Friday, November 25, 2022

WAHITIMU TPSC WATAKIWA KUTUMIA ELIMU YAO KUFANYA KAZI KWA UFANISI ILI KUWA NA TIJA KATIKA MAENDELEO YA TAIFA


Na. James K. Mwanamyoto-Mtwara

Tarehe 25 Novemba, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka wahitimu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kutumia elimu na ujuzi walioupata  kufanya kazi kwa ufanisi ili kuwa na tija kiutendaji mahala pa kazi, ikiwa ni pamoja na kutoa mchango katika maendeleo ya taifa. 

Mhe. Jenisa ametoa wito huo kwa wahitimu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) wakati wa Mahafali ya 36 ya chuo hicho yaliyofanyika katika Kampasi ya Mtwara. 

Mhe. Jenista amesema, wahitimu hao ambao baadhi yao ni watumishi wa umma na watakaoajiriwa hapo baadae, wahakikishe elimu waliyoipata isiishie kwenye kutunukiwa vyeti tu bali waitumie katika kufanya kazi kwa bidii, weledi na ufanisi mkubwa ili kuleta tija kiutendaji katika maeneo yao ya kazi. 

“Serikali inatarajia kuwa wahitimu wote mtakuwa watendaji kazi mahiri na wenye tija katika maendeleo ya taifa kwani tunaamini kwamba mmepata mafunzo mazuri ambayo yamewawezesha muive kimaadili na kiutendaji,” Mhe. Jenista amesisitiza. 

Aidha, Mhe. Jenista amewataka wahitimu hao kuwa mabalozi wazuri wa kukitangaza Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) katika jamii ili kiendelee kuaminiwa na kutumika katika kutoa mafunzo yatakayoimarisha Utumishi wa Umma nchini. 

“Tusingependa taswira nzuri ya chuo chetu cha Utumishi wa Umma iharibiwe na kuchafuliwa na baadhi ya wahitimu ambao kwa mapungufu yao wenyewe watashindwa kuiishi miiko na maadili waliyofundishwa wakati wakiwa hapa chuoni,” Mhe. Jenista amehimiza. 

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Ahmed Abbas amesema kuwa, mkoa wake una vyuo visivyopungua 10 lakini anajisikia fahari ya uwepo wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Mtwara kwani Kampasi hiyo ni mfano wa kuigwa kimaadili kwa jinsi wanavyovaa na kuishi vizuri na jamii inayowazunguka. 

“Mimi ninaishi jirani na chuo, kila siku ninakutana na wanafunzi wa Kampasi hii ya Mtwara wakielekea chuoni hakika wanavaa vizuri na kuakisi taswira halisi ya utumishi wa umma na Serikali kwa ujumla, hivyo wanapaswa kuigwa na vyuo vingine,” Mhe. Kanali Abbas amesisitiza. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Dkt. Emmanuel Shindika amesema, chuo chake kinatoa mafunzo kwa mitaala inayokidhi matakwa ya soko na kuzingatia umahiri, na kuongeza kuwa kwa sasa chuo kinatoa elimu ya  kuanzia ngazi ya astashahada mpaka shahada. 

Jumla ya wahitimu 6,315 kutoka Kampasi za Dar es Salaam, Tabora, Mtwara, Singida, Tanga na Mbeya wametunikiwa vyeti kwenye Mahafali ya 36 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) katika kozi mbalimbali kwa ngazi ya Astashahada ya Awali, Astashahada, Stashahada na Shahada ya Kwanza. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa kozi mbalimbali wakati wa mahafali ya 36 ya Chuo cha Utumishi wa Umma yaliyofanyika mkoani Mtwara.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na wahitimu wa kozi mbalimbali (hawapo pichani) wakati wa mahafali ya 36 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika mkoani Mtwara.


Sehemu ya wahitimu wa kozi mbalimbali katika mahafali ya 36 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa mahafali ya 36 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika mkoani Mtwara.


Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Ahmed Abbas akitoa salamu za mkoa wake kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzungumza na wahitimu wa kozi mbalimbali katika mahafali ya 36 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika mkoani Mtwara.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akitoa neno kuhusu mahafali ya 36 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika mkoani Mtwara.


Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Florens Turuka akitoa neno la utangulizi wakati wa mahafali ya 36 ya Chuo cha Utumishi wa Umma yaliyofanyika mkoani Mtwara.


Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Selemani Shindika akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake wakati wa mahafali ya 36 ya Chuo cha Utumishi wa Umma yaliyofanyika mkoani Mtwara.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akitunuku cheti kwa mmoja wa wahitimu waliofanya vizuri katika masomo yao wakati wa mahafali ya 36 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika mkoani Mtwara.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro mara baada ya kuhitimisha mahafali ya 36 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika mkoani Mtwara.


 

No comments:

Post a Comment