Na. Veronica E. Mwafisi-Dodoma
Tarehe 26 Novemba, 2022
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi amewataka wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kuishi
kwa kuzingatia maadili ya kitanzania ili kutimiza malengo yao kitaaluma na
kujenga taswira nzuri ya chuo katika jamii.
Mhe. Ndejembi ametoa nasaha hizo jijini Dodoma, wakati akifunga Kongamano la Kukuza Maadili
na Elimu ya Mapambano Dhidi ya Rushwa kwa wanafunzi na wafanyakazi wa chuo
hicho lililofanyika katika ukumbi wa Chimwaga.
Mhe. Ndejembi amesema kuwa
Serikali ya Awamu ya Sita imejipambanua kusimamia utawala bora, kuzingatia
maadili na ndio maana inapinga vitendo vya rushwa hivyo, wanafunzi wa UDOM
wanapaswa kuzingatia maadili mema kwa lengo la kujenga taswira nzuri ya chuo,
ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan za
kujenga taifa lenye uadilifu.
“Mnapaswa kuishi kwa
kuzingatia maadili ya Kiafrika na Kitanzania kwa sababu tabia zote mbaya
mtakazozifanya, jamii haitowaelewa na itakishushia hadhi Chuo Kikuu cha Dodoma
ambacho Serikali inakitegemea katika kuzalisha rasilimaliwatu yenye tija katika
maendeleo ya taifa,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa,
hata chuo kikiendelea kuwa na matokeo mazuri ya wanafunzi kwa kiwango kikubwa
lakini wanafunzi na watumishi wa chuo wasipoishi kwa kuzingatia maadili itakuwa
ni sawa na kazi bure kwani hakitakuwa na hadhi mbele ya jamii.
Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka
wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kuwa mabalozi wazuri wa kupinga vitendo vya
rushwa katika kipindi chote wanapokuwa chuoni na hata baada ya kuhitimu.
Mhe. Ndejembi amewataka washiriki
wa kongamano hilo, kuhakikisha wanafanya mjadala utakaolenga kulinda na kukuza maadili
kwa maslahi mapana na mustakabali wa maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mhandisi Joseph Mwaiswelo amesema kuwa, vitendo vya rushwa vikipuuzwa vitaathiri
taifa kimaadili na kukwamisha juhudi za maendeleo.
Naye, Mmoja wa wanafunzi wa
Chuo Kikuu cha Dodoma, Bw. Henry Magodi kwa niaba ya wenzie, amemshukuru Mhe.
Ndejembi kwa kuwahimiza kuzingatia maadili na kupinga vitendo vya rushwa ili
wawe ni sehemu ya watanzania wazalendo wenye nia thabiti ya kutoa mchango wa
maendeleo katika taifa.
Kongamano hilo la Kukuza Maadili na Elimu ya
Mapambano Dhidi ya Rushwa lililofungwa na Mhe. Deogratius Ndejembi, ni
sehemu ya Maadhimishio ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu ambayo kilele
chake ni tarehe 10 Disemba, 2022.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma walioshiriki
Kongamano la Kukuza Maadili na Elimu ya Mapambano Dhidi ya Rushwa lililofanyika
katika ukumbi wa Chimwaga Jijini Dodoma.
Baadhi ya Wanafunzi na
Watumishi wa Chuo Kikuu cha Dodoma wakimsikiliza Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao wakati akifunga Kongamano la Kukuza Maadili na Elimu ya Mapambano Dhidi ya
Rushwa katika ukumbi wa Chimwaga Jijini Dodoma.
Mwakilishi
wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),
Mhandisi Joseph Mwaiswelo akitoa salamu za Mkurugenzi Mkuu wa (TAKUKURU) kwa Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi, wakati wa Kongamano
la Kukuza Maadili na Elimu ya Mapambano Dhidi ya Rushwa kwa wanafunzi na
wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Dodoma lililofanyika katika ukumbi wa Chimwaga.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka akimkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na washiriki wa Kongamano la Kukuza Maadili na Elimu ya Mapambano Dhidi ya Rushwa lililofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma katika ukumbi wa Chimwaga Jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora, Bw. Patrick Ntwina, akitoa neno la utangulizi kabla ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kufunga Kongamano la Kukuza Maadili na Elimu ya Mapambano Dhidi ya
Rushwa kwa wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa
katika picha ya pamoja na Jumuiya wa Wanafunzi Wapinga Rushwa ya Chuo Kikuu
Dodoma mara baada ya kufungua Kongamano la Kukuza Maadili na Elimu ya Mapambano
Dhidi ya Rushwa lililofanyika katika ukumbi wa Chimwaga Jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment