Na.
Veronica Mwafisi - Kigoma
Tarehe 15 Novemba, 2022
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka
walengwa wa TASAF Kata ya Rusimbi, Mtaa wa Kawawa na Taifa kuboresha maisha yao
kupitia ruzuku wanayoipata ili kutomuangusha Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan
ambaye amefanya jitihada za kutafuta fedha na kuongeza muda wa kutekeleza
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini hadi kufikia mwaka 2025 badala ya mwaka
2023 ambao ndio ulikuwa ni ukomo wa utekelezaji wa mpango huo.
Mhe. Ndejembi ametoa wito huo,
kwa wananchi na walengwa wa TASAF wa Kata ya Rusimbi Kigoma Ujiji, wakati wa
ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Mhe. Ndejembi amesema, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya jitihada za
kutafuta fedha na kuongeza muda wa kutekeleza mpango wa TASAF, ili kuwasaidia
watanzania kutoka katika hali duni ya maisha na kuwa na maisha bora.
Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa,
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa upande wake ameshatekeleza wajibu wake kwa kuwajali
wananchi ambao ni walengwa wa TASAF na ndio maana utekelezaji wa mpango wa
TASAF utaendelea hadi mwaka 2025, hivyo umebakia wajibu wa walengwa wa TASAF kuhakikisha
wanaboresha maisha yao na kumuunga mkono Mhe. Rais kuliletea taifa maendeleo.
Kwa upande wake, Mratibu wa
TASAF Manispaa Kigoma Ujiji Bw. Isaac Vyabandi amemueleza Mhe. Ndejembi kuwa,
TASAF imekuwa ni chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wenye kipato cha
chini mkoani humo, na kuongeza kuwa tangu mwaka 2014 ambapo mpango huo ulianza kutekelezwa
katika Manispaa ya Kigoma Ujiji jumla ya shilingi bilioni 15 zimepokelewa na
kuwanufaisha walengwa.
Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa mikoa ambayo imenufaika na ruzuku inayotolewa kupitia Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini, unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wananchi wa Kata
ya Rusimbi, Mtaa wa Kawawa na Taifa mkoani
Kigoma wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Wananchi
wa Kata ya Rusimbi, Mtaa
wa Kawawa na Taifa mkoani
Kigoma wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
(Wakwanza kulia) wakati akizungumza nao alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi
ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri ya
Wilaya ya Kigoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Mhe. Ester Mahawe akimkaribisha Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Deogratius Ndejembi kuzungumza na wananchi
wa Kata
ya Rusimbi, Mtaa wa Kawawa na Taifa mkoani
Kigoma wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu
Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya
Maskini kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.
Mwakilishi
wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bi. Catherine Kisanga akielezea utekelezaji wa
majukumu ya TASAF katika Halmashauri ya Mkoa wa Kigoma wakati wa ziara ya
kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi yenye lengo la
kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri hiyo.
No comments:
Post a Comment