Thursday, November 10, 2022

MHE.JENISTA NA MHE. KAIRUKI WAWEKA MKAKATI KUTEKELEZA MAELEKEZO YA MHE. RAIS YA KUIMARISHA MAADILI KATIKA UTUMISHI WA UMMA

 Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma

Tarehe 10 Novemba, 2022 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Angellah Kairuki wamefanya kikao kazi cha kujadili namna ya kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha maadili katika utumishi wa umma aliyoyatoa wakati wa Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 mkoani Kagera.

Akiongoza kikao kazi hicho, Mhe. Mhagama amesema, wameona ni vema wakakutana pamoja na watendaji wa ofisi zao ili kuwa na mtazamo wa pamoja na mkakati madhubuti utakaowezesha kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais ya kuimarisha maadili ya kiutendaji katika utumishi wa umma ili uwe na tija katika usimamizi wa miradi ya maendeleo nchini. 

Mhe. Mhagama amesema, kikao kazi hicho kitatoa mwelekeo wa namna  TAKUKURU itakavyotekeleza jukumu la kuzuia  na kupambana na vitendo vya rushwa ili visiathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo Mhe. Rais amekuwa mstari wa mbele kutafuta fedha kwa wadau wa maendeleo ili ziwanufaishe wananchi. 

“Mhe. Rais amekuwa akitafuta fedha kwa hali na mali ili ziwanufaishe wananchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo ni wajibu wa ofisi yangu na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa,” Mhe. Mhagama amesisitiza.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Angellah Kairuki amesema kikao kazi hicho kitawezesha kuwa na Rasilimialiwatu yenye uwezo wa kusimamia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuwa na mifumo imara ya usimamizi wa fedha hizo. 

Mhe. Kairuki ameongeza kuwa, Ofisi yake itashirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika kusimamia maadili ya watumishi wa umma waliopewa dhamana ya kutekeleza miradi ya maendeleo. 

Akiwasilisha mpango kazi wa namna ya kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais katika mapambano dhidi ya rushwa, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bi. Neema Mwakalyelye amesema TAKUKURU imeandaa programu ya TAKUKURU RAFIKI inatakayowawezesha wananchi kushiriki katika kuzuia vitendo vya rushwa.

Bi. Mwakalyelye ameongeza kuwa, programu hiyo shirikishi ambayo inatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni itawajengea uwezo wananchi katika kutambua miradi ya maendeleo iliyopo, kubaini mianya ya rushwa ili kuhakikisha fedha za umma hazipotea na zinatumika katika kuleta maendeleo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiongoza kikao kazi leo jijini Dodoma kilichowakutanisha watendaji wa Ofisi yake na Ofisi ya Rais-TAMISEMI ili kuweka mkakati wa kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa hivi karibuni ya kuboresha maadili katika utumishi wa umma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Angellah Kairuki akizungumza kwenye kikao kazi leo jijini Dodoma kilichowakutanisha watendaji wa Ofisi yake na Ofisi ya Rais-UTUMISHI ili kuweka mkakati wa kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa hivi karibuni ya kuboresha maadili katika utumishi wa umma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Angellah Kairuki wakiwa katika kikao kazi na watendaji wa ofisi zao leo jijini Dodoma ili kuweka mkakati wa kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa hivi karibuni ya kuboresha maadili katika utumishi wa umma.


Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi, Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi akiwasilisha mpango kazi wa namna Taasisi yake itakavyotekeleza maelekezo ya ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha maadili katika utumishi wa umma.


Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bi. Neema Mwakalyelye akiwasilisha mpango kazi wa namna ya kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais katika mapambano dhidi ya rushwa wakati wa kikao kazi leo jijini Dodoma cha kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa hivi karibuni ya kuboresha maadili katika utumishi wa umma.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Angellah Kairuki wakifuatilia taarifa ya mpango kazi iliyokuwa ikiwasilishwa na Watendaji wa Ofisi zao leo jijini Dodoma juu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha maadili katika utumishi wa umma.

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Angellah Kairuki wakichukua kumbukumbu ya taarifa ya mpango kazi iliyokuwa ikiwasilishwa na Watendaji wa Ofisi zao leo jijini Dodoma juu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha maadili katika utumishi wa umma.

 



 

No comments:

Post a Comment