Na. Veronica E. Mwafisi-Kasulu
Tarehe 16 Novemba, 2022
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka walengwa wa Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini kuendelea kuboresha maisha yao kwa kutumia fursa ya uwepo
wa mikopo ya vikundi ya asilimia kumi (10%)
inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri, iliyotengwa kwa ajili ya
kukopesha vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu kwa uwiano wa asilimia 4:4:2.
Mhe. Ndejembi ametoa wito huo kwa walengwa wa TASAF wakati
akizungumza na wananchi na walengwa wa mpango huo katika Kijiji cha Nyakitonto,
Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, akiwa katika ziara yake ya
kikazi wilayani humo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru
Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwenye wilaya
hiyo.
Mhe. Ndejembi amewahimiza walengwa wa TASAF nchini,
kujiongezea mtaji kupitia mikopo ya asilimia kumi inayohusisha vikundi vya
wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ili waweze kufanya
shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazowaongezea kipato na kuboresha maisha
yao.
“Licha ya kuwa mna
vikundi vyenu vya kuweka na kukopa, vilevile mjitahidi kukopa mikopo ya
asilimia kumi ya Halmashauri ili muitumie kuboresha maisha yenu, kwani Wakurugenzi
walishaelekezwa kutoa kipaumbele pia kwa walengwa wa TASAF wenye sifa ya
kukopesheka,’’ Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaac
Mwakisu, amemshukuru Naibu Waziri Ndejembi kwa kufanya ziara katika Halmashauri
ya Kasulu ili kuwahimiza walengwa wa TASAF kutumia ruzuku vizuri katika
kuboresha maisha yao, na kuahidi kuwa wilaya yake itaendelea kusimamia
utekelezaji wa mpango wa TASAF ili kuunga mkono kwa vitendo azma ya Mhe. Rais
Samia Suluhu Hassan ya kuboresha maisha ya kaya maskini nchini.
Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bi.
Catherine Kisanga amesema kuwa, TASAF inategemea walengwa wataunda vikundi vitakavyowawezesha
kupata mikopo na kuanza kufanya shughuli za kuwaongezea kipato ili kuondokana
na umaskini.
Walengwa
wa TASAF wamehimizwa kuichangamkia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na
Halmashauri nchini, ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Fedha ya Serikali za
Mitaa Sura 290 ya Mwaka 2019, iliyotungwa Chini ya Kifungu 37A (4) pamoja na
Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo ya Asilimia 10 ya mapato ya ndani za
Mwaka 2019 na Marekebisho yake ya Mwaka 2021, inayozitaka Mamlaka za Serikali
za Mitaa nchini kutenga fedha asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya
kukopesha vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu kwa uwiano wa asilimia
4:4:2.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza
na walengwa wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Nyakitonto katika Halmashauri ya
Wilaya ya Kasulu wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye Halmashauri hiyo.
Walengwa
wa TASAF na wananchi wa Kijiji cha Nyakitonto katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu
wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo
iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwenye
Halmashauri hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu
akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi mara baada ya Naibu
Waziri huyo kuzungumza na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
kwenye Kijiji cha Nyakitonto, Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma
wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru
Kaya Maskini katika halmashauri hiyo.
Mwakilishi
wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bi. Catherine Kisanga
akitoa salamu za TASAF kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wakati
wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi iliyolenga
kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kijiji cha
Nyakitonto Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
No comments:
Post a Comment