Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Tarehe 21 Novemba,
2024
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amewasisitiza watumishi wa umma kote nchini kufanya kazi kwa ushirikiano na
upendo ili kufikia malengo ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Katibu Mkuu Mkomi ameyasema hayo leo tarehe 21.11.2024 ofisini kwake
katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma akiadhimisha siku ya kuzaliwa kwake.
Amesema watumishi wanatumia muda mwingi sana sehemu za kazi kuliko
nyumbani hivyo ni vizuri wakaishi kwa upendo na mshikamano ili kufikia malengo
ya serikali ya kuwahudumia wananchi.
Ameongeza kuwa sehemu ya kazi ambayo haina upendo na ushirikiano kunakuwa
hakuna amani na matokeo yake watumishi hushindwa kufanya kazi kwa ufasaha.
“Mahali pa kazi ndio sehemu ya kujenga upendo na kuleta amani kwa
watumishi wote kwani tusipofanya hivyo tutashindwa kuwahudumia wananchi
kikamilifu na kurudisha nyuma maendeleo ya taifa letu.” Bw. Mkomi amesisitiza.
Katibu
Mkuu Mkomi ametumia fursa hiyo ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake kwa kuwashukuru
Viongozi, Menejimenti na Watumishi wote wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa upendo na ushirikiano ambao wamekuwa
wakimpatia katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala
Bora, Bw. Xavier Daudi amempongeza katibu Mkuu Mkomi kwa kuongeza mwaka
mwingine katika utumishi wa umma na kuwahamasisha
watumishi wa umma wote nchini kufanya kazi kwa umoja jambo ambalo linaleta
amani na upendo katika maeneo ya kazi kama ilivyo kwa Ofisi ya Rais-UTUMISHI.
Naye Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa
Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Bw. Musa Magufuli, amempongeza Katibu Mkuu Mkomi kwa kuongeza mwaka
mwingine na kuahidi kuendeleza upendo na mshikamano kwa watumishi wa Ofisi ya
Rais-UTUMISHI.
No comments:
Post a Comment