Tarehe 02 Novemba, 2022
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema, mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND ulioanzishwa na Serikali kupitia Watumishi Housing Investments (WHI), ni matokeo ya utawala bora wa Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan uliolenga kuwawezesha Watanzania wenye kipato cha chini kuwekeza ili kupata mitaji itakayoboresha maisha yao.
Mhe. Ndejembi amesema hayo jijini Dar
es Salaam, wakati akizindua mauzo ya vipande vya mfuko wa uwekezaji wa pamoja
wa FAIDA FUND ulioanzishwa na Watumishi Housing Investments (WHI) iliyo chini
ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mhe. Ndejembi amesema, Serikali ya
Awamu ya Sita inaongoza kwa kusimamia misingi ya utawala bora na ndio maana
kupitia Watumishi Housing Investments (WHI) imekuja na mfuko huu wa FAIDA FUND
ambao ni wa uhakika zaidi kwa wananchi kuwekeza kwani fedha yao inakuwa kwenye
mikono salama.
“Tumeoneshwa mfumo hapa ambao
umetengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ambao unamuwezesha mwananchi
kufuatialia fedha yake na kuona faida atakayoipata, hivyo unamhakikishia
mwananchi usalama wa vipande alivyonunua ili kuwekeza,” Mhe. Ndejembi
amesisitiza.
Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, uwepo
wa Benki ya CRDB kama msimamizi wa masuala yote ya uwekezaji wa fedha kwenye
mfuko huo wa FAIDA FUND unaondoa mashaka na hofu ya wananchi wenye kipato cha
chini wenye nia ya kuwekeza kwenye mfuko huo.
Aidha, Mhe. Ndejembi amesema kuwa
FAIDA FUND ni fursa kubwa sana kwa watumishi wa umma wanaotamani kuingia katika
uwekezaji kwani siku za nyuma uwekezaji ulikuwa ukitafsiriwa ni kwa watu wenye
kipato kikubwa, lakini kupitia kiwango rafiki cha uwekezaji kilichowekwa na
FAIDA FUND kinafungua milango ya watumishi wa umma kuwekeza.
“Kiwango cha awali cha uwekezaji
kuanzia shilingi 10,000/= ambacho FAIDA FUND imekuja nacho kinamuwezesha
mtumishi wa umma kufungua akaunti na kuendelea kuwekeza kwa shilingi 5,000/=,
pia kinayawezesha kuwekeza makundi mengine yanayofanya kazi katika sekta isiyo
rasmi yakiwemo ya bodaboda, mama lishe na mengineyo,” Mhe. Ndejembi amefafanua.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa
Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko, Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Charles
Shirima amesema mfuko wa FAIDA FUND umepata idhini ya mamlaka hiyo kuendeshwa
na kuongeza kuwa, ni mmoja wa mfuko wa uwekezaji wa pamoja unaowezesha
wawekezaji wa aina zote wakiwemo wadogo, wa kati na wakubwa kuwekeza kwa lengo
la kupata faida na kuchangia katika uchumi wa nchi.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa
Watumishi Housing Investments (WHI), Dkt. Fred Msemwa ambaye taasisi yake
imeanzisha mfuko huo wa FAIDA FUND amesema kuwa, FAIDA FUND itawawezesha watu
wenye kipato kidogo kuweka akiba itakayozaa na baadae kuuza vipande vyake na
kununua kiwanja au nyumba au kufanya shughuli nyingine ya kiuchumi kadiri
atakavyoona yafaa.
Mfuko wa FAIDA FUND ni mpango ulio wazi ambao unatoa fursa ya uwekezaji kwa Watanzania hasa wa kipato cha chini kupitia uwekezaji katika vipande ili kupata mapato shindani kupitia ukuaji wa mitaji na kutengeneza utamaduni wa kuwekeza katika Masoko ya Mitaji na Fedha.
Baadhi ya wadau wa Watumishi Housing
Investments (WHI) wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani)
wakati akizindua mauzo ya vipande vya mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA
FUND jijini Dar es Salaam, ulioanzishwa na WHI ili kuwawezesha Watanzania wenye
kipato cha chini kupata mitaji itakayoboresha maisha yao.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizindua
mauzo ya vipande vya mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND jijini Dar es
Salaam, ulioanzishwa na Watumishi Housing Investments (WHI) ili kuwawezesha Watanzania
wenye kipato cha chini kupata mitaji itakayoboresha maisha yao.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya
Watumishi Housing Investments (WHI) CPA Hosea Kashimba akitoa neno la
utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzindua mauzo ya
vipande vya mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND jijini Dar es Salaam, ulioanzishwa
na WHI ili kuwawezesha Watanzania wenye kipato cha chini kupata mitaji
itakayoboresha maisha yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi
Housing Investments (WHI), Dkt. Fred Msemwa akieleza manufaa ya mfuko wa
uwekezaji wa pamoja wa FAIDA FUND kabla ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
kuzindua mauzo ya vipande vya mfuko huo jijini Dar es Salaam, ulioanzishwa na
WHI ili kuwawezesha Watanzania wenye kipato cha chini kupata mitaji
itakayoboresha maisha yao.
Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa
Mamlaka ya Masoko, Mitaji na Dhamana (CMSA), Bw. Charles Shirima akiwasilisha
salamu za Mtendaji Mkuu wa CMSA wakati wa
uzinduzi wa mauzo ya vipande vya mfuko wa uwekezaji wa pamoja wa FAIDA
FUND jijini Dar es Salaam, ulioanzishwa na WHI ili kuwawezesha Watanzania wenye
kipato cha chini kupata mitaji itakayoboresha maisha yao.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akifuatilia maelezo
ya namna mfumo wa FAIDA FUND unavyofanya kazi.
No comments:
Post a Comment