Thursday, November 28, 2024

WAZIRI SIMBACHAWENE AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA KARAKANA YA TGFA AMTAKA MKANDARASI KUKAMILISHA UJENZI KWA VIWANGO NA KWA WAKATI

 Na. Veronica Mwafisi-Dar es Salaam

Tarehe 28 Novemba, 2024

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amemtaka Mkandarasi SUMA JKT anayejenga Karakana ya Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) kukamilisha haraka ujenzi wa karakana hiyo na kwa viwango ili ianze kutumika kama ilivyokusudiwa.

Mhe. Simbachawene amesema hayo leo tarehe 28 Novemba, 2024 wakati wa kikao kazi chake na Menejimenti ya TGFA na Mkandarasi SUMA JKT mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa karakana hiyo jijini Dar es Salaam.

“Muongeze nguvu ili kazi ifanyike kwa haraka na kwa viwango kulingana na makubaliano yaliyofikiwa, mjitahidi kwa muda uliobakia, vinavyopaswa kukamilika vikamilike kwa wakati,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.

Aidha, ameisisitiza Menejimenti ya Wakala hiyo kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuhakikisha kazi inafanyika kwa haraka na kukamilika kwa wakati. 

“Nitoe msisitizo kwa Menejimenti ya TGFA kufanya ufuatiliaji wa maendeleo ya ujenzi wa Karakana hii, binafsi nitajitahidi kufuatilia kwa karibu sana kwani tunahitaji ukamilike kwa wakati kama ilivyokusudiwa,” Mhe. Simbachawene ameongeza.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa ujenzi wa kararakana hiyo, Mkurugenzi wa TGFA, Capt. Budodi Budodi amesema, mradi wa Karakana ya Wakala ya Ndege za Serikali umeanza tarehe 7 Mei, 2023 na unarajiwa kukamilika tarehe 6 Mei, 2025.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na Menejimenti ya Wakala ya Ndege za Serikali wakati wa kikao kazi chake na menejimenti hiyo kilicholenga kukagua maendeleo ya ujenzi wa Karakana ya Wakala wa Ndege za Serikali jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (aliyenyoosha kidole) akikagua maendeleo ya ujenzi wa Karakana ya Wakala wa Ndege za Serikali jijini Dar es Salaam. Wengine ni Menejimenti ya Wakala wa Ndege za Serikali.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akitazama mchoro wa Karakana ya Wakala wa Ndege za Serikali wakati alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa Karakana hiyo jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (kushoto) akiteta jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ndege za Serikali Prof. Mhandisi Idrissa Mshoro wakati wa kikao kazi cha Waziri huyo na Menejimenti ya Wakala wa Ndege za Serikali kilicholenga kukagua maendeleo ya ujenzi wa Karakana ya Wakala hiyo jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akielekea kukagua maendeleo ya ujenzi wa Karakana ya Wakala wa Ndege za Serikali jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi wa TGFA, Capt. Budodi Budodi (kulia) akisoma taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Karakana ya Wakala wa Ndege za Serikali wakati wa kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene na Menejimenti ya Wakala hiyo kilicholenga kukagua maendeleo ya ujenzi huo jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisalimiana na Viongozi na Watendaji wa Wakala wa Ndege za Serikali baada ya kuwasili katika eneo hilo kwa lengo la kufanya kikao kazi na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Karakana ya Wakala wa Ndege za Serikali jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (wa pili kutoka kulia) akiteta jambo na Mwakilishi wa Katibu Mkuu-IKULU, Bi. Neema Jamu (wa kwanza kulia). Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ndege za Serikali Prof. Mhandisi Idrissa Mshoro na wa pili kutoka kulia ni Mkurugenzi wa TGFA, Capt. Budodi Budodi.


MHE. SIMBACHAWENE AZINDUA BODI MPYA YA WAKURUGENZI YA TAASISI YA UONGOZI ASISITIZA KUZINGATIA MISINGI IMARA ILIYOWEKWA NA BODI ILIYOPITA

Na. Veronica Mwafisi-Dar es Salaam

Tarehe 28 Novemba, 2024

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amezindua Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Taasisi ya UONGOZI huku akiisisitiza Bodi hiyo kuzingatia misingi thabiti iliyowekwa na Bodi iliyomaliza muda wake ili kufikia malengo ya uanzishwaji wa Taasisi hiyo.

Mhe. Simbachawene amesema Taasisi ya UONGOZI ilianzishwa kama kituo cha kikanda ambacho lengo lake ni kuimarisha uwezo wa viongozi wa Afrika kusimamia maendeleo endelevu ya Bara la Afrika.

Mhe. Simbachawene amezindua Bodi hiyo leo tarehe 28 Novemba, 2024 jijini Dar es Salaam.

Amesema kulingana na wasifu wa wajumbe wa Bodi hiyo mpya ya Wakurugenzi ana imani kuwa italeta mitazamo isiyo na kifani kwa Taasisi ya UONGOZI.

Kutokana na malengo ya uanzishwaji wa Taasisi ya UONGOZI, ni lazima bodi iwe na hadhi ya kimataifa na kutambuliwa jambo ambalo ndilo hitaji la Hati ya Kuanzisha Taasisi hiyo.

Mhe. Simbachawene amewapongeza wajumbe wapya wa Bodi kwa kuaminiwa na kuteuliwa. Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuteua bodi yenye mchanganyiko wa watu wa mataifa mbalimbali na kuamini kuwa itakuwa na kitu kipya ili kufikia malengo ya kuanzishwa kwa taaisi hiyo.

Ameongeza kuwa, Wakurugenzi wa Bodi waliotangulia waliweka misingi ya Taasisi kustawi. “Hivi ndivyo uongozi bora ulivyo. Tunapowapongeza wakurugenzi wapya kwa uteuzi wao unaostahili, tunawashukuru wakurugenzi waliopita kwa kazi nzuri na kwa kutumikia muda wao kwa uadilifu.” Mhe. Simbachawene amesisitiza.

Amesema Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa uongozi na maendeleo ya uongozi katika maendeleo endelevu ya Tanzania na Bara la Afrika na ndio maana imeendelea kuunga mkono maendeleo ya Taasisi ya UONGOZI.

Vile vile ameishukuru Serikali ya Finland kwa kuunga mkono na kushirikiana na Tanzania katika kuiendeleza Taasisi ya UONGOZI kwa kipindi cha miaka kumi na minne iliyopita ambao umechangia mafanikio makubwa ya Taasisi hiyo.

Amesema, pamoja na wadau mbalimbali wanaochangia maendeleo ya Taasisi ya UONGOZI Serikali ya Tanzania na Finland zimechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taasisi hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya UONGOZI, Balozi Ombeni Sefue amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaamini na kuwateua katika bodi hiyo na amemshukuru Waziri Simbachawene kwa kuwazindulia Bodi hiyo.

Balozi Sefue, amesema bodi hiyo ambayo ni ya tano itaendeleza kazi ya bodi iliyomaliza muda wake ambayo iliweka mkakati wa muda mrefu unaoongoza kazi ya taasisi na mkakati huo una Idhini ya Serikali, hivyo inachukua pale walipoachia bodi iliyopita kuhakikisha mkati unatekelezwa na kufikia malengo ya taasisi. 


Sehemu ya Wakurugenzi wa Bodi mpya ya Taasisi ya UONGOZI wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo uliofanyika Jijini Dar es Salaam.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya UONGOZI, Balozi Ombeni Sefue akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) baada ya Waziri huyo kuzindua Bodi hiyo Jijini Dar es Salaam.


Sehemu ya Wakurugenzi wa Bodi mpya ya Taasisi ya UONGOZI wakijadili jambo wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo uliofanyika Jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (katikati) akitazama baadhi ya Nyaraka kabla ya kuzindua Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Taasisi ya UONGOZI Jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar, Mhandisi Zena Said, kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Balozi Ombeni Sefue. Wa kwanza kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo na wa kwanza kulia ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu-IKULU, Bi. Neema Jamu.


Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI Bw. Kadari Singo akitoa maelezo ya awali kuhusu Taasisi ya UONGOZI kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kuzindua Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Taasisi ya UONGOZI Jijini Dar es Salaam.


Sehemu ya washiriki waliohudhuria uzinduzi wa Bodi mpya ya Taasisi ya UONGOZI wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Jijini Dar es Salaam.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakurugenzi wa Bodi mpya ya Taasisi ya UONGOZI baada ya kuzindua bodi hiyo Jijini Dar es Salaam. Wengine ni Watendaji na Viongozi mbalimbali.

 


Tuesday, November 26, 2024

MHE. SIMBACHAWENE ASISITIZA WATUMISHI WA UMMA NA WATANZANIA WALIOJIANDIKISHA KUPIGA KURA KUJITOKEZA KUCHAGUA VIONGOZI WA SERIKALI ZA MITAA TAREHE 27.11.2024

 Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 26 Novemba, 2024

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewasisitiza Watumishi wa Umma na Watanzania wote waliojiandikisha kupiga kura kujitokeza kufanya uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika kesho tarehe 27 Novemba, 2024 Tanzania Bara.

Mhe. Simbachawene ametoa rai hiyo leo akiwa Ofisini kwake katika Mji wa Serikali, Mtumba, Jijini Dodoma.

Mhe. Simbachawene amesema, zoezi la kesho ni la kihistoria katika nchi yetu hivyo kila Mtanzania mwenye sifa wakiwemo Watumishi wa Umma wote ni muhimu wakashiriki katika kuwachagua Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.

 

“Kwa kuwa zoezi hili ni la kikatiba, nikiwa ndiye Waziri mwenye dhamana ya kusimamia masuala ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ninatoa rai kwa Watumishi wote wa Umma na wananchi wote waliojiandikisha kujitokeza kupiga kura ili kuchagua viongozi bora kwa maendeleo ya taifa letu.” Mhe. Simbachawene amesisitiza.

Ameongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza siku ya Jumatano tarehe 27 Novemba, 2024 kuwa ni siku ya mapumziko ili kutoa nafasi kwa watumishi wote kwenda kupiga kura. Hivyo, Watumishi wa umma kutokushiriki kwenye mambo muhimu ya kikatiba ni upungufu katika kutekeleza majukumu ya kiutumishi, hivyo amewasisitiza kwenda kupiga kura bila kupuuza.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisisitiza Watumishi wa Umma na Watanzania kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.


Monday, November 25, 2024

OFISI YA RAIS - UTUMISHI YAENDELEA KUTOA MAFUNZO ELEKEZI KWA WATUMISHI WAKE IKISISITIZA UTOAJI WA HUDUMA BORA

 Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

25 Novemba, 2024

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeendelea kutoa mafunzo elekezi kwa watumishi wa ofisi yake kwa lengo la kuboresha utendaji kazi ili kuwawezesha watumishi hao kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau mbalimbali wa Serikali.

Akiwasilisha mada kuhusu Huduma kwa Mteja, Afisa Utumishi Mwandamizi kutoka Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Emmanuel Luvanda amesema malengo ya Utumishi wa Umma ni kuwahudumia wananchi kwa kiwango cha hali ya juu, hivyo kila mtumishi ni vizuri akawajibika kikamilifu ili kufikia malengo hayo.

Bw. Luvanda ameongeza kuwa, kwa kuendelea kuwajibika kwa wananchi kwa kutoa huduma bora kwao kunawafanya wawe na imani kubwa na Serikali yao.

Aidha, Bw. Luvanda amewashauri watumishi wa Ofisi hiyo kutumia changamoto mbalimbali kama fursa ya kujifunza na kuona namna ya kutatua changamoto hizo na kuleta maboresho yenye ufanisi mkubwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bw. Musa Magufuli ametoa wito kwa watumishi wa ofisi hiyo kuwahudumia wadau wote wanaohitaji huduma katika ofisi hiyo kwa kuzingatia misingi ya huduma bora ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi pamoja na kujenga taswira nzuri ya ofisi.

Mafunzo hayo elekezi ni utaratibu uliowekwa na Ofisi hiyo kwa lengo la kutoa uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya Utumishi wa Umma ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Musa Magufuli (aliyenyoosha mkono) akizungumza baada ya kumalizika mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa ofisi hiyo yaliyofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.


Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi hao katika masuala ya utendaji kazi yaliyofanyika katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.


Sehemu ya Wakurugenzi na Wakurugenzi wasaidizi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora wakimsikiliza Afisa Utumishi Mwandamizi kutoka ofisi hiyo Bw. Emmanuel Luvanda (hayupo pichani) wakati akifanya wasilisho kuhusu Huduma kwa Mteja walipokuwa kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo katika masuala ya utendaji kazi.


Afisa Utumishi Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Emmanuel Luvanda (aliyesimama) akiwasilisha mada kuhusu Huduma kwa Mteja wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora yaliyofanyika katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.


Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi hao katika masuala ya utendaji kazi yaliyofanyika katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.


Mtumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bi. Zena Makaye (aliyesimama) akichangia hoja wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi hao katika utendaji kazi yaliyofanyika katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.


Mtumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Baraka Kilagu (aliyesimama) akiwasilisha hoja wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi hao katika utendaji kazi yaliyofanyika katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.


Thursday, November 21, 2024

KATIBU MKUU MKOMI AWASISITIZA WATUMISHI WA UMMA KUFANYA KAZI KWA UPENDO NA USHIRIKIANO

 
Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 21 Novemba, 2024

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw.  Juma Mkomi amewasisitiza watumishi wa umma kote nchini kufanya kazi kwa ushirikiano na upendo ili kufikia malengo ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Katibu Mkuu Mkomi ameyasema hayo leo tarehe 21.11.2024 ofisini kwake katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma akiadhimisha siku ya kuzaliwa kwake.

Amesema watumishi wanatumia muda mwingi sana sehemu za kazi kuliko nyumbani hivyo ni vizuri wakaishi kwa upendo na mshikamano ili kufikia malengo ya serikali ya kuwahudumia wananchi.

Ameongeza kuwa sehemu ya kazi ambayo haina upendo na ushirikiano kunakuwa hakuna amani na matokeo yake watumishi hushindwa kufanya kazi kwa ufasaha.

“Mahali pa kazi ndio sehemu ya kujenga upendo na kuleta amani kwa watumishi wote kwani tusipofanya hivyo tutashindwa kuwahudumia wananchi kikamilifu na kurudisha nyuma maendeleo ya taifa letu.” Bw. Mkomi amesisitiza.

Katibu Mkuu Mkomi ametumia fursa hiyo ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake kwa kuwashukuru Viongozi, Menejimenti na Watumishi wote wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa upendo na ushirikiano ambao wamekuwa wakimpatia katika utekelezaji wa majukumu yake.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amempongeza katibu Mkuu Mkomi kwa kuongeza mwaka mwingine katika utumishi wa umma na kuwahamasisha watumishi wa umma wote nchini kufanya kazi kwa umoja jambo ambalo linaleta amani na upendo katika maeneo ya kazi kama ilivyo kwa Ofisi ya Rais-UTUMISHI.

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Musa Magufuli, amempongeza Katibu Mkuu Mkomi kwa kuongeza mwaka mwingine na kuahidi kuendeleza upendo na mshikamano kwa watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI.



 

 


Wednesday, November 20, 2024

KATIBU MKUU MKOMI AHIMIZA VIONGOZI KATIKA UTUMISHI WA UMMA KUZINGATIA UADILIFU WAKATI WA UJAZAJI FOMU ZA TAMKO LA RASILIMALI NA MADENI

 Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 20 Novemba, 2024

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi amewahimiza Viongozi katika Utumishi wa Umma kuzingatia uadilifu wakati wa ujazaji wa fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa masilahi mapana ya taifa.

Katibu Mkuu Mkomi ameyasema hayo leo tarehe 13 Novemba, 2024 wakati wa mafunzo ya ujazaji wa fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya kielektroniki yaliyotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa Menejimenti na Wakurugenzi Wasaidizi wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika Ofisi ya Mtumba jijini Dodoma.

“Nilitoa maelekezo ya kupewa mafunzo, niwapongeze waratibu wa Ofisi yangu na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuitikia wito wa kuja kutupatia mafunzo haya muhimu ya ujazaji wa fomu hizi kwa njia ya kielektroniki,” Bw. Mkomi amesisitiza.

Amesema mafunzo haya ni muhimu kwasababu viongozi walizoea kujaza kwa njia ya karatasi, hivyo ni vema wakafundishwa namna ya kujaza ili waweze kujaza kwa ufasaha.

“Mafunzo haya ni muhimu na yenye tija, tuwasikilize kwa makini wakufunzi wetu ili tuweze kujaza kwa ufasaha na kuwa wakweli kwani tukidanganya mifumo itatuumbua kwa kuwa sasa mifumo mbalimbali inasomana,” Bw. Mkomi amesisitiza.

Ameipongeza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuanzisha ujazaji wa fomu za matamko kwa njia ya kieletroniki na kuwasisitiza kutoa uelewa kwa taasisi za Serikali ili wasipate changamoto katika ujazaji.

“Kwa kuwa mfumo huu wa ujazaji ni mpya, basi ingekuwa ni vizuri mkajipanga kwa kushirikiana na Idara yangu ya Uendelezaji Maadili ili kutoa elimu ya namna ya kujaza.” Katibu Mkuu Mkomi ameongeza.

Awali Katibu wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Bw. Waziri Kipacha amesema ujazaji wa Tamko la Rasilimali na Madeni ni takwa la kisheria kwa mujibu wa Kifungu cha 9 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Ameongea kuwa, kwa Viongozi wote ambao wametajwa kwenye Fungu la 4 la Sheria ya Maadili wa Viongozi wa Umma pamoja na Marekebisho ya Orodha ya Viongozi ambayo yalifanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Tangazo la Serikali Namba 856 lililoorodhesha viongozi wote wa umma wanaowajibika chini ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, wanawajibika kutoa tamko kuhusu rasilimali na madeni yao.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi akizungumza wakati wa mafunzo ya ujazaji wa fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya kielektroniki yaliyotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa Menejimenti na Wakurugenzi Wasaidizi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika Ofisi ya Mtumba jijini Dodoma.


Sehemu ya Menejimenti na Wakurugenzi Wasaidizi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi alipokuwa akizungumza nao kabla ya kuanza kwa mafunzo ya ujazaji wa fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya kielektroniki yaliyotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa Menejimenti hiyo  katika Ofisi ya Mtumba jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maadili, Bi. Leila Mavika akielezea malengo ya mafunzo ya ujazaji wa fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya kielektroniki yaliyotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa Menejimenti na Wakurugenzi Wasaidizi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika Ofisi ya Mtumba jijini Dodoma.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi (kulia) akifuatilia mafunzo ya ujazaji wa fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya kielektroniki yaliyotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa Menejimenti na Wakurugenzi Wasaidizi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika Ofisi ya Mtumba jijini Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa ofisi hiyo Bw. Xavier Daudi.


Baadhi ya Menejimenti na Wakurugenzi Wasaidizi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifuatilia mafunzo ya ujazaji wa fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya kielektroniki yaliyotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa Menejimenti hiyo katika Ofisi ya Mtumba jijini Dodoma.


Katibu wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Bw. Waziri Kipacha akifafanua jambo kwa Menejimenti na Wakurugenzi Wasaidizi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakati wa mafunzo ya ujazaji wa fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya kielektroniki yaliyotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa Menejimenti hiyo katika Ofisi iliyopo Mtumba jijini Dodoma.


Sehemu ya Menejimenti na Wakurugenzi Wasaidizi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakifuatilia mafunzo ya ujazaji wa fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya kielektroniki yaliyotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa Menejimenti hiyo katika Ofisi ya Mtumba jijini Dodoma.


Afisa Tehama, kutoka Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Bw. Musa Mwakasambala akitoa mafunzo kwa Menejimenti na Wakurugenzi Wasaidizi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora namna ya ujazaji wa fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya kielektroniki yaliyotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa Menejimenti hiyo jijini Dodoma.


Sehemu ya Menejimenti na Wakurugenzi Wasaidizi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi alipokuwa akizungumza nao kabla ya kuanza kwa mafunzo ya ujazaji wa fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya kielektroniki yaliyotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa Menejimenti hiyo katika Ofisi ya Mtumba jijini Dodoma.