Na. Veronica Mwafisi-Sikonge na Tabora
Tarehe 09 Julai, 2026
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameisihi Kamati ya
Miradi ya Maendeleo mkoani Tabora kusimamia kwa umakini miradi inayotekelezwa
katika maeneo mbalimbali mkoani humo ili iendane na thamani halisi ya fedha.
Mhe. Kikwete amesema hayo kwa nyakati tofauti
leo tarehe 9 Julai, 2026 katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Halmashauri
ya Wilaya ya Tabora na Manispaa ya Tabora wakati akikagua na kuweka jiwe la
msingi na kuzindua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Tabora.
Amesema katika kuhakikisha nchi inakuwa na
maendeleo kwenye sekta zote, Serikali itaendelea kutoa fedha za miradi ya
maendeleo, hivyo ni jukumu la wasimamizi kusimamia kwa ufasaha ili miradi hiyo
itekelezwe kikamilifu kulingana na fedha inayotolewa.
Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la
msingi katika kituo cha afya cha Igigwa, Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Mhe.
Kikwete amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho na kusema
Serikali inahitaji eneo kubwa ili kujenga majengo mengi zaidi kwa lengo la kuwa
na huduma mbalimbali za afya.
“Kituo hiki cha afya ni kwa ajili ya wagonjwa
wa nje, hivyo tunahitaji eneo kubwa zaidi ili tuweke majengo mengi kwa lengo la
kutoa huduma mbalimbali za afya kwa wananchi,” ameongeza.
Akizungumza katika hatua nyingine mara baada
ya kuzindua majengo ya Shule ya Msingi Kigamboni katika Halmashauri ya Wilaya
ya Tabora, Mhe. Kikwete amesema Sera ya Elimu ni kuhakikisha vijana wanapata
elimu jirani badala ya kutembea umbali mrefu.
Amesema lengo la Serikali ni kupunguza adha
ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kutafuta elimu na ndio maana inajenga shule
jirani ili wapate muda mrefu wa kusoma badala ya kutumia muda huo kutembea.
Aidha, ameongeza kuwa wingi wa majengo
unasaidia kupunguza idadi ya wanafunzi kurundikana kwenye darasa moja na
kuwarahisishia Walimu kufundisha na wanafunzi kupata uelewa.
“Zamani wakati sisi tunasoma, darasa moja
lilikuwa na wanafunzi wengi kwasababu madarasa yalikuwa machache, lakini sasa
hivi madarasa mengi hivyo wanafunzi katika darasa moja hawazidi 45, aidha
Walimu wanapata muda wa kuwa na wanafunzi karibu wanaoweza kuwamudu, wanafunzi
sasa hivi mtake wenyewe kufeli,” ameongeza.
Amesema akiwa ndiye Waziri mwenye dhamana wa
masuala ya Utumishi, atahakikisha anasimamia zoezi la kupatikana kwa Walimu wa
kutosha ili wanafunzi wapate elimu bora.
“Majengo yamejengwa, ni mazuri, hata sehemu
nyingine mjini hakuna majengo kama haya, hivyo wanafunzi muhakikishe mnafanya
vizuri katika masomo yenu, tutaleta Walimu ili watoto wapate elimu bora huku
akisisitiza utunzaji wa majengo hayo ili yadumu muda mrefu.
Suala la usimamizi wa miradi ya maendeleo
amelisisitiza tena wakati akikagua na kuzindua kituo cha afya cha Maili Tano
katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.
“Hongereni kwa kazi nzuri, kikubwa
niwasisitize usimamizi katika miradi hii kama nilivyosema hapo awali, ili
thamani ya fedha ionekane,” ameongeza.
Mhe. Ridhiwani amehitimisha ziara yake kwa
siku ya leo kwa kuzungumza na Wananchi Manispaa ya Tabora ambapo alipata fursa
pia ya kusikiliza changamoto zao kwa
lengo la kuzifanyia kazi.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Ridhiwani Kikwete akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge baada ya kuweka jiwe la msingi
katika kituo cha afya cha Igigwe wakati
wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua na kuzindua utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo mkoani Tabora.
Wananchi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo
pichani) alipokuwa akizungumza nao mara baada ya kuweka jiwe la Msingi katika
kituo cha afya cha Igigwe wakati
wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua na kuzindua utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo mkoani Tabora.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Ridhiwani Kikwete (kushoto) akijadili jambo na Watendaji wa Mkoa wa Tabora baada
ya kukagua na
kuzindua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.
Mwonekano wa Jengo la wagonjwa wa nje (OPD) lililopo katika kituo
cha afya cha Maili Tano, katika Halmashauri
ya Manispaa ya Tabora.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akielekea kukagua jengo la Kitengo cha Tiba na Mionzi wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua na kuzindua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, mkoani Tabora. Wengine ni Viongozi, Watendaji, Madaktari na Wananchi.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Ridhiwani Kikwete akishauri jambo wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga
kukagua na kuzindua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akisalimiana na Katibu Tawala Wilaya ya Tabora, Bi. Asha Churu wakati Waziri huyo ali[powasili katika Halmashauri ya Wilaya Tabora kukagua na kuzindua majengo ya Shule ya Msingi Kigamboni wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Tabora.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akipata maelezo kuhusu
maabara ya kituo cha afya cha Igigwa wakati wa ziara yake ya kikazi
iliyolenga kukagua na kuzindua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Tabora.
Sehemu
ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kigamboni wakimsikilza Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete
(hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi
iliyolenga kukagua na kuzindua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Tabora.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete
akipiga makofi mara baada ya kuzindua kituo cha
afya cha Maili Tano kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora wakati
wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua na kuzindua utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo. Wengine ni Viongozi na Watendaji wa mkoa huo.
Mwonekano wa jengo la Kitengo cha Tiba na Mionzi lililopo katika kituo cha afya cha Maili Tano, katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.
Mwonekano wa jengo la kituo cha afya cha Igigwa kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.
Mwonekano wa jengo la Shule ya Msingi Kigamboni lililopo katika Halmashauri ya Wilaya
ya Tabora









No comments:
Post a Comment