Tuesday, July 7, 2026

MHE. RIDHIWANI AZINDUA NYUMBA ZA WATUMISHI NZEGA ASISITIZA UTENDAJI KAZI

Na. Veronica Mwafisi-Nzega

Tarehe 08 Julai, 2026

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amezindua nyumba mbili za Wakuu wa Idara katika Halmashauri ya Mji Nzega na kuwasisitiza kufanya kazi kwa bidii na weledi katika kuwatumikia wananchi.

 

Mhe. Kikwete ameyasema hayo leo tarehe 08 Julai, 2026 alipokuwa akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji Nzega baada ya kuzindua ujenzi wa nyumba hizo zilizojengwa jirani na ofisi za Halmashauri hiyo.

 

“Tunayoyaona hapa ni ushuhuda tosha kwamba Serikali imekuwa ikiwajali watumishi wake, nyumba hizi zimejengwa kwa ustadi wa hali ya juu, ni nzuri sana, ziko kwenye mazingira mazuri, haya yanatekelezwa ili mfanye kazi kwa bidii,” amesisitiza.

 

Amesema amekuwa akipata barua za mara kwa mara za watumishi wanaoomba uhamisho, “hali hii hainifurahishi hata kidogo na ndio maana Serikali imekuwa ikijitahidi kuweka mazingira mazuri ili mtulie kwenye vituo vyenu vya kazi, ukikaa kwenye nyumba kama hii huwezi kufikiria kuhama,” amesema.

 

Amesema Serikali imekuwa ikishughulikia changamoto mbalimbali za watumishi ili waweze kutoa huduma bora kwa umma, akitolea mfano upandishwaji wa madaraja na malipo ya stahiki mbalimbali, huku akiwasisitiza waajiri kulipa madai ya watumishi na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kuwajali Watumishi wa Umma wakati wote.

 

Ameongeza kuwa, maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha watumishi wanatatuliwa changamoto zinazowakabili ili waweze kuwatumikia wananchi kwa ufasaha, hivyo hakuna sababu ya Waajiri kutoshughulikia changamoto za watumishi.

 

 

Mhe. Kikwete yuko katika ziara ya kikazi ya siku tatu aliyoianza leo mkoani Tabora ambapo ametembelea katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga na Halmashauri ya Mji Nzega kwa lengo la kukagua shughuli za maendeleo katika halmashauri hizo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (aliyevaa shati jeupe) akipiga makofi mara baada ya kuzindua nyumba mbili za Wakuu wa Idara katika Halmashauri ya Mji Nzega wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua na kuzindua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Tabora. Wengine ni Viongozi na Watendaji wa mkoa huo.


Mwonekano wa nyumba mojawapo ya Wakuu wa Idara iliyojengwa katika Halmashauri ya Mji Nzega mkoani Tabora.


Viongozi, Watendaji na Wananchi wa Halmashauri ya Mji Nzega wakishuhudia uzinduzi wa nyumba mbili (hazipo pichani) za Wakuu wa Idara katika Halmashauri hiyo wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete alipozizindua baada ya kuzikagua wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Tabora.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (wapili kutoka kushoto) akifurahia jambo wakati akikagua nyumba za Wakuu wa Idara katika Halmashauri ya Nzega wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua na kuzindua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri hiyo mkoani Tabora. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Tukai.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (aliyevaa shati jeupe meza kuu) akipokea taarifa kuhusu utekelezaji wa ujenzi wa nyumba mbili za Wakuu wa Idara katika Halmashauri ya Nzega wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua na kuzindua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Halmashauri hiyo mkoani Tabora.



No comments:

Post a Comment