanamichezo hao walitumia fursa hiyo kumkabidhi Katibu Mkuu makombe hayo huku wakiahidi kuendelea kujiimarisha zaidi katika michezo kwa ustawi wa taifa.

 

 


 

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akitoa hotuba fupi kwa watumishi wa Ofisi hiyo katika hafla fupi ya kupokea Makombe ya ushindi wa timu za Ofisi hiyo walioshiriki katika Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara na Wakala wa Serikali, (SHIMIWI) lililofanyika jijini

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi (wanne kutoka kushoto) akipokea kombe la mchezo wa Darts” kutoka kwa Mtumishi wa ofisi hiyo, Bi Loveness Choga (watatu kutoka kulia) wakati wa hafla fupi ya kupokea makombe hayo yaliyopatikana wakati wa mashindano ya michezo ya SHIMIWI.

Mwenyekiti wa Timu za Michezo mbalimbali kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Charles Shija akitoa maneno ya utangulizi kwa Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Bw. Juma Mkomi (hayupo pichani) kuhusu ushindi walioupata katika  mashindano ya SHIMIWI.

Watumishi wa Ofisi ya Rais, UTUMISHI wakiwa nje ya ofisi hiyo tayari kwa kupokea Makombe ya ushindi kutoka kwa washiriki wa mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha ya mbio za kupokezana, darts na mchezo wa baiskeli waliyoyapata katika mashindano ya SHIMIWI yaliyofanyika jijini Mwanza. 


Washiriki wa Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara na Wakala wa Serikali, SHIMIWI kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakiwa wanafurahia Ushindi walioutwaa katika mashindano hayo baada ya kuwasili katika Ofisi hiyo iliyopo Mtumba jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Timu mbalimbali za Michezo kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Charles Shija akikabidhi Kombe la Ubingwa wa Mpira wa Miguu kwa Mgeni Rasmi ambaye ni Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Bw. Juma Mkomi wakati wa hafla fupi iliyofanyika jijini Dodoma

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi (aliyenyanyua kombe) akifurahia ushindi walioupata Watumishi wanamichezo wa ofisi hiyo kwenye mashindano ya michezo ya SHIMIWI.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi akifurahia pamoja na Wakurugenzi wa Idara na Vitengo, Watumishi na timu ya michezo ya ofisi hiyo ushindi wa makombe waliyoyapata kwenye mashindano ya michezo ya SHIMIWI.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi (katikati mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Idara na Vitengo kutoka katika ofisi hiyo na timu ya washiriki wa michezo ya SHIMIWI mara baada kupokea makombe ya ushindi ya mashindano ya michezo ya SHIMIWI.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi (watano kutoka kulia) akipokea kombe la mchezo wa Baiskeli kutoka kwa Mtumishi wa Ofisi hiyo, Bw. Hassan Ligoneko (wasita kutoka kulia) wakati wa hafla fupi ya kupokea makombe ya ushindi ya mashindano ya michezo ya SHIMIWI.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi akiwa ameongozana na baadhi ya Wakurugenzi wa Ofisi hiyo mara baada ya kupokea makombe ya ushindi ya mashindano ya michezo ya SHIMIWI.

Watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI wakionyesha makombe ya ushindi kwa Katibu Mkuu wa ofisi hiyo Bw. Juma Mkomi (hayupo pichani) waliyoyapata katika mashindano ya michezo ya SHIMIWI.

 Watumishi wa Ofisi ya Rais, UTUMISHI wakiwa nje ya ofisi hiyo tayari kwa kupokea Makombe ya ushindi kutoka kwa washiriki wa mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha ya mbio za kupokezana, darts na mchezo wa baiskeli waliyoyapata katika mashindano ya SHIMIWI yaliyofanyika jijini Mwanza. 

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi (kulia) akiwa anateta jambo na Mkurugenzi Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bw. Musa Magufuli (kushoto) wakati wa hafla fupi ya kupokea makombe ya ushindi walioupata katika michezo ya SHIMIWI.

Mlezi wa Timu za michezo mbalimbali kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi Mwanadawa Nchemwa (watano kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi ambaye ni Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Bw. Juma Mkomi (watatu kutoka kushoto) baada ya kukabidhi Kombe la Ushindi uliotokana na mchezo wa netiboli wakati wakati wa mashindano ya SHIMIWI.

No comments:

Post a Comment