Na.
Veronica E. Mwafisi-Kigoma
Tarehe 15 Novemba, 2022
Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi amekemea tabia ya baadhi ya waajiri katika Taasisi za Umma
kuficha barua za uhamisho wa watumishi wa umma ambao Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ameridhia na kutoa kibali cha uhamisho
ili wakautumikie umma katika maeneo mengine ya nchi ambayo mamlaka imeona kuna
uhitaji.
Akizungumza na Watumishi wa
Umma wa Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji na Halmashauri ya Wilaya ya
Kigoma, Mhe. Ndejembi amesema, waajiri na Maafisa Utumishi wanapaswa kutenda
haki kwa watumishi wa umma ambao wanastahili kuhama baada ya kupatiwa kibali
cha uhamisho na mwenye mamlaka ambaye ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, na si kufichiwa
barua zao za uhamisho kwa lengo la kukwamisha mchakato wa uhamisho.
“Waajiri na Maafisa Utumishi tendeni haki kwa
watumishi wa umma ambao wanastahili kuhama baada ya uhamisho wao kuridhiwa na
mamlaka, tusifiche barua zao kwani kitendo hicho kinakwenda kinyume na mamlaka
na ni kinyume cha Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma
iliyopo,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, wapo
watumishi wa umma ambao wamefanya kazi kwa muda mrefu katika kituo kimoja cha
kazi, hivyo mamlaka kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu-UTUMISHI ikaamua kumpeleka
mtumishi huyo katika eneo lingine la kazi ili abadili mazingira ya kazi ambayo
yatamuongezea ufanisi kiutendaji, lakini baadhi ya waajiri hukwamisha uhamisho
huo wakati mamlaka iliridhia baada ya kufanya uchambuzi yakinifu.
Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka
waajiri katika Taasisi za Umma kutopitisha barua za kuomba uhamisho za
watumishi ambao ni ajira mpya, kwani ajira zao hazina muda mrefu na baadhi yao
wanakuwa hawajathibitishwa kazini, hivyo kutotimiza kigezo cha kutumikia miaka
mitatu tangu waajiriwe.
Kwa upande wake, Mkuu wa
Wilaya ya Kigoma, Mhe. Ester Mahawe amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuhimiza
uwajibikaji, kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi ikiwa ni
pamoja na kutatua kero na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili watumishi
walio katika wilaya yake.
Mhe. Mahawe, amewahimiza
watumishi wa umma walio katika eneo lake la utawala, kufanya kazi kwa bidii na
weledi kama alivyoelekeza Mhe. Ndejembi ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono kwa
vitendo Kaulimbiu ya KAZI IENDELEE ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Naye, Mtumishi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Kigoma Ujiji, ambaye ni Afisa Utumishi, Bw. Stafordi Bidebuye amemshukuru
Mhe. Ndejembi kwa kwa kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi,
ikiwa ni pamoja na kutatua kero na changamoto zilizokuwa zikiwakabili watumishi
wa Halmashauri hiyo kwa muda mrefu.
Mhe. Bidebuye amesema kupitia
elimu ya masuala ya kiutumishi waliyoipata kutoka kwa Mhe. Ndejembi, anaamini
Mkoa wa Kigoma utafunguka katika kila sekta na kupata maendeleo chini ya
uongozi makini wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameanza
ziara ya kikazi mkoani Kigoma yenye lengo kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa
umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini
unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma
na watumishi
wa Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji (hawapo
pichani), akiwa katika ziara yake ya kikazi yenye lengo kuhimiza uwajibikaji na
kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma walio katika halmashauri
hizo.
Watumishi wa Umma wa Halmashauri
ya Wilaya ya Kigoma na watumishi
wa Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji wakimsikiliza
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi
(hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi
iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa
halmashauri hizo.
Mkuu wa
Wilaya ya Kigoma, Mhe. Ester Mahawe akitoa neno la utangulizi kabla ya
kumkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius
Ndejembi kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na watumishi wa
Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji
(hawapo pichani), wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza
uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma walio katika
halmashauri hizo.
Afisa Mifugo, Kilimo na Uvuvi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Bw. Evans Mdee akiwasilisha hoja kwa
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani), wakati wa ziara ya kikazi ya
Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto
zinazowakabili watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na watumishi wa
Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati)
akisikiliza hoja iliyokuwa ikiwasilishwa na mtumishi wa Manispaa ya Kigoma, wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga
kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma wa Halmashauri
hiyo. Kushoto kwake ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma, Bw. Ntime Mwalyambi
na kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mhe. Ester Mahawe.
No comments:
Post a Comment